Baba arejea nyumbani baada ya miaka 60 akiwa mikono mitupu

Nairobi. Boniface Muhandia (99) ndiyo jina linalojadiliwa nchini Kenya kwa sasa baada ya mzee huyo aliyeondoka nyumbani kwake Kijiji cha Eshisari, Mumias Mashariki, Kaunti ya Kakamega kwenda nchini Uganda kutafuta maisha, kurejea akiwa mikono mitupu.
 
Tovuti ya Taifa Leo imeripoti jana kuwa Muhandia ambaye ametimiza miaka 60 bila kuiona familia yake wala kujua kinachoendelea, aliondoka nyumbani kwake mwaka 1965, akiwa na umri wa miaka 39.
Aliondoka akiwa kijana, sasa ni mzee, amerejea nyumbani baada ya ndugu zake kumsaka kwa miaka mingi bila mafanikio jambo lililowafanya wadhani kuwa huenda ameshafariki.

Muhandia amesema amekuwa akiishi Uganda ambako alipata ajira na kuishi maisha mazuri lakini akarejea nyumbani bila mali yoyote.

Baba huyo wa watoto sita amerejea nyumbani kwake mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa na mkongojo na sanduku dogo, akitokea Uganda alikoishi kwa zaidi ya miongo sita.


Hata hivyo, baada ya kuwasili nyumbani ni watu wachache wa familia yake walioweza kumkumbuka.

Baada ya kurejea nyumbani, alikutana na taarifa za majonzi baada ya kuelezwa kuwa mkewe na watoto wake wawili wa kiume walishafariki dunia. Jambo la kushangaza hata watoto wake aliowakuta ilielezwa hawakuweza kumkumbuka baba yao.

Baada ya kuhitimu kama fundi ujenzi, Muhandia hakubahatika kupata kazi jambo lililomlazimu kukimbilia Uganda kutafuta ajira yenye mshahara mzuri utakaoweza kumsaidia kutunza familia yake.

Mzee Muhandia aliyezaliwa mwaka wa 1926, amesema katika safari yake ya kutafuta maisha, alitua katika mji wa Busoga kabla ya kuhamia Jiji la Kampala alikokuwa akiiishi hadi wiki iliyopita alipoamua kurejea nyumbani.

“Nilifanya kazi kwa muda mrefu zaidi jijini Kampala na watu walinipenda kutokana na bidii yangu kwenye kazi. Hii ndiyo maana niliweza kuishi Uganda kwa muda huo wote,” anasema Muhandia.

“Nimerejea nyumbani kuwatafuta ndugu zangu  lakini nimekuta wengi wao walikufa na kuzikwa nikiwa Uganda. Nilijua kwamba ningerudi kujumuika nao  lakini sikujua kwamba ningewakosa baadhi ya watoto wangu na mke wangu,” anasema.


Ingawa mkewe, Kelemendia Adhiambo, alimfuata Uganda mwishoni mwa mwaka 1970, alirejea nyumbani kuwatunza watoto baada ya kukaa kwa muda mfupi katika nchi hiyo jirani.

Akiwa Uganda, alijaliwa kupata watoto wawili, wa kiume na kike. Pia, amerejea nao nchini Kenya.

Watoto wawili wa kiume wa Mzee Muhandia walifariki mwishoni mwa miaka ya 1990 na mkewe alikutwa na mauti miaka miwili iliyopita.

“Ingawa awali nilikuwa nikiwasiliana na familia yangu kwa barua nilizozituma kupitia Shirika la Posta nchini, baadaye nilipoteza mawasiliano nao na ndiyo maana sikupata habari za vifo vya baadhi yao,” anasema.

Mzee Muhandia ambaye alionekana kuchanganyikiwa, hakumbuki mara ya  mwisho alipowasiliana na mkewe marehemu pamoja na watoto wote.

Hata hivyo, familia yake imempokea kwani, mtoto wake wa mwisho, Protus ameahidi kumjengea nyumba.

Related Posts