ZEC msifumbie macho malalamiko, fanyieni kazi

Kadri siku zinavyozidi kusogea kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, hali ya kisiasa Zanzibar inaendelea kujaa maswali na sintofahamu. Kama ilivyokuwa katika baadhi ya chaguzi zilizopita tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, kuna viashiria vya dosari na ukosefu wa uwazi katika hatua mbalimbali za maandalizi ya uchaguzi huo.

Baadhi ya matukio yanayozua tashwishi yamejitokeza mapema, likiwemo agizo la mmoja wa wakuu wa mikoa kuwataka watumishi wa umma ndani ya mkoa wake kuwasilisha kadi zao za mpiga kura.

Hili limeibua hofu kuhusu uwazi na usiri wa mchakato wa kupiga kura. Kinachozidisha hofu hiyo ni ukimya wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), hali inayotafsiriwa na wengi kuwa ni ishara ya kuunga mkono au kuridhia jambo hilo.

Pamoja na hayo, kuna malalamiko ya watu wengi kunyimwa vitambulisho vya Uraia wa Zanzibar, hali inayowanyima haki ya msingi ya kushiriki uchaguzi.

Aidha, madai ya baadhi ya watu kuandikishwa zaidi ya mara moja bado hayajafanyiwa kazi ipasavyo, na ukweli utadhihirika pale ZEC itakapotoa orodha rasmi ya wapiga kura, sambamba na uchunguzi huru utakaoainisha iwapo madai hayo yana msingi. Hoja nyingine inayoibua mjadala ni kuhusu uhalali wa baadhi ya vipengele vya sheria ya uchaguzi. Ingawa Katiba ya Zanzibar inasisitiza kuwa uchaguzi wa Rais ufanyike kwa siku moja, imekuwepo sheria inayotoa mwanya wa uchaguzi kufanyika kwa nyakati tofauti. Hadi sasa, ZEC haijatoa maelezo ya kina kuhusu tafsiri ya sheria hiyo na namna inavyohusiana na Katiba.

Sasa tunakaribia kipindi cha kampeni rasmi ambacho kitaendeshwa kwa muda wa mwezi mmoja hadi usiku wa kuamkia siku ya kupiga kura. Ni wakati wa vyama na wagombea kunadi sera zao mbele ya wapiga kura. Hata hivyo, mazingira ya kampeni yanapaswa kuwa huru, sawa na yenye kufuata misingi ya haki ili kuhakikisha kila chama au mgombea anapata fursa ya kweli ya kuwafikia wapiga kura.

Katika chaguzi zilizopita, kumekuwepo malalamiko kuhusu upendeleo kwa chama tawala, ikiwa ni pamoja na kuongezewa muda wa kampeni huku vyama vya upinzani vikikabiliwa na vikwazo vya muda na taratibu. Vitu kama hivyo vinakiuka misingi ya usawa na vinaweza kuvuruga uhalali wa uchaguzi. Kwa mantiki hiyo, mamlaka husika zinapaswa kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa kweli kwa vyama vyote.

Pia kuna changamoto ya matumizi ya rasilimali za serikali kama magari katika kampeni za baadhi ya vyama.

Hili halipaswi kuendelea kwani uchaguzi ni mchakato wa kisiasa na si shughuli ya kiserikali. Vyombo vya usimamizi vinapaswa kudhibiti matumizi ya mali za umma katika shughuli za vyama vya siasa.

Eneo jingine la malalamiko ni katika utoaji wa vibali vya matumizi ya viwanja vya umma kama vile shule na viwanja vya manispaa kwa ajili ya mikutano ya kampeni.

Wakati vyama vingine vinaruhusiwa, vingine hukataliwa kwa visingizio visivyoeleweka. Hali hii inajenga picha ya upendeleo na huondoa imani ya umma katika uadilifu wa mchakato wa uchaguzi.

Kwa nyongeza, kumekuwepo na matukio ya makundi ya wafuasi wa vyama kuvamia viwanja vya mikutano kabla ya muda na kufanya shughuli zisizo rasmi kama kucheza ngoma na kugawa chakula. Vitendo hivi, ambavyo kwa wengine ni uchokozi, vinaweza kusababisha mivutano na hata vurugu. Jeshi la Polisi lina wajibu wa kudhibiti mwenendo huu kwa kuzingatia sheria na kuhakikisha usalama na utulivu vinadumishwa.

Wakati huu wa kampeni ni fursa muhimu kwa wagombea na vyama kuelezea ajenda zao kwa wapiga kura. Vyombo vya habari vya umma vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha vinaendesha shughuli zake kwa uwazi na bila upendeleo.

Hili linamaanisha kutoa nafasi sawa kwa wagombea wote bila kuonyesha upendeleo wa moja kwa moja au wa kificho kwa chama fulani au mgombea fulani.

Aidha, ni muhimu kuwaelimisha wapiga kura juu ya haki zao, umuhimu wa kupiga kura na jinsi ya kushiriki ipasavyo katika uchaguzi. Kwa sasa, Zanzibar haijaonekana kutoa elimu hiyo kwa kiwango cha kuridhisha, hali inayoacha mianya kwa watu kutopiga kura kwa usahihi au kuwa waathirika wa udanganyifu kama kuporwa kadi au kudanganywa ndani ya vituo vya kupigia kura.

Jambo jingine linalohitaji ufafanuzi wa haraka kutoka ZEC ni kuhusu marufuku ya baadhi ya waandishi wa habari kuandika au kupiga picha za matokeo yanayobandikwa vituoni baada ya uchaguzi.

Matokeo hayo si siri, na hivyo ZEC inapaswa kueleza hadharani sababu za hatua hiyo ambayo inahofiwa kuficha ukweli.

Kwa ujumla, kuna haja ya kuhakikisha kuwa kampeni na uchaguzi vinakuwa wa haki, huru na unaozingatia misingi ya kidemokrasia.

Hili linaweza kufanikishwa kwa kuwapa nafasi sawa wagombea, kuepuka matumizi mabaya ya rasilimali za umma, kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa wapiga kura na kutoa taarifa kwa uwazi.

Ni muhimu kwa Zanzibar kujifunza kutokana na changamoto zilizopita ili kujenga mazingira bora zaidi kwa uchaguzi wa mwaka huu.

Related Posts