Nairobi. Serikali imeamuru vyombo vyote vya habari vinavyoendesha vituo vya televisheni na redio nchini Kenya kusitisha urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya maandamano yanayoendelea nchini humo, huku Chama cha Wahariri nchini humo (KEG) kikikosoa uamuzi huo.
Hatua hiyo imetangazwa leo Jumatano Juni 25, 2025, kupitia taarifa kwa umma ya Tume ya Mawasiliano Kenya (CAK), ikiwa ni saa chache tangu waandamanaji hao maarufu kama ‘Gen Z’ waingie mitaani katika kile kinachotajwa ni kuwakumbuka wenzao waliouawa kwenye maandamano ya Juni 25, 2024.
Pia, imeelezwa awali, Gen Z wanamefanya maandamano hayo kupinga mwenendo wa uongozi na hali ngumu ya maisha nchini humo.
Katika barua kwa vyombo vya habari, CAK imeagiza matangazo hayo ya moja kwa moja kusitishwa mara moja.
Mkurugenzi Mkuu wa CAK, David Mugonyi, kupitia taarifa hiyo, amesema kuwa matangazo ya moja kwa moja ya maandamano yanakiuka Kifungu cha 33 (2) na 34 (1) cha Katiba ya Kenya pamoja na Sehemu ya 461 ya Sheria ya Mawasiliano na Habari ya Kenya ya mwaka 1998.
“Hii ni agizo kwa vituo vyote vya televisheni na redio kusitisha mara moja matangazo yoyote ya moja kwa moja ya maandamano haya. Kushindwa kufuata agizo hili kutaibua hatua za kisheria kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Mawasiliano na Habari ya Kenya, 1998,” imesomeka taarifa hiyo.
Dail Nation imeripoti kuwa baada ya tangazo hilo, KEG imetoa taarifa kwa umma iikiitaka CAK kufuta marufuku hiyo kwa kile ilichodai Ibara ya 33 na 34 ya Katiba ya Kenya inayosemwa imetumiwa na CAK visivyo.
Kauli hiyo ya KEG imetolewa na rais wake, Zubeidah Kananu.
“Uamuzi huu siyo tu kwamba unakiuka kanuni, pia ni ishara ya kuua haki na uhuru wa kujieleza nchini mwetu,” amesema Kananu.
Huku ikinukuu uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu mwaka 2023, kuwa ilitengua na kuzuia CAK kupiga marufuku urushaji wa matangazo ya aina hiyo.