Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo (TIB) imethibitisha tena dhamira yake ya kuyawezesha makampuni madogo na ya kati (SMEs) kama chachu ya ukuaji wa uchumi, baada ya kusaini mkataba wa mkopo wa Sh30 bilioni na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB).
Fedha hizo ni sehemu ya mgao mpana wa Sh63 bilioni uliotolewa kwa taasisi tatu za Tanzania ili kuimarisha ukuaji wa uchumi, kusaidia viwanda na makampuni madogo na kati (SMEs), na kushughulikia upungufu wa nyumba nchini.
Akizungumza na gazeti mama la The Citizen, mara baada ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo ya Biashara wa TIB, Joseph Chilambo, alisema benki hiyo imekuwa na ajenda ya kimkakati ya kuwawezesha wajasiriamali kupitia upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha.
“SMEs ndio injini halisi ya uchumi wetu wa kitaifa. Zinaajiri idadi kubwa zaidi ya watu na pia ndizo kitovu cha ubunifu,” alisema.
Chilambo alibainisha kuwa hii si mara ya kwanza kwa TIB kupata ufadhili wa aina hii, kwani mikopo ya awali tayari imewafikia walengwa katika sekta mbalimbali za uchumi.
“Utaratibu huu wa sasa wa mikopo ni mpango maalum kwa ajili ya SMEs. Athari kubwa ya makampuni haya hasa katika uundaji wa ajira kwenye sekta kama vile uzalishaji, huduma, miundombinu, na nishati ndiyo ilituchochea kuimarisha msaada wetu,” alieleza
Kwa mujibu wa Chilambo, ingawa mikopo hiyo itakuwa wazi kwa wajasiriamali wote wanaostahiki, kipaumbele kitatolewa kwa vijana na wanawake.
“Kuna juhudi mahsusi ndani ya benki yetu kuhakikisha kwamba wanawake na vijana wajasiriamali wanapata fursa, kukuza biashara zao, na kuchangia kwa maana katika mapato ya taifa,” alisema.
Chilambo aliongeza kuwa dira ya jumla ya TIB ni kusaidia SMEs kukua na kuwa biashara rasmi na endelevu.
“Biashara zilizo rasmi huchangia sana katika uchumi. Tunawahimiza wajasiriamali kusajili kampuni zao na kuweka kumbukumbu sahihi za kifedha ili tuweze kuwasaidia vizuri zaidi,” alisema.
“Kwa hivyo, mkopo huu utatolewa kwa wajasiriamali wenye biashara zilizosajiliwa katika sekta zote za uchumi,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya EADB, Charles Mwamwaja, alisema dhamira ya benki hiyo ni kuchochea maendeleo endelevu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Mikataba hii si tu kwamba inafungua fursa za fedha kwa sekta muhimu, bali pia inaonyesha namna tunavyosikiliza maoni ya wadau na kujibu mahitaji halisi ya uchumi wa nchi wanachama,” alisema.
Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia miradi ya muda mrefu 20–25 katika sekta za kimkakati zinazoendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025, ikiwa ni pamoja na uzalishaji viwandani, utalii, huduma, madini, mali isiyohamishika, na miundombinu.
Kupitia msaada huo maalum, EADB na TIB wanatarajia kuchangia katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kipato cha kati kwa kuimarisha SMEs na kuendeleza maendeleo jumuishi na endelevu.