Iran yawanyonga majasusi watatu wa Israel, yatangaza kuwasaka wengine

Tehran. Iran imetekeleza adhabu ya kuwanyonga majasusi watatu wa Israel waliokuwa wakitumikia kifungo katika Gereza la Urmia Mkoa wa Azerbaijan Magharibi nchini humo, huku Serikali ikitangaza kufanya msako na kuagiza majasusi wengine kama wapo kujisalimisha.

Utekelezaji wa adhabu hiyo umefanyika leo Jumatano Juni 25, 2025 baada ya mahakama nchini Iran kuwakuta raia hao wa Israel na hatia ya kufanya ujasusi nchini Iran ikiwemo kuingia vifaa vya kufanya mashambulizi nchini humo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Serikali la Iran (IRNA), kunyongwa kwa majasusi hao ni adhabu ya pili kutekelezwa tangu kuibuka kwa mgogoro baina ya mataifa hayo Juni 16 mwaka huu. Mgogoro kati ya Israel na Iran ulitulia jana baada ya kudumu kwa siku 13.

Iran iliwatambua wanaume hao waliouawa kwa kunyongwa kama Azad Shojaei, Edris Aali, na Rasoul Ahmad Rasoul ambaye ni raia wa Iraq anayedaiwa kufanya kazi kwa niaba ya Israel.


Adhabu hizo za kunyongwa zilitokea katika Gereza la Urmia, mkoani Azerbaijan Magharibi, ambao ndio mkoa wa kaskazini magharibi wa nchi hiyo. Israel ilipotafutwa na Shirika la Habari la Associated Press kuzungumzia suala hilo haikutoa jibu lolote.

IRNA ilinukuu taarifa ya Idara ya Mahakama ya Iran, ikisema kuwa wanaume hao walikutwa na hatia ya kuingiza nchini humo vifaa vya kutekelezea mauaji kutoka nchini Israel.

Utekelezaji wa adhabu ya kunyongwa raia wa Israel wanaotajwa kuwa majasusi umeibua hofu kutoka kwa wanaharakati kwamba huenda Serikali ikazidisha wimbi la kunyonga watu zaidi baada ya kumalizika kwa mgogoro huo.

Shirika la Amnesty International hapo awali lilieleza hofu kuwa wanaume hao wanaweza kunyongwa wakati wowote hususan ni kipindi hiki ambacho uhusiano kati ya mataifa hayo umetetereka.
Kunyongwa kwao leo kunafanya idadi ya watu waliouawa kwa madai ya ujasusi tangu Juni 16 kufikia sita. 

Wanaharakati wana hofu kwamba watu zaidi wakanyongwa, baada ya utawala wa Iran kutoa muda wa mwisho hadi Jumapili Juni 29, 2025, kwa watu kujisalimisha iwapo wamehusika kufanya ujasusi nchini Iran kwa niaba ya mataifa mengine.

Katika hatua nyingine, watu wasiopungua 28 wameuawa na zaidi ya 1,000 kujeruhiwa katika vita hivyo. 

Kwa mujibu wa Serikali ya Iran watu 606 wameuawa na wengine 5,332 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel nchini humo.

Wakati huohuo, wananchi nchini Iran wameanza kurejea katika maisha ya kawaida wakati huu ambao kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump ya kusema amekubali kusitisha mapigano na Iran inaendelea kutekelezwa.

Misururu ya magari imeanza kuonekana hususan maeneo ya ukingo wa Bahari ya Kaspi na sehemu nyingine za vijijini nje ya mji mkuu, Tehran. Watu hao wanatajwa kuwa ni waliochukua tahadhari ya vita na kuondoka katikati mwa Jiji la Tehran.

Tehran ilikumbwa na mashambulizi makali ya anga kutoka Israel wakati wote wa vita, yakiwemo yale yaliolenga viongozi wa kijeshi wa Iran, miundombinu ya nyuklia na maeneo mengine yanayohusishwa na utawala wa Iran.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari. 
 

Related Posts