Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu Damian Nyanga (42) kifungo cha nje cha miezi 12, kutofanya kosa lolote la jinai, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa akimiliki vipande vya meno ya tembo na kiboko bila kibali.
Pia mahakama hiyo imemuamuru Nyanga kulipa fidia ya Sh8 milioni kupitia mkataba wa makubaliano (plea bargaining) aliouingia kwa ajili ya kumaliza kesi hiyo kwa njia ya majadiliano.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Jumatano Julai 25, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, baada ya mshtakiwa kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ya kumaliza kesi yake.
Nyanga na wenzake watatu, ambao hawajafanya majadiliano na DPP, wanakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukutwa na vipande saba vya meno ya tembo na vipande saba vya meno ya kiboko, vyote vikiwa na thamani ya Sh41 milioni.
Mshtakiwa huyo na wenzake wanadaiwa kukutwa na nyara hizo za Serikali bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo amefanikiwa kulipa fidia hiyo.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Erick Kamala aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa baada ya kufanya majadiliano na DPP, alikiri makosa na kuomba kupunguziwa adhabu.
Hivyo, alifutiwa shtaka moja la kuongoza genge la uhalifu na kubaki na mashtaka mawili ya kukutwa na nyara za Serikali.
Kamala, baada ya kutoa taarifa hiyo, alisoma mkataba wa majadiliano mahakamani hapo.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mwankuga alisema mshtakiwa ametiwa hatiani katika mashtaka hayo mawili.
“Pamoja na kuingia makubaliano na mkurugenzi wa mashtaka nchini, mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kutoa adhabu,” amesema Hakimu Mwankuga.
Baada ya kutiwa hatiani, upande wa mashtaka ulidai kuwa hauna kumbukumbu ya makosa ya jinai kwa mshtakiwa, hivyo ukaomba mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ana familia inayomtegemea na mama yake mzazi ni mgonjwa.
“Mheshimiwa Hakimu, naomba mahakama yako inipunguzie adhabu kwa sababu mama yangu ni mgonjwa, nina mke na watoto wanaonitegemea, na mimi afya yangu haiko vizuri,” amedai Nyanga.
Hakimu Mwankuga baada ya kusikiliza shafaa za mshtakiwa na ombi la upande wa mashtaka, alisema mahakama imezingatia hoja zote na inampa adhabu ya kifungo cha nje cha miezi 12 kwa kila kosa, na adhabu hizo zitaendeshwa kwa pamoja.
“Kwa kuwa mshtakiwa ni mkosefu wa mara ya kwanza na amekiri kwa hiyari yake mwenyewe kwa kufanya majadiliano na mkurugenzi wa mashtaka, na kutoa ushirikiano kwa upande wa mashtaka na kuipunguzia mahakama muda na gharama za kuendesha kesi hii.
“Hivyo ninakuhukumu kila shtaka kifungo cha nje cha miezi 12 kwa kutokufanya kosa lolote la jinai katika kipindi hicho,” amesema Hakimu Mwankuga.
Mwankuga amefafanua kuwa adhabu zote zitaendeshwa kwa pamoja, hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha nje cha miezi 12 kwa kutokufanya kosa lolote la jinai kwa kipindi hicho.
“Na ikibainika umefanya kosa la jinai katika kipindi hicho cha adhabu, adhabu uliopaswa kupewa kwa makosa hayo mawili uliotiwa hatiani itatumika kwa mujibu wa sheria,” ameongeza Hakimu Mwankuga.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Nyanga anadaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 16, 2020, eneo la Mbagala.
Inadaiwa siku hiyo na eneo hilo, alikutwa na vipande saba vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola 15,000 za Marekani (sawa na Sh34,293,000) mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia anadaiwa kukutwa na meno saba ya kiboko yenye thamani ya Dola 3,000 (Sh6,858,600) mali ya Serikali.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kukutwa na vipande hivyo bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.
Kwa mara ya kwanza, Nyanga alifikishwa mahakamani hapo Novemba 3, 2020 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 86 ya mwaka 2020 yenye mashtaka hayo.