Hegemony ni nadharia ya dola moja kuongoza nyingine kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Taifa moja linakuwa kiranja wa mataifa mengine duniani.
China, Urusi na Marekani ndiyo wanaopambana kujisimika ukuu wa Hegemony. Kila mmoja anataka awe kiranja wa dunia kiuchumi, kisiasa na kijeshi.
Mipango ya dola moja kuwa kiranja wa dunia haijaanza leo. Karne 4 Kabla ya Ujio wa Kalenda, Ugiriki ya Kale ilitawaliwa na Alexander III wa Macedon, kwa umaarufu zaidi alifahamika kama Alexander the Great.
Alexander aliunda jeshi lake na kutangaza azma yake ya kutawala dunia akitokea Ugiriki, kwamba dunia nzima ingefuata amri zake. Viongozi wa dola nyingine wawe kama magavana, wenye kufuata maagizo yake.
Nyakati hizo Alexander the Great alikuwa anajidanganya tu. Ulimwengu wa kijima wakati huo, angeweza vipi kuifikia dunia yote? Akiwa Ugiriki hakuwa akijua chochote kuhusu nguvu za China na maeneo mengine.
Hata hivyo, Alexander anabaki kuwa mfano hai wa ulimwengu na walimwengu. Ni kipimo cha akili kwa dunia na busara za watu wake. Kwamba nyakati zote tamaa za kutawala dunia zimeendelea kuwepo.
Taifa moja linakuwa na sera ya kutaka kutawala dunia. Wakuu wa mataifa mengine wawe wafuata maagizo. Taifa moja linakuwa na mipango endelevu ya kutawanya mabavu yake ya kijeshi duniani ili kumiliki uchumi wa dunia.
Unapokuwa na uchumi imara pamoja na uwezo mkubwa wa kijeshi, dunia utaielekeza upande wako. Na hapo ndipo kwenye vita kubwa ya China, Marekani na Urusi. Ukraine ipo taabani. Sababu ni Marekani na Urusi. Mataifa makubwa, yana teknolojia na yote yanamiliki nyuklia na nguvu kubwa za kijeshi, kila moja linataka dunia ielekee upande wake.
Mataifa yote hayo yana uchokozi wa ajabu kwa dunia.
Yametengeneza mashushushu ambao wamesambaa ulimwenguni kote. Sababu za uwepo wa mashushushu hao ni maslahi ya nchi hizo.
Marekani, China na Urusi, wanafahamu kuwa ulimwengu wa sasa huwezi kuitawala dunia kwa mtindo wa Adolf Hitler. Dunia ya sasa inataka utawale kwa nguvu za ushawishi, au mamlaka laini.
Kama ambavyo tangu muongo wa nane wa Karne ya 19, baada ya anguko la Dola za Papa (Papal States), nguvu za kijeshi za Kanisa Katoliki zilikoma rasmi. Kuanzia hapo Kanisa Katoliki lilibaki kutegemea mamlaka laini na diplomasia.
Hata Uislam, hizi siyo zama za vita za Jihad na kueneza dini huku damu inavuja, bali ni nyakati za kujenga mtandao wa kufikisha neno na kulitafsiri, wasio Waislam walielewe na kusilimu. Ni soft power!
Ardhi inaharibiwa Israel na Iran, maisha ya watu yanapotea kila siku. Ni kwa sababu matamanio ya kumwaga damu yamekuwa makubwa kuliko diplomasia.
Israel ilianzisha mashambulizi, Iran ikajibu. Marekani ikadai haihusiki. Hata hivyo, baadaye Wamarekani wakashambulia maeneo matatu yenye vinu vya nyuklia Iran.
Halafu, Iran ikaelekeza mashambulizi yake Doha, Qatar, palipo na kambi kuu ya kijeshi ya Al Udeid. Mwaka 1996, Marekani, ilianzisha kambi ya Al Udeid, na kuifanya kuwa kambi yake kuu Mashariki ya Kati. Qatar, wameripoti kuwa makombora 19 ya Iran, yalielekezwa Al Udeid. Mashambulizi hayo ya Iran kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani, yanatafsiri uthabiti wa kiapo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, aliyesema: “Hakuna atakayeishambulia Iran, halafu asijibiwe.”
Kitendo cha Marekani kuishambulia Iran kwenye maeneo yake ya nyuklia; Fordo, Natanz na Isfahan, wakati ilikuwa ikijipambanua kuwa yenyewe siyo sehemu ya mgogoro wa kivita, haina tofauti na ilichofanya Japan, Agosti 1945.
Siku mbili za mauaji, utiaji ulemavu na mateso makubwa, Agosti 6 na 9, 1945, ni kumbukumbu mbaya ya Marekani, kuelekea mwishoni mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Marekani haikuwa nchi iliyopigana vita moja kwa moja, lakini ilirusha nyuklia kwenye miji ya Hiroshima na Nagasaki, Japan.
Kama hoja ilivyojengwa na aliyekuwa Rais wa Marekani, Harry Truman, kuwa mapigo mawili ya nyuklia, Hiroshima na Nagasaki, lengo lilikuwa kuilazimisha Japan kusitisha Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ndivyo Rais wa Marekani, Donald Trump, anavyojipiga kifua baada ya kuishambulia Iran.
Trump sasa anasema pande zote mbili, Iran na Israel, zipo tayari kusitisha mapigano ya kivita. Anaamini kwamba mapigo yake Fordo, Natanz na Isfahan, yalikuwa kuifanya Iran ikose chaguo zaidi ya kukubali mwafaka wa kusitisha vita. Kama Truman, kama Trump.
Uchaguzi Mkuu 2016, Trump, alifanya kampeni akinadi kuwa Marekani ilifanya makosa makubwa kuvamia Iraq, Libya na Syria. Trump alisema, dunia ingekuwa salama kama Saddam Hussein na Muammar Gaddafi, wangekuwa hai, wakiongoza nchi za Iraq na Libya.
Ted Cruz alikuwa anawania tiketi ya kuwa mgombea urais Marekani kupitia Republican, moja ya mambo ambayo aliyapa mstati wa mbele kwenye kampeni zake ni kwamba nchi yake ilifanya makosa kuwavamia Saddam na Gaddafi.
Alisema: “Mashariki ya kati ingekuwa salama zaidi kama Saddam na Gaddafi wangeendelea kuwepo. Kuuawa kwa watu hao wawili kumesababisha machafuko kuwa mabaya. Mashariki ya Kati imekuwa sehemu hatari zaidi ya kuishi.”
Alisema siyo Mashariki ya Kati tu, dunia nzima ingekuwa salama kama Gaddafi na Saddam wangekuwepo. Alisema Marekani ilifanya kosa kubwa kuivamia Syria ili kumng’oa Bashar al-Assad.
Aliulizwa haoni kwamba Saddam na Gaddafi waliua watu wengi, hivyo walistahili kuondolewa? Jibu la Trump liliishutumu nchi yake moja kwa moja kuwa inaua watu wengi hivyo, taifa hilo halina utakatufu.
Kitendo cha Trump kuwa sehemu ya mgogoro wa Iran na Israel, ni sawa na mtu mwenye kulamba matapishi yake.