Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limefungua milango kwa wawekezaji kutoka sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya nishati ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na nafuu.
Katika kufanikisha hilo, shirika hilo limeanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Tanesco (TIMS), unaomwezesha mwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuona taarifa za miradi ya kuwekeza na kutuma maombi.
Kuanzishwa kwa mfumo huo, kunatoa fursa rasmi kwa watu binafsi kuzalisha umeme na ukaingizwa katika gridi ya Taifa kwa ajili matumizi.
Akizungumzia hilo leo, Jumatano, Juni 25, 2025 Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema mfumo huo umebuniwa kuongeza uwazi, kuimarisha ufanisi na kuchochea uwekezaji zaidi katika la sekta ya nishati kwa maendeleo ya Taifa.
“Katika mfumo huu itaonyeshwa miradi mikubwa inayofaa kuwekezwa na sekta binafsi kutoka ikiwa ni pamoja na miradi ya uzalishaji na usafirishaji,” amesema.
Judith amesema mfumo utaziwezesha taasisi na kampuni binafsi kushiriki kwa urahisi katika miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini ili kuiwezesha sekta binafsi kuwekeza kwa kupunguza urasimu, kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kutoa majibu yanayohusu uwekezaji kwa haraka.
Matumizi ya mifumo ya teknolojia, amesema ndiyo njia mojawapo itakayowezesha kutekelezwa kwa hayo yote.
Kwa sababu Tanzania inapiga hatua katika uwekezaji wa viwanda, amesema na mahitaji ya umeme wa uhakika yanaongezeka.
Kati ya mwaka 2021/25, amesema matumizi ya umeme yameongezeka kwa takriban megawati 700.
Kwa mwaka huu wa fedha 2024/25, amesema sekta ya nishati imechangia asilimia 14.4 katika Pato la Taifa ikiwa ni sekta ya pili baada ya habari na utamaduni.
“Haijawahi kuwa hivyo kwa miaka 10 iliyopita. Yaani tumetoka kuchangia asilimia 5.4 mwaka 2015/20 na sasa tunachangia kiwango hicho,” amesema.
Amesema kuanzishwa kwa mfumo huo ni uthibitisho wa dhamira ya Tanesco ya kushirikiana na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kupatikana umeme wa kutosha, uhakika na gharama nafuu.
Amesema tayari baadhi ya miradi imeshaingizwa kwenye mfumo, hivyo ni wakati wa wawekezaji kuchangamkia fursa.
Amesema wanafanya kazi kuhakikisha wanakuwa na vyanzo zaidi vinavyotosheleza uzalishaji wa umeme.
“Kuzinduliwa kwa mfumo ni ushahidi kuwa Tanesco iko tayari kushirikiana na sekta binafsi ili kuwezesha kupatikana kwa umeme wa uhakika na nafuu,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange ametaja kupunguza urasimu ni miongoni mwa shabaha za kuanzishwa kwa mfumo huo.
Sambamba na hilo, amesema mfumo huo utasaidia kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuongeza hofu kwa wale wenye nia ya kufanya uovu kwa sababu kila kitu kiko wazi.
“Zipo nyakati ambazo ofisi za umma hazisemwi vizuri kutokana na urasimu na mamlaka inaweza kuelekeza lolote kuhusu wewe na vitu vinapokuwa vingi unajikuta unashindwa kuweka taarifa zote kichwani, sasa mfumo huu utasaidia,” amesema.
Kwa mujibu wa Twange, uamuzi wa kuanzisha mfumo huo, pamoja na mambo mengine pia, unalenga kuonyesha kuwa ni shirika la kibiashara, lenye maeneo ya kuwekeza na linawapenda wawekezaji.
Amesema ndani ya mfumo huo, taarifa zote za fursa za uwekezaji zitajumuishwa na hata wawekezaji wataomba kupitia humo kwa kuingiza taarifa zao.
“Mfumo unaongeza uwazi, uwajibikaji na wasiokuwa na mapenzi mema unaleta hofu ya mtu kufanya kisichofaa kwa sababu ya uwazi wa mfumo,” amesema.
Amesema mfumo huo ni muhimu kwa sababu Tanesco ina watu wengi inaotaka kushirikiana nao kuwekeza na utaondoa tabia ya kupiga maneno matupu.
“Tanesco ni taasisi ya kibiashara tunawakaribisha sana tufanye biashara, sisi tutapunguza maneno na kufanya kazi kwa mfumo,” amesema Twange.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Mipango, Utafiti na Uwekezaji, Renatha Ndege amesema kwa sababu ni dhamira ya shirika hilo, kuwaweka karibu wawekezaji, ilihitajika kuwepo mfumo maalumu wa kuongeza ufanisi na uwekezaji.
Ukiacha dhamira hiyo, amesema kuanzishwa kwa mfumo huo pia kumeakisi mkakati wa Tanesco kuendana na matumizi ya teknolojia katika shughuli zake.
Kwa mujibu wa Lenatha, mfumo huo wa kidigitali umetengenezwa na wataalamu wa ndani na jukumu lake ni kuwezesha mawasiliano kati ya Tanesco na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
“Wawekezaji wanaweza kuona miradi ya uwekezaji ya nishati wanayoweza kushirikiana na Tanesco, ili wawekeze. Ndani ya mfumo kutakuwa na taarifa za miradi, pia zile za mwekezaji,” amesema.
Amesisitiza mfumo huo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha nishati Afrika na duniani kwa ujumla.
Akizungumzia umuhimu wa mfumo huo, mmoja wa wawekezaji, Geoffrey Sir amesema inawezekana kwa sababu moja au nyingine kumefanyika mabadiliko ya uongozi ndani ya shirika na anayekuja atahitaji muda zaidi kujiridhisha na maombi ya wawekezaji husika.
Amesema mfumo huo utampa mtendaji hata nafasi ya kujua nini kimefanyika na kupata nafasi ya kufanya uamuzi, hivyo kuwapunguzia wawekezaji muda wa kusubiri.