Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimetangaza kuwa mchakato wa kumpata mgombea wa urais wa Tanzania kupitia chama hicho, pamoja na kupitisha ilani ya uchaguzi, utafanyika baada ya kukamilika kwa mikutano ya awamu ya pili ya Operesheni C4C.
Kalenda ya kumpata mgombea huyo, imesogezwa mbele kwa mara ya pili mfululizo kwa sababu tofauti, awali mchakato huo ulitakiwa kufanyika Mei 10 na 11, 2025 lakini ulifunikwa kupisha tukio la kuwapokea wanachama wapya (G-55) walioihama Chadema.
Baada ya kuwapokea wanachama hao, chama kilipanga kufanikisha mchakato huo Juni 27 hadi 28 2025.
Hata hivyo, tarehe hizo nazo zimesogezwa mbele, kwa mujibu wa uongozi, kutokana na Kamati Kuu inayopaswa kuandaa ajenda za mkutano huo kutoketi hadi sasa.
Baada ya kuwapokea wanachama hao wapya, walipanga mchakato huo ufanyike Juni 27 hadi 28, 2025, nako pia umesogezwa mbele, kwa kile kinachoelezwa na uongozi kuwa kamati kuu inayopaswa kuandaa ajenda za mkutano haijaketiwa.
Sasa watampata mgombea wao hadi Agosti 3 na 4, 2025 baada operesheni ya C4C iliyozinduliwa jijini Mwanza Juni 3, 2025 yenye lengo la kukiandaa chama hicho kwa Uchaguzi Mkuu itakapo tamati kwa kufika mikoa yote Tanzania.
Ngwe ya pili ya operesheni hiyo inatarajiwa kuendelea kuanzia Julai kwa mikoa ya Kanda ya Kanda ya Nyasa, Kusini, Kati, Pwani na kisha kuvuka maji hadi Zanzibar.
Hatua hiyo ni baada ya kukamilisha ngwe ya kwanza waliyotumia siku 12 kufanya mikutano ya hadhara ya kuongea na umma mikoa iliyopo kanda nne, ikiwamo Victoria, Serengeti, Magharibi na Kaskazini.
Akizungumza na Mwananchi, Leo Jumatano Juni 25,2025, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Salum Mwalimu amesema mchakato wa kumpata mgombea utafanyika baada ya kumaliza ziara ya C4C mzunguko wa pili.
“Ratiba ya mwanzo ya Juni 27 na 28, 2025 tuliikuta wenzetu wamepanga, lakini kutokana na kubadilisha mipango tutatoa kalenda mpya siku chache zijazo baada ya kamati kuu kukaa,” amesema Mwalimu.
Mwalimu amesema hata leo sekretarieti ya chama hicho ilikuwa imeketi kujadili mambo mbalimbali ikiwamo ya ratiba ya ziara hiyo na kupata ofisi zao mpya maeneo ya Mikocheni zitakazokuwa zinamesheheni ofisi za watendaji wote wa chama.
“Sekretarieti inapanga matukio yote hadi uchaguzi mkuu na kutafuta ofisi, kama hivyo imepatikana na tunajipanga na masuala ya kiutawala. Na tumejipanga ndani ya siku mbili hizi tutazungumza na umma,”amesema Mwalimu.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara, Benson Kigaila akizungumzia ratiba ya ngwe ya pili amesema wataanza kumalizia kiporo Mkoa wa Tanga ambao katika mzunguko wa kwanza hawakufanya mkutano kutokana na mbio za mwenge kuingia mkoani hapo.
“Baada ya hapo tutaenda Kanda ya Nyasa, Kusini, Pwani, Kati na Zanzibar tutapita kote huko mapema Julai na baada ya hapo tutarudi Dar es Salaam tayari kwa mkutano mkuu kumpata mgombea urais na kupitisha ilani ya chama chetu,” amesema Kigaila.
Mbali na hivyo, Kigaila amesema mchakato wa kuchukua fomu na kurejesha kwa ngazi ya ubunge na udiwani bado unaendelea tangu siku aliyotangaza katibu mkuu.
“Baada ya muda fulani tutatoka hadharani kuwaeleza tumefikia wapi? Lakini michakato inaendelea ili kuhakikisha wenye nia ya kuwawakilisha wananchi wanachukua fomu za kutangaza nia,”amesema Kigaila.
Kada wa chama hicho, Julius Mwita amesema muda wowote kuanzia sasa anatarajia kuchukua fomu ya kuwania ubunge wa Musoma Mjini, mkoani Mara.
“Nilikuwa nimebanwa na mambo mengi, lakini sasa yamepungua na muda wowote kuanzia sasa nitatoa notisi ya kuchukua fomu, kwa kuwa dirisha bado liko wazi,”amesema.
C4C mbali na kukiandaa chama hicho kwa uchaguzi mkuu, inazunguka mikoa yote kutambulisha safu mpya ya uongozi wa kitaifa, kuziba ombwe la uongozi kwa nafasi zilizowazi kwa ngazi ya mikoa, wilaya na kata.