Unguja. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) imesema baada ya kusambaratisha mitandao ya uhalifu na kuziba mianya ya uingizaji wa dawa hizo nchini, kumeibuka biashara haramu na matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya, na kutishia usalama wa afya za watumiaji na jamii.
Hayo yamebainika leo Jumatano, Juni 25, 2025, katika semina ya wadau wa afya ikiwa ni kuelekea katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya ambayo hufanyika Juni 26.
Akizungumza na wadau wa afya, Kamishna Mkuu wa ZDCEA, Kanali Burhani Zuberi Nassoro, amesema kuna haja wadau kujipanga kuondoa mwanya huo wa watu wachache kujinufaisha binafsi, lakini jamii kubwa ikaangamia.
“Tumeona ni vyema kuandaa kikao kazi ili kujadiliana kwa pamoja namna ya kubaini na kudhibiti uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya, na kuweka mkazo katika maduka ya kuuza dawa za binadamu bila ya kuwa na maelekezo ya daktari,” amesema Kamishna huyo.
Amesema imegundulika sasa hivi kuwa dawa tiba zenye asili ya kulevya kama tramadol, valium, zimekuwa mbadala wa dawa za kulevya.
Ikumbukwe kwamba, dawa tiba zenye asili ya kulevya huingizwa nchini kwa shughuli za matibabu ya magonjwa mbalimbali, na inapotumika kinyume huwa mbadala na kuleta matokeo sawa na dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar, katika mwaka 2024 jumla ya mls 8,794 na kilogramu 20 za dawa tiba zenye asili ya kulevya ziliingizwa nchini.
Taarifa zinaonyesha kuwa dawa aina ya Fentanyl inaongoza kwa wingi na inakadiriwa kufikia asilimia 57, ikifuatiwa na Pethidine kwa asilimia 38.
“Mamlaka haiwezi kushinda vita hii peke yake, hivyo ushirikiano wa dhati unahitajika kwa jamii hasa makundi maalumu kwa lengo maalumu kama walimu, wazazi, walezi na Serikali kwa ujumla ili kuweza kunusuru kizazi cha sasa na baadaye,” amesema.
Naye Waziri wa Afya Zanzibar, Ahmed Nassor Mazrui, aliyekuwa mgeni rasmi, amesema baadhi ya dawa tiba hizo huingizwa nchini kihalali na nyingine kinyume na taratibu.
Ametaka wadau kutafuta mwarobaini na kuazimia kukabiliana na tatizo hili linalotishia usalama wa afya za wananchi wetu.
“Tusipochukua hatua madhubuti na thabiti za kuziba mianya ya uchepushwaji na kudhibiti matumizi holela ya dawa tiba zenye asili ya kulevya, Taifa litakosa nguvu kazi kwa mmomonyoko wa maadili na kupotea kwa silka na utamaduni wa Mzanzibari,” amesema