Tanga. Wakati joto la uchaguzi mkuu 2025 likizidi kupamba moto, Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimeweka wazi msimamo wake kuwa kitakata majina ya watia nia au wagombea wote wanawania udiwani na ubunge watakaobainika kujihusisha na utoaji rushwa.
Chama hicho kimebainisha kuwa kitahakikisha mchakato wote wa kura za maoni katika kata 245 majimbo 12 yaliyopo kwenye wilaya tisa za Mkoa wa Tanga unakuwa huru na kwamba kitasimamia kanuni na taratibu zilizowekwa kwa lengo la kukijengea heshima.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdurahman ametoa msimamo huo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua ukarabati wa jengo la CCM Mkoa wa Tanga.
“Nimeamua kuweka wazi kabisa msimamo wa CCM kuwa hatutamfumbia macho yeyote atakayebainika kujihusisha na rushwa au rafu yoyote wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi ndani ya chama na kwa kuwa mimi ni Mwenyekiti wa CCM Tanga, sitakubali kichafuliwe na yeyote,” amesema Rajabu.
Amesema atahakikisha kila mtia nia na mgombea anatimiza wajibu wake ikiwamo kufuata taratibu na kanuni ili kujenga misingi imara iliyowekwa na waasisi wa chama hicho chenye sifa ndani na nje ya nchi.
Abdurahman amesema mbali ya ukarabati wa jengo la CCM Mkoa wa Tanga ambao umefikia asilimia 90, tayari umeanza utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa ya kila Wilaya ijenge nyumba nne za watumishi wa chama hicho na jumuiya zake.
“Nilielekeza kila wilaya ihakikishe inajenga nyumba nne za watumishi wa chama na jumuiya zake, hadi sasa zipo wilaya ambazo zinakaribia kukamilisha, tutahakikisha ifikapo 2027 CCM katika wilaya zote tisa za Mkoa wa Tanga zina nyumba nne za kisasa za watumishi.
Ameeleza kuridhishwa kwake na hatua iliyofikiwa ya ukarabati wa jengo hilo ambalo linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni.

Meneja mradi wa ukarabati wa jengo hilo lenye ghorofa tatu, Mhandisi Amon Kyando amesema linajengwa na kampuni ya uhandisi ijulikanayo kama Centroid Contractors Ltd.
“Gharama halisi za mradi huu, tutazitoa baada ya kukamilisha lakini kwa sasa limefikia asilimia 95 ambapo kazi zilifoanyika ni urekebishaji wa vyumba, miundombinu ya umeme, maji sakafu, upakaji wa rangi, tunatarajia ifikapo mwishoni mwa Juni, litakamilika,” amesema Kyomo.