Geita. Ni kicheko kwa wauza madini Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya Tume ya Madini kupunguza tozo kutoka asilimia saba zilizokuwa zikitozwa awali hadi kufikia asilimia 4 kwa wachimbaji wote wanaouza madini yao benki hiyo.
Katibu tawala Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wachimbaji wadogo wa madini yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Madini yaliyofanyika Juni 25, 2025 Manispaa ya Geita.
Gombati amewataka wachimbaji wadogo kutumia fursa hiyo ya punguzo la tozo na kusema imelenga kuhamasisha wachimbaji wauze dhahabu zao kwenye viwanda vya uchenjuaji vilivyopo nchini na kwa wale wasiouza BoT watalazimika kulipa tozo zote za asilimia 9.3.
“Uzuri kwenye mkoa wetu tunakiwanda cha uchenjuaji na kwenye soko la dhahabu Geita kuna kituo cha kununulia dhahabu kupitia mpango wa BoT changamkieni fursa hii ili muweze kunufaika”amesema Gombati.
Kwa sasa wachimbaji wanaouza dhahabu kwenye masoko ya dhahabu wanalipa tozo asilimia 9.3 lakini kwa wale watakaouza madini yao kwenye viwanda vya kuchenjua dhahabu vilivyoko chini ya BoT watalipa asilimia 6.3 pekee.
Akizungumzia mafunzo hayo, Gombati amesema Serikali ina imani kubwa na wachimbaji wadogo kwani ni injini katika sekta ya madini na kwamba kwa sasa wachimbaji wadogo wanachangia asilimia 40 ya mapato yatokanayo ya madini nchini hususan dhahabu.
Amesema pamoja na mafanikio hayo bado wachimbaji wadogo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mitaji, mbinu za uchimbaji, masuala ya usalama, uelewa wa sheria na upatikanaji wa masoko.
Kutokana na changamoto hizo Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, Vijana na wenye Ulemavu inatekeleza programu ya kukuza ujuzi ambayo ni mahususi kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inapata ujuzi stahili ili iweze kujiajiri na kuajiriwa.
“Ili tuweze kufanya kazi kwa ufanisi tunapaswa kuwa na ujuzi stahiki ndio maana wameona iko haja ya kukutana na wachimbaji wadogo kutoa mafunzo ili kutoa ujuzi wa vitendo na kitaalamu ili kuboresha uzalishaji, kuimarisha na kuhakikisha usalama kazini na kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria na kuwapa wachimbaji uwezo wa kupata masoko ya uhakika na yenye tija,” amesema Gombati.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ajirana ukuzaji ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Alana Nchimbi amesema mafunzo hayo yamelenga wachimbaji wadogo kutokana na wao kubaini wengi wanaupungufu wa ujuzi wa kutambua miamba yenye madini na aina ya vilipuzi wanavyopaswa kutumia pamoja na uelewa mdogo wa sera na sheria.
Amesema mafunzo hayo ya siku tano yanatolewa kwa wachimbaji wadogo zaidi ya 250 ambao watafundishwa sheria na sera za madini, namna bora ya kutumia vilipuzi na namna ya kutambua miamba yenye madini na namna ya kuongeza thamani ya madini.
“Lengo kubwa ni kuongeza ujuzi kwao kutokana na teknolojia ili waweze kutoka kwenye uchimbaji mdogo kwenda wakati, warasimishe shughuli zao na waboreshe maisha yao na kutengeneza ajira nyingi ili Watanznaia wengi wapate ajira,”amesema Nchimbi.
Mjiolojia Mwandamizi kutoka Wizara ya Madini, Joseph Matalu amesema mafunzo hayo yametolewa na Serikali kuwajengea uwezo wananchi wake, hususan vijana na watu wenye ulemavu, ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwa tija na uendelevu.
Amesema kupitia programu hiyo, washiriki wanapata mafuzo ya ujuzi ya msingi na ya vitendo kuhusu mbinu bora za utafiti uchimbaji na uchenjuaji salama, utunzaji wa mazingira, usimamizi wa afya na usalama kazini, pamoja na matumizi ya teknolojia sahihi katika shughuli za madini.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Wanawake Mkoa wa Geita (Gewoma) amesema uamuzi wa Serikali kupunguza tozo umejibu kilio cha muda mrefu cha wachimbaji wadogo waliokuwa wakilalamikia utitiri wa tozo.
Amesema mafunzo hayo yamewasaidia wachimbaji kujua madhara ya kemikali ya zebaki na kupata elimu ya namna ya kutunza kumbukumbuza fedha ili waweze kukopesheka kwenye taasisi za fedha.