Mchengerwa atema cheche miradi kuwekwa wazi

Dodoma. Serikali imeagiza Wakurugenzi kote nchi kuweka wazi mikataba ya wakandarasi wanaojenga miradi kwenye maeneo yao kwani kufanya kwa kificho kunapeleka mashaka kwa wananchi na Serikali.

Agizo hilo limetolewa leo Jumatano Juni 25,2025 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Mohamed Mchengerwa wa utiaji saini mikataba ya uboreshaji wa Miundombinu ya miji Tanzania (Tactic) ambapo miji 11 ipo katika miradi 12 iliyosainiwa.

Ujenzi wa miundombinu hiyo unajumuisha stendi mpya, masoko, barabara, mifereji na ujenzi wa kingo za mito pamoja na uwekaji wa taa za barabarani ambapo thamani ya miradi yote ni Sh1.1 trilioni.

Waziri amesema kila Mkurugenzi katika Halmashauri inapaswa kuitisha mikutano ya hadhara kabla mkandarasi hajaanza kazi ili kuwatangazia wananchi.

“Lakini muhimu kuangalia kazi zote ambazo zinawagusa wananchi ambazo hazihitaji utaalamu naagiza wapewe wazawa ili wazifanye na kukipatia kipato,” amesema Mchengerwa.
Waziri ameagiza miradi yote kujengwa kwa viwango vinavyokubalika ili iweze kujiendesha yenyewe lakini ikijengwa chini ya kiwango inaweza kuwa tatizo.

Katika hatua nyingine Mchengerwa ameagiza kunyang’anywa kazi kwa makandarasi wote ambao wamelipwa fedha lakini wakaenda kuzitumia kwenye mradi mingine na kuitelekeza ambayo wamesaini.

Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu amesema mpango wa Tactic utakuwa na maana kubwa kama utasimamiwa kikamilifu kwa kuwashirikisha wananchi.

Ummy ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Tamisemi wakati wa uanzishwaji wa mpango huo, ameiomba Serikali kupitia wataalamu wa Tarura kusimamia ujenzi wa barabara ili ziwe za kiwango kwa kuwezesha zidumu zaidi ambapo italeta maana sahihi.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Mbunge wa Tarime Vijijini Mwita Waitara amesema thamani ya fedha itapatikana tu ikiwa miradi yote itakamilika kwa wakati na kwa thamani inayotakiwa.

Related Posts