Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametoa wito kwa wasafirishaji wote wa mizigo nchini kuhakikisha wanazingatia viwango vya juu vya usalama barabarani.
Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa malori yote yanayofanya shughuli za usafirishaji yamewekewa vifaa muhimu vya usalama, ikiwemo mifumo ya GPS, ili kufuata kikamilifu miongozo na kanuni zilizopo.
Dk Biteko amesema usalama wa barabarani si jukumu la Serikali pekee bali ni wajibu wa kila mdau katika sekta ya usafirishaji, ili kulinda maisha ya watumiaji wa barabara na mali zinazohamishwa.
Aidha, Dk Biteko amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kwa karibu kwa lengo la kuimarisha mazingira bora ya kufanya biashara.

Amesema Serikali imejipanga kuweka sera thabiti na zinazotabirika ambazo si tu zitalinda maslahi ya wafanyabiashara wa ndani, bali pia zitachochea uaminifu na kuvutia wawekezaji wapya kuwekeza nchini.
Dk Biteko ametoa kauli hiyo leo Juni 25, 2025, jijini Dar es Salaam, aliposhiriki maadhimisho ya miaka 30 ya ushirikiano kati ya Kampuni ya Super Star Forwarders (SSF) na Total Energies.
“Leo tumekusanyika hapa kusherehekea miaka 30 ya ushirikiano wa kimkakati kati ya kampuni zetu, Total Energies na Super Star Forwarders.
“Katika kipindi hiki, mmekuwa washirika wakuu wa kimataifa katika usafirishaji wa bidhaa mbalimbali, hasa kwa kutumia matenki maalum. Binafsi nimefurahishwa sana na nawasifia kwa mafanikio haya,” amesema Dk Biteko.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo umewezesha upatikanaji wa mafuta kwa uhakika nchini, kuunda ajira kwa mamia ya vijana, na kuvutia nchi jirani kutumia Bandari ya Dar es Salaam kwa usafirishaji wa mizigo, hivyo kutoa fursa kwa Watanzania.
Pia, Dk Biteko amewapongeza Kampuni za Total Energies na Super Star Forwarders (SSF kwa kufanikisha kufikia viwango vya juu vya usalama katika usafirishaji wa mizigo.
Amesisitiza kuwa kampuni hizo zimekuwa mfano bora wa kuigwa, na kuwahimiza wasafirishaji wengine kufuata nyayo zao ili kuboresha usalama na ufanisi katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka wasafirishaji kuzingatia kwa umakini masuala ya usalama barabarani, akibainisha kuwa suala hilo si suala la sera pekee bali ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwa maslahi ya Taifa.
Amesema ajali za barabarani husababisha hasara kubwa, ikiwemo upotevu wa maisha ya watu na athari kwa uchumi wa nchi.
Profesa Mbarawa ametoa wito kwa wasafirishaji kote nchini kutumia barabara zilizopo kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa, ili kuhakikisha usalama na uendelevu wa miundombinu hiyo.
Pia, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie, amesema maadhimisho hayo ni ya kihistoria kwa Tanzania na Ufaransa, yakibeba uzito wa miaka 30 ya ushirikiano kati ya kampuni za Total Energies na Super Star Forwarders (SSF).
Amesema ushirikiano huo umekuwa na manufaa makubwa, ukiwemo utoaji wa mafunzo kwa madereva na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kuhakikisha usalama barabarani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Super Star Forwarders, Seif Seif, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake madhubuti na jitihada za Serikali katika kuimarisha na kukuza sekta ya usafirishaji nchini.
Makamu wa Rais Mwandamizi wa Total Energies Kanda ya Afrika (Huduma za Masoko), Jean Torres ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji na kwa dhamira yake ya dhati ya kuendeleza sekta ya nishati.