Hizi hapa njia kupambana na selimundu

Dar es Salaam. Utolewaji wa elimu, ugunduzi wa mapema, matibabu na utolewaji wa dawa kwa wakati ni miongoni mwa njia za kupambana na ugonjwa wa Selimundu zilizoainishwa na wataalamu wa afya.

Ugonjwa wa selimundu ni tatizo la muda mrefu kwenye seli nyekundu za damu, ni hali anayozaliwa nayo mtu ikisababisha baadhi ya seli nyekundu za damu kuwa na umbo lisilo la kawaida badala ya kuwa na umbo linalofanana na diski, zinakuwa na umbo kama la nusu mwezi (mwezi mwandamo).

Umbo la nusu mwezi ni kwa sababu zinajumuisha umbo lisilo la kawaida la hemoglobini. Hemoglobini ni dutu iliyo kwenye seli nyekundu za damu ambayo inabeba oksijeni. Umbo la nusu mwezi linasababisha seli nyekundu za damu kuvunjika kwa urahisi na zisitoshe vizuri kwenye mishipa midogo ya damu ili kusafirisha oksijeni.

Takwimu za Selimundu kama ilivyoanishwa wakati wa maadhimisho yaliyofanyika Juni 19, 2025 Serikali kupitia Wizara ya Afya ilisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshika takwimu za juu duniani ikishika nafasi ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ikitanguliwa na Nigeria, India na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.


Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha zaidi ya watoto 300,000 huzaliwa na Sikoseli kila mwaka duniani huku Tanzania peke yake watoto takribani 14,000 huzaliwa na ugonjwa huo kwa mwaka sawa na watoto 14 kati ya kila watoto 1,000.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 26, 2025 kwenye kikaokazi cha ugonjwa wa selimundu kilichowakutanisha wataalamu kutoka nchi 16 kilichoratibiwa na Kituo vya Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge amesema kikundi hicho kimetaka Afrika ijitegemee katika utambuzi wa ugonjwa na utoaji dawa huku ikitakiwa kuachana na misaada.

Dk Kisenge ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya wa Tanzania amesema kikundi kazi hicho kimekuja na njia za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo ikiwemo jinsi ya kuwahudumia wagonjwa, kupunguza ugonjwa huo na uelewa.

“Maumivu makali wanayopata wanaougua ugonjwa huu yanasababisha wengine kutokwenda shuleni, kwa sasahivi Tanzania tunatoa bure dawa zinazosaidia watoto wanaougua,” amesema Dk Kisenge.

Akitaja madhara ya maumivu ya ugonjwa huo amesema unaweza kusababisha madhara kwenye figo, moyo kuchoka hivyo magonjwa anapopatiwa dawa zinamsaidia kama ilivyoazimia kikundi kazi hicho.

Mwenyekiti wa wataalamu wanaopambana na Selimundu Tanzania, Dk Elisha Osati amesema mkutano huo uliofanyikia Tanzania unakuja na mpango wa pamoja wa kukabiliana na ugonjwa huo.

“Asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania wote wanavinasaba vya selimundu na wengine wanaoana bila ya kujua hivyo inasababaisha watoto kuzaliwa wengi. Tatizo hili ni kubwa katika kanda ya ziwa, Pwani maeneo ya kati ya nchi.

“Ili kuzuia usiongezeke, wagonjwa kupatiwa huduma sahihi, watu wapimwe watoto tuwape dawa wasipate maumivu na maambukizi ni jukumu letu sisi kama wataalamu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha tunakuja pamoja ili kukabiliana na ugonjwa huu,” amesema.

Akitaja juhudi za Serikali amesema watoto karibu 20 wamepandikizwa uroto wa mfupa na wamepona ugonjwa huu.

Dk Joseph Lubega, Mkurugenzi wa mpango wa Texas Children’s Global Hope amesema changamoto kubwa moja wapo kwa watoto wa Kiafrika ni Selimundu na umekuwa kwa muda mrefu hivyo juhudi zaidi zinahitajika katika kuwahudumia watoto hawa.

“Tanzania inaonesha juhudi za kuwahudumia wagonjwa ikiwemo kuwapatia dawa bure, mbali na hilo tumekuwa tukishirikiana juu ya maradhi mbalimbali ya watoto,” amesema.

Dk Mohammed Abdulaziz, Mkuu wa kitengo cha kudhibiti magonjwa Africa CDC amesema kukabiliana na selimundu kunapaswa dawa, uchunguzi, huduma, nguvukazi kwaajili ya kuzuia ugonjwa huo.

Neema Mohamed anayeishi na ugonjwa huo akiwa amegunduliwa akiwa na miaka 10 amesema ametumia dawa na kufuata ushauri wa daktari hali iliyomfanya kuishi vizuri hadi sasa akiwa na miaka 34 huku akitoa rai kwa jamii kutonyanyapaa wenye ugonjwa huo.

Je, wazazi wakitibiwa vinasaba watapata mtoto mwenye selimundu

Akizungumza na Mwananchi pembeni ya mkutano huo, Dk Deogratius Soka amesema njia ya msingi ya kuzuia mtoto kuzaliwa na selimundu ni pale wazazi wanapotambua hali zao hivyo hakuna matibabu ya kuondoa kinasaba kwakuwa mtu amezaliwa nacho.


Amesema baba na mama wenye vinasaba vya selimundu wakioana wanauwezekano wa kupata watoto wenye selimundu, wa kawaida au wenye vinasaba kama wao au mchanganyiko.

“Mzazi anapaswa kupata mwenza asiye na kinasaba cha selimundu ndipo watapata mtoto asiye na ugonjwa huo. Sikuhizi kupima ni rahisi sana damu inachukuliwa dakika tano tu unajua,” amesema Dk Soka.

Related Posts