Afrika yatakiwa kuungana kudhibiti ubora, kuongeza ushindani wa biashara

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali za Afrika zina kila sababu ya kuunga mkono viwanda vidogovidogo na vya kati, ili kuweka mazingira mazuri kwa lengo la kuviboresha na kuleta maendeleo na mapinduzi ya viwanda Afrika.

Pia, zinapaswa kuimarisha ushindani wa kibiashara pamoja na kuleta mageuzi ya sera, teknolojia za kisasa na kujenga uwezo, mazingira ya udhibiti wa ubora wa biashara Afrika.

Rais Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Juni 25, 2025, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, alipomwakilisha katika ufunguzi wa mkutano wa 31 wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO) mjini Unguja.

“Hatua hizi zitasaidia kushughulikia changamoto kubwa za kiuchumi na kuboresha biashara Afrika,” amesema.

Amesema jukumu kuu la viwango katika kuwezesha matumizi ya viwango kwenye biashara kati ya nchi za Afrika ni kukuza usalama wa watumiaji na kuimarisha ushindani wa viwanda Afrika.

“Ni wazi mikusanyiko kama hii ni majukwaa muhimu kwa kubadilishana mawazo, kusimamia miongozo ya viwango Afrika. Kwa vile tunakutana hapa leo, tukumbuke kwamba viwango vilivyoainishwa ni muhimu si kwa kuwezesha biashara tu, bali pia kwa upatikanaji wa masoko ya haki na kusaidia taasisi zetu ndogo na za daraja la kati,” amesema.

Pamoja na kuimarisha ushindani, amesema nchi za Afrika zinatakiwa kuunganisha mifumo ya uthibiti kwa ufanisi wa bidhaa bora.

Amesema ipo haja ya baraza kuu la biashara kusisitiza umuhimu wa biashara ya haki, ambayo ni ushirikiano wa kibiashara uliotokana na mazungumzo katika mikutano mbalimbali ya viongozi wakuu wa Afrika na mifumo mbalimbali iliyowekwa katika kurahisisha biashara.

“Lengo ni kukuza usawa katika biashara za kitaifa, kanda na kimataifa kwa kuhakikisha wazalishaji wa Afrika, hasa wadogo na wa daraja la kati (SMEs), wanapata bei nzuri na uhakika wa maisha ya bidhaa zao,” amesema Dk Mwinyi.

Kuhusu kupata masoko ya nje, amesema mashirika ya viwango yanapaswa kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa lazima utimize mahitaji ya ubora, usalama na kuaminika kwa mashirika ya viwango yaliyopo Afrika.

“Ni lazima tuendelee kufanya kazi pamoja kuunganisha mifumo ya uthibiti ya Afrika kwa ufanisi, na kusaidia ushindani wa bara letu la Afrika,” amesema.

Kadhalika, amesema umuhimu pia utolewe kurahisisha mifumo ya udhibiti ya Afrika juu ya kuwa na viwango, vyeti na kanuni sawa chini ya Umoja wa Viwango Afrika (ARSO) na Miundombinu ya Ubora wa Pan-Afrika (PAQI).

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, Afrika ipo mkiani katika mnyororo wa thamani, kutokana na kuchangia asilimia 1.9 ya thamani iliyoongezwa katika uzalishaji duniani kote.

Hata hivyo, amesema manufaa ya kiuchumi ya muda mrefu yapo katika kufungua mnyororo wa maeneo muhimu ya uwezo wa maadili ya kikanda kama usindikaji wa mazao ya kilimo, magari, nguo na ngozi, madini na dawa.

“Sekta hizi ni muhimu katika kukuza biashara na viwanda. Katika mabadiliko haya, viwanda vidogo vidogo na vya daraja la kati vina jukumu muhimu la kuwa na viwango ili kupata mafanikio,” amesema.

Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Shaaban, amesema wana ndoto ya kuwa na soko la Afrika lisilokuwa na vikwazo, ambapo bidhaa na huduma zitathaminiwa na kutambulika kiuhakika.

“Viwango vinavyotumika ni silaha yetu katika ushindani. Kupitia mkutano huu, tumechangamkia hatua madhubuti za kuufikia malengo haya. Tunaamini kuwa kupitia ARSO, tutaweka misingi imara ya usalama, ubora na matumaini ya ukuaji endelevu,” amesema.

Rais wa ARSO, Profesa Alex Dodoo, amesema Bara la Afrika linakuwa kwa kasi na idadi ya watu inaongezeka, kwa hiyo ni wakati wa mataifa hayo kutembea pamoja, si tu kuyafikia masoko ya Afrika bali pia kujipanua zaidi kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Ashura Katunzi, amesema licha ya kila nchi kuwa na sheria zake, wanatumia miongozo kuhakikisha usalama wa ubora wa bidhaa unazingatiwa.

“Mbali na sheria, lakini tunapotumia miongozo hii tunapata ubora wa bidhaa zinazokubalika. Kwa hiyo, ndiyo maana tunakuwa na vikao hivi ili kuendeleza makubaliano haya, na hiki ni kikao cha 31,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS), Yussuph Majid Nassor, amesema huo ni mkutano mkubwa kuwahi kutokea, kwani zimehudhuria nchi zote 54 kukiwa na washiriki zaidi ya 500. Hivyo ni fursa kwa Zanzibar kuendelea kujitangaza kimataifa.

Related Posts