Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinakuwa na amani na umoja wa kitaifa ili kushirikiana kufanikisha hatua nyingine za mageuzi ya kifikra na kutafuta uhuru wa kiuchumi.
Hatua mojawapo, amesema, ni kuhakikisha nchi hizo zinaunganisha watu na kuleta umoja wa kitaifa, ikiwa ni sehemu ya jitihada ya kujitafutia uhuru wa kiuchumi baada ya kupata uhuru kutoka kwa wakoloni.
Rais Samia amesema hayo leo, Jumatano, Juni 25, 2025, alipowahutubia wananchi wa Msumbiji wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa taifa hilo, kufuatia mualiko wa mwenyeji wake, Rais wa nchi hiyo, Daniel Chapo.

Rais Samia, ambaye amewaongoza marais wenzake waliolikwa kwenye sherehe hizo, amesema jitihada za maendeleo zinazofanyika nchini Msumbiji na katika mataifa mengine, zinapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha wananchi wanakuwa na imani na nchi yao.
Lakini pia, waweze kutanguliza maslahi ya nchi kabla ya kwao wenyewe, kulinda na kuhifadhi rasilimali zao kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi.
“Bara letu limefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika hatua ya kwanza ya ukombozi, yaani uhuru wa kisiasa. Tunapaswa kuhakikisha kuwa nchi zetu zinakuwa na amani na umoja wa kitaifa, ili tushirikiane kufanikisha hatua nyingine za mageuzi ya kifikra na kutafuta uhuru wa kiuchumi.
“Leo tumeshuhudia uwepo wa Mwenge wa Uhuru, mwenge ambao umetembezwa nchi nzima kwa nia ya kuwaleta watu pamoja na kuamsha ari ya mshikamano na uzalendo. Kupitia mwenge huu, heshima na matumaini ya wananchi yanakwenda kuamshwa,” amesema Rais Samia.
Hivyo, Rais Samia amesema sherehe kama hizo za uhuru ni ukumbusho wa mapambano ya kutafuta uhuru, haki na usawa.
“Kwa hakika, ni katika nyakati kama hizi sisi, kizazi cha sasa, tunakumbushwa kuhusu namna wazee wetu walivyojitoa mhanga kwa ajili ya kupigania haki ya Waafrika kujitawala,” amesema Rais.

Matukio mbalimbali wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri hiyo, ikiwa ni mwaliko maalum wa Rais wa nchi hiyo, Daniel Francisco Chapo. Sherehe hizi zimefanyika katika Uwanja wa Machava, Mjini Maputo, tarehe Juni 25, 2025.
Amesema licha ya harakati hizo kuigharimu Msumbiji, zipo nchi zilizokuwa mstari wa mbele kuiunga mkono, zikiwamo Botswana, Tanzania na Zambia.
“Ndugu Sergio Vieira, aliyekuwa Katibu wa Hayati Samora Machel, alipata kusema, ‘Tanzania ilifanya kitu cha kishujaa ambacho kisingeweza kufanywa na nchi nyingine. Kulikuwa na kambi Kongwa na Nachingwea, ambako tulitoa mafunzo na kufanya lolote lile. Jeshi la Anga la Ureno lilikuwa likija kila wakati’,” amekumbushia historia.
Hivyo, amesema wakati wanasherehekea miaka 50 ya Uhuru, anatumia fursa hiyo kuipongeza Serikali na wananchi wa Msumbiji kwa mafanikio makubwa waliyoyapata katika kipindi hicho cha nusu karne iliyopita.
Amesema kupitia umoja, kujituma na dhamira njema isiyotetereka, Msumbiji imeinuka kutoka kwenye kivuli cha ukoloni na kujenga mustakabali mpya wa uhuru, heshima na ustawi wa pamoja kwa raia wake.
Katika sherehe hizo, Rais Samia ametangaza kuwa Shirika la Ndege la Tanzania litaanza safari zake kati ya Tanzania na Msumbiji mwishoni mwa mwaka huu.

Amesema hatua hiyo inalenga kufungua fursa zaidi za kibiashara na kiuchumi baina ya wananchi wa mataifa hayo jirani.
“Nina furaha kueleza kuwa, Shirika la Ndege la Tanzania linatarajia kuanza safari za ndege kati ya Tanzania na Msumbiji mwisho wa mwaka huu, hatua itakayoimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya watu wetu,” amesema Rais Samia.
Akumbushia nafasi ya mwanamke
Katika hotuba yake, Rais Samia amesema kuna haja ya kumuinua mwanamke kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Amesema viongozi wa Afrika hawana budi kuendelea kuchukua hatua ya kuwawezesha wanawake na vijana kunufaika zaidi na fursa zitokanazo na utangamano wa kikanda na soko la Afrika kwa ujumla.
“Niwapongeze sana viongozi na wananchi wa Msumbiji kwa hatua kubwa zilizochukuliwa, kama ile ya kuwekeza kwenye miundombinu na huduma za afya zilizochangia kupungua kwa vifo vya wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.
“Umoja wa Afrika umepitisha Itifaki ya AfCFTA ya wanawake na vijana kwenye biashara, inayolenga kujibu baadhi ya changamoto zinazoyakabili makundi haya na kuyazuia wasifaidike na fursa zinazotengenezwa na soko la kikanda,” amesema.
Mataifa hayo mawili yamekuwa na uhusiano wa kihistoria, ambapo Tanzania ilikuwa moja ya hifadhi kwa wakimbizi na wapigania uhuru waliokimbia Msumbiji, na kutafuta nafasi ya kujipanga vyema kukabiliana na wakoloni.
Hali hiyo ndiyo iliwezesha Chama cha Frelimo kuanzishwa jijini Dar es Salaam mwaka 1962.

Katika kuchochea matayarisho ya kupambana na kumng’oa mtawala dhalimu, Tanzania iliweka kambi za kuandaa mikakati na kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wapigania uhuru wa Msumbiji. Kambi za aina hiyo zilikuwepo kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Vilevile, Tanzania ilikuwa ndiyo Makao Makuu ya Jukwaa la Nchi za Mstari wa Mbele (Front Line States), na mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).