Serikali Zambia yapeleka zuio la mahakama, mazishi ya Lungu yasimamishwa Afrika Kusini

Johannesburg. Mgogoro kuhusu mahali atakapozikwa Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, umechukua sura mpya baada ya Mahakama Kuu ya Afrika Kusini kusitisha mazishi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo, Jumatano.

Familia ya Lungu, ambayo imepinga ushiriki wa Rais wa sasa wa Zambia, Hakainde Hichilema, katika mazishi hayo, imeshindwa kumzika leo, Jumatano, Juni 25, 2025, baada ya Mahakama Kuu ya Afrika Kusini kutoa zuio la muda hadi pale kesi ya msingi iliyofunguliwa na Serikali ya Zambia itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Kesi hiyo ya msingi kuhusu maombi ya Serikali ya Zambia imepangiwa kusikilizwa tena Agosti 4, 2025.

Familia iliamua kutohamisha mazishi yake na kupanga ibada yao ya mazishi pamoja na mazishi ya faragha. Viongozi wakuu wa chama cha kisiasa cha Lungu walisafiri kwenda Afrika Kusini kuhudhuria mazishi.

Serikali ya Zambia, kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wake, Mulilo Kabesha iliwasilisha maombi ya dharura katika Mahakama Kuu ya Afrika Kusini na imefanikiwa kupata amri ya kusitisha mazishi ya faragha ya Rais wa zamani, Lungu, yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo nchini humo.

Maombi hayo yaliwasilishwa kwa dharura dakika za mwisho na yakasikilizwa siku hiyo hiyo ya mazishi.

Kesi hiyo ilisababisha familia ya Lungu kuchelewa kuhudhuria ibada ya mazishi na badala yake kulazimika kufika katika Mahakama Kuu ya Pretoria kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi, wakiwa wamevalia mavazi rasmi ya maombolezo yenye rangi nyeusi.

Mahakama Kuu ya Pretoria iliamua kuwa, baada ya mashauriano, pande zote mbili zilikuwa zimekubaliana kwamba mazishi ya Lungu yasifanyike hadi pale kesi kuhusu mahali atakapozikwa itakapopatiwa uamuzi. Jaji alitaja tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo kuwa Agosti 4, 2025.


Mgogoro huu wa kisheria baina ya Serikali ya Zambia na familia ya Lungu kuhusu mazishi kufanyika Afrika Kusini ni hatua mpya katika mvutano wa karibu mwezi mmoja kuhusu taratibu na mahali sahihi pa maziko ya kiongozi huyo wa zamani.

Serikali ya Zambia inataka marehemu Lungu azikwe kwa heshima za kitaifa nchini humo, lakini familia yake imekataa kuruhusu hilo, wakieleza kuwa ni kutokana na mzozo wa kisiasa uliokuwepo kati yake na Rais wa sasa, Hakainde Hichilema.

Lungu (68) aliyetumikia kama Rais wa Zambia kutoka mwaka 2015 hadi 2021, alifariki dunia Juni 5, 2025, kutokana na ugonjwa ambao hakuelezwa, wakati akipatiwa matibabu katika hospitali moja nchini Afrika Kusini.

Mazishi ya kitaifa yaliyoandaliwa na Serikali ya Zambia yameahirishwa mara mbili kufuatia mvutano unaoendelea kati ya Serikali na familia ya marehemu Lungu.

Familia ya Lungu, kupitia mawakili wao, walidai kuwa marehemu alitoa maelekezo maalumu kwamba Rais Hakainde Hichilema asihudhurie mazishi yake.

Hata hivyo, Serikali ya Zambia ilieleza kuwa Hichilema alikuwa amepangwa kuongoza mazishi hayo ya kitaifa.

Mwanasheria Mkuu wa Zambia, Mulilo Kabesha, aliwasilisha nyaraka mahakamani nchini Afrika Kusini Jumanne, Juni 24, 2025, akiomba amri ya dharura ya kusitisha mazishi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo, Jumatano, Juni 25, 2025, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Utangazaji la Taifa la Zambia (ZNBC).

Maombi ya Serikali ya Zambia katika Mahakama Kuu ya Pretoria yalianza kusikilizwa takriban saa moja kabla ya ibada ya mazishi ya Lungu kuanza. Waombolezaji walifika kwenye ibada kanisani Johannesburg, kilomita 60 (maili 37) mbali wakati kesi ilikuwa ikisikilizwa.

Baadaye ibada ya kumbukumbu ilifanyika, lakini agizo la mahakama lilizuia familia kumzika Rais huyo wa zamani kabla ya uamuzi wa mwisho.

Kabesha amesema baada ya kusikilizwa kwa kesi hiyo kuwa Serikali inatarajia kufikia makubaliano ya kuhamisha mwili wa Lungu nyumbani wiki hii. “Yeye si mkimbizi,” alisema.

Kwa mujibu wa Kabesha, Serikali ilitaka marehemu Lungu azikwe nchini Zambia kwa heshima kamili za kijeshi, kama inavyotakiwa na sheria za nchi hiyo na kwa kuzingatia masilahi ya umma.

Serikali ya Zambia pia ilieleza kuwa tayari imeandaa kaburi kwa ajili ya Lungu katika makaburi ya kitaifa, ambako marais wote wa zamani huzikwa kama sehemu ya utaratibu wa kitaifa.

Aidha, ilisisitiza kuwa matakwa ya mtu binafsi yanapaswa kupisha masilahi ya taifa.

Mgogoro wa Lungu, Hichilema

Lungu na Hichilema walikuwa na historia ndefu ya uhasama wa kisiasa nchini Zambia.

Lungu alimshinda Hichilema katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2016, na Serikali yake ilimfunga gerezani Hichilema kwa miezi minne mwaka 2017 kwa mashtaka ya uhaini kwa sababu msafara wake uliingilia msafara wa Rais.


Hatua ya kumfunga gerezani Hichilema ilikosoolewa na jamii ya kimataifa na Hichilema aliachiwa huru na mashtaka yalifutwa.

Baada ya Hichilema kuchukua madaraka, Lungu alimshutumu mrithi wake kwa kumwandama kwa vitendo ikiwamo kumweka chini ya kifungo cha nyumbani.

Mwaka 2023, polisi walizuia Lungu kutoka kutoka kwa mazoezi ya kukimbia, wakisema ni utendaji wa kisiasa na ilikuwa inahitaji idhini kabla ili kuhakikisha usalama wa umma.

Mke wa Lungu, Esther Lungu na watoto wao wamekabiliwa na mashtaka mbalimbali ya rushwa. Amekana mashtaka ya kuiba magari, ambayo alikuwa anatarajiwa kuyakabili mahakamani wiki hii.

Kuna wakati Lungu alijaribu kurudi kwenye siasa, lakini alizuiwa kuwania tena urais katika uchaguzi. Mahakama ya Katiba ya Zambia iliamua kuwa kipindi alichokuwa rais baada ya kifo cha aliyekuwa rais, Michael Sata, mwaka 2015 kilihesabiwa kama muhula kamili wa kwanza.

Related Posts