Dar es Salaam. Baadhi ya vituo vya mafuta vimekuwa vikitumika kama maegesho ya magari, jambo ambalo ni hatari na kinyume cha masharti ya leseni, sheria na kanuni za usalama wa mafuta.
Katika baadhi ya vituo vya mafuta kuanzia saa 2:00 usiku hadi saa 11:00 alfajiri huwapo malori ya mizigo, daladala, teksi, magari binafsi na yale yanayosafirishwa nje ya nchi (IT), baadhi yakiwa yameegeshwa kando mwa pampu za mafuta.
Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli Namba 21 ya mwaka 2015, vituo vya mafuta vinatakiwa kutumika kwa shughuli rasmi pekee kama utoaji wa mafuta, huduma za kiufundi na rejareja kwa kuzingatia usalama na utunzaji wa mazingira.
Mei 17, 2024, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, Hudson Kamoga, ilitoa onyo kwa magari yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi (IT) kuegeshwa katika vituo vya mafuta.
TRA ilisema agizo hilo linatokana na Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2010.
Madereva wanaoegesha magari kwenye vituo hivyo wanadai hufanya hivyo kwa kukosekana maeneo salama ya maegesho na urahisi wa kuanza safari asubuhi, kwa kuwa kwenye vituo hivyo pia hupatikana huduma za kijamii kama vile maji na vyoo.
Idd Kandoro, dereva wa daladala linalofanya safari kati ya Kawe na Segerea, anasema magari mengi yanayoegeshwa kwenye vituo vya mafuta ni ambayo wamiliki hawana sehemu ya kuyahifadhi.
“Mmiliki anaweza kuwa na nyumba lakini eneo alipojenga gari haliwezi kupita. Anakabidhi gari kwa dereva na kumwachia ajue wapi atalilaza, dereva naye hana pa kuegesha, hivyo kituo cha mafuta kinakuwa sehemu pekee salama kwake,” anasema.
Rashid Mansur, ambaye ni dereva wa daladala anasema baadhi ya magari yanayoegeshwa ni mali ya wamiliki wa vituo vya mafuta.
Anasema madereva hupewa maelekezo ya kupeleka magari kwenye vituo hivyo kila siku kuanzia saa 2:00 usiku hadi saa 11:00 alfajiri yanapoondolewa.
“Unakuta mmiliki ana daladala sita, hawezi kuzipeleka nyumbani au kulipia maegesho sehemu nyingine. Akiwa na kituo kikubwa anataka magari yote yalale hapo, hiyo ni sehemu ya bure kwake na salama,” anasema.
Madereva wengine katika maeneo ya Vingunguti, Mburahati na Mbezi wanasema licha ya kufahamu kulaza magari vituo vya mafuta ni hatari, wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa hakuna mahali panapoaminika zaidi.
“Ukiacha gari mtaani, wezi hawana huruma. Wanaweza kufungua na kuiba betri, spika au vifaa vya ndani. Vituoni kuna mwanga, walinzi na watu wanaoingia na kutoka, ni vigumu kuibiwa,” anasema Hamisi Nyundo, dereva wa daladala eneo la Mbezi.
Dereva wa IT, Amani Shirima mkazi wa Kinondoni anasema: “Mteja akinikabidhi gari ili nianze safari kama muda umeenda sana, huwa naona sehemu salama ya kulaza gari ni kituo cha mafuta.”
Anasema magari yanayosafirishwa nje ya nchi yana masharti ya wapi pa kuyalaza, lakini pia kuangalia usalama wake.
Shirima anasema madereva na hata mawakala wanaotoa magari bandarini huona mahali salama pa kuyalaza ni kwenye vituo vya mafuta.
Mussa Mwaikaja, dereva anayefanya safari Rwanda na DR Congo anasema hakuna sheria wala kanuni inayotaka magari kuegeshwa kwenye vituo vya mafuta kwa sababu kuna yadi ambako yanapaswa kuegeshwa.
“Lakini matajiri wanakimbia gharama, hela ya kulaza gari yadi na kwenye kituo cha mafuta ni tofauti, ya kituo cha mafuta ni ndogo, huwa tunawalipa walizi au uongozi wa kituo Sh5,000 tu,” anasema pasipo kutaja bei ya kulaza gari kwenye yadi na masharti yake.
Baadhi ya wasimamizi na walinzi wa vituo vya mafuta wanasema kuna makubaliano ya kibiashara kati yao na wamiliki wa magari yanayoegeshwa hapo.
Daniel Kipenda, msimamizi wa kituo cha mafuta kilichopo Tabata, Dar es Salaam anasema utaratibu wa kulaza magari kwao ni sehemu ya uhusiano wa kibiashara kati yao na wateja wanaojaza mafuta kituoni hapo.
“Tunaruhusu kulaza magari kwa wateja wetu pekee, hizi daladala unazoziona zote zinajaza mafuta hapa. Tulimweleza tajiri kuwa hawa ni wateja wetu na amekubali, tofauti na hivyo wangekwenda sehemu nyingine,” anasema.
Kwa magari madogo yanayolazwa hapo, anasema walinzi hupewa nafasi ya kupata kipato cha ziada nje ya mshahara kwa kutoza fedha.
Hata hivyo, anasema hana ufahamu iwapo kuegesha magari kituoni ni kinyume cha sheria, akieleza mwenye uelewa wa leseni na masharti ya uendeshaji ni mmiliki wa kituo.
Kwa upande wake, Jesca Mrema, meneja wa kituo cha mafuta kilichopo Mbezi, anasema hawaruhusu magari kuegeshwa au kulazwa kituoni kwa kuwa mmiliki amepiga marufuku jambo hilo na ameweka kamera za ulinzi (CCTV) kufuatilia mwenendo wa eneo hilo usiku na mchana.
“Kwetu tumepiga marufuku. Ukiona gari limeegeshwa hapa ni la bosi au limekuja kuweka mafuta na linasubiri huduma fulani. Yale yanayoshusha mafuta usiku ndiyo yanaruhusiwa kwa muda tu, ukionekana umeegesha muda mrefu bosi mwenyewe anapiga simu kuuliza,” anasema.
Katika kituo cha mafuta kilichopo Kinyerezi, mlinzi (jina linahifadhiwa) anasema hupokea Sh2, 000 kwa kila gari dogo linalolazwa hapo usiku.
“Sijui makubaliano yaliyopo, kazi yangu ni kulinda tu, nikiitwa naambiwa nitapewa pesa na wamiliki wa magari madogo niyaangalie kwa karibu,” anasema.
Anasema utaratibu wa malipo hutofautiana, wengine hulipa kwa siku, wiki au mwezi kulingana na sababu ya kulaza gari.
“Wapo wanaolaza kwa sababu hawana maeneo salama, wapo wanaofanya hivyo kwa dharura, huku wengine wakiwa ni waathirika wa mvua kwa kuwa barabara kuelekea kwao hazipitiki,” anasema.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa si msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ofisa mmoja anasema uegeshaji magari kwenye vituo vya mafuta ni ukiukwaji wa masharti ya leseni. Anasema wamiliki wa vituo wanapaswa kuwazuia madereva kulaza magari vituoni.
“Kituo cha mafuta hakipaswi kutumika kama stendi ya magari, wale wanaoruhusu hilo wanavunja sheria na tumeendelea kutoa elimu na maonyo kwa wamiliki wa vituo ili kuhakikisha usalama wa maeneo yao na kuzuia shughuli zisizoruhusiwa,” anasema.
Kwa upande wake Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala katika kukabiliana na hali hiyo, limesema linakuja na mkakati maalumu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu hatari ya magari kuegeshwa vituo vya mafuta.
Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi amesema: “Tutaanza kutoa elimu kwenye vituo vya mafuta, kwa madereva na wamiliki wa magari hapa Ilala. Kisha tutapita maeneo mengine yote nchini. Tunahitaji kueleweka kabla ya kuchukua hatua kali.”
Amesema lengo ni kuzuia majanga kabla hayajatokea, hasa ikizingatiwa kuna ongezeko la magari yanayolala kwenye vituo vya mafuta bila kuzingatia sheria, kanuni wala usalama wa eneo hilo.
Amesema wamiliki wa vituo vya mafuta wanapaswa kuzingatia masharti ya leseni zao ambazo haziruhusu maeneo hayo kutumika kwa shughuli nyingine tofauti na uuzaji mafuta.
“Leseni zao ziko wazi. Vituo hivi havipaswi kubeba mzigo wa maegesho ya usiku wala kuwa maeneo ya malazi kwa madereva. Wanatakiwa kusimamia maeneo yao kwa weledi na kuwazuia wanaoegesha kinyume cha utaratibu,” amesema.
Kamanda Mabusi amesema mpango uliopo ni kutoa elimu ya kina kwa wamiliki wa vituo, madereva na wafanyakazi wake kuhusu namna ya kuzuia majanga ya moto, mbinu za kudhibiti moto endapo utatokea na jinsi ya kutoa taarifa mapema kwa vikosi vya uokoaji.
“Kila mmoja anahitaji kufahamu hatari ya kuendesha injini karibu na pampu, athari za kuacha gari likiwa limewaka kwenye eneo la gesi na umuhimu wa kuwa na vifaa vya kuzima moto. Hii ni elimu ambayo inaweza kuokoa maisha na mali,” anasema.
Baada ya elimu, anasema hatua za ukaguzi wa mara kwa mara zitafuata na watakaobainika kukiuka sheria watachukuliwa hatua.
“Usalama wa eneo la mafuta si wa muuzaji tu, ni wa kila aliye karibu. Tunaomba ushirikiano kwa sababu madhara ya moto hayachagui, yanateketeza kila kitu,” amesema.
Ofisa Madai Mwandamizi wa Kampuni ya Bima ya Tanzindia, Allen Nyange anaeleza ugumu wa kulipa madai endapo ajali imetokea eneo ambalo haliruhusiwi kuegesha kisheria.
“Kama sheria hairuhusu kulaza au kuegesha gari katika kituo cha mafuta, kwa nini mtu afanye hivyo? Labda mteja aseme alikuwa anaingia katika supamaketi ndani ya kituo kununua bidhaa na hakuweza kuegesha barabarani, hapo tunaweza kulipa, lakini tutachukua pia maelezo ya wahusika kuthibitisha,” anasema.
Amesema katika kushughulikia madai ya bima, jambo la kwanza wanaangalia chanzo cha ajali na uwepo wa gari husika eneo ajali ilipotokea wakishirikiana na kamati ya uchunguzi.
Anasema baadhi ya ajali zinasababishwa na uzembe wa madereva, ikiwamo kuyaegesha maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, jambo linaloweza kusababisha kampuni kukataa kulipa fidia.
Nyange ameonya tabia ya baadhi ya wateja kukata bima kubwa lakini hawana mkataba na kampuni ya ulinzi, badala yake wanamlipa mlinzi wa kituo cha mafuta Sh1, 000 ili alinde gari.
Amesema hilo ni hatari kwa kuwa endapo litatokea tukio lolote, hakuna msingi wa kisheria wa kumwajibisha mlinzi huyo.
“Kuna wakati magari yanapata ajali kwenye maeneo yasiyoruhusiwa na tathmini inaonyesha fidia inafikia hadi Sh1 bilioni. Si rahisi kulipa kiasi hicho ikiwa gari liliachwa sehemu isiyo salama,” amesema.