Kesi ya kanisa kumnyang’anya zawadi mtoto wa Askofu Sepeku kuunguruma leo

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi leo Juni 26, 2025 itaendelea na usikilizwaji wa kesi ya ardhi iliyofunguliwa na mtoto wa Askofu John Sepeku, Bernardo Sepeku (63).

Bernado alifungua kesi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes na mwekezaji huyo, Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Katika kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, Bernado ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yao anapinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yao. 

Anaiomba Mahakama iamuru alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.

Pia, anaiomba alipwe  Sh493.65 milioni kama fidia ya hasara ya mazao yaliyoharibiwa katika shamba hilo.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Arafa Msafiri na ipo hatua ya utetezi ambapo wadaiwa katika shauri hilo wameanza kutoa utetezi wao tangu, Juni 4, 2025.

Tayari mashahidi wawili wa upande wa utetezi wameshatoa ushahidi wao kuhusiana na kesi hiyo, baada ya upande wa mlalamikaji kufunga ushahidi wao.

Miongoni mwa mashahidi wa upande wa utetezi waliotoa ushahidi wao mahakamani hapo ni Katibu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Mchungaji George Lawi.

Katika utetezi wake, Lawi akiongozwa na wakili wake, Denis Malamba aliiomba Mahakama ipokee Katiba ya Kanisa hilo ya Mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, iwe sehemu ya ushahidi wake.

Katiba hiyo ilikusudiwa kuwa sehemu ya ushahidi wake katika kuunga mkono ushahidi wake wa maandishi aliouwasilisha mahakamani kwa maandishi pamoja na ufafanuzi alioutoa mahakamani kwa mdomo.

Hata hivyo, Katiba hiyo ilipingwa na mawakili wa madai katika kesi hiyo, Deogratius Butawantemi na Gwamaka Sekela, kutokana na ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika uwasilishaji na upokewaji wa vielelezo mahakamani.

Wakili Butawantemi alipinga Katiba hiyo isipokewe na mahakama kama  kielelezo cha upande wa utetezi kutokana na kuwasilishwa kinyume na matakwa ya kisheria.

Pamoja na mambo mengine, Butawantemi  alifafanua kuwa nyaraka hiyo ni mpya kwa kuwa haikuwepo katika orodha ya vielelezo vya upande wa utetezi vilivyotarajiwa kuwasilishwa mahakamani tangu mwanzo.

Pia alidai kuwa mahakamani haikuwa imeelekezwa vyema kuhusiana na upokewaji wake na kwamba shahidi hakuwa ameijengea msingi kwanza kabla ya kuomba ipokewe.

Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Msafiri alikataa Katiba hiyo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi za mawakili wa mlalamikaji.

Jaji Msafiri alisema ni takwa la sheria, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai (CPC) kuwa nyaraka inayokusudiwa kutolewa (kupokewa) mahakamani kama kielelezo sharti iwe imebainishwa kwanza katika nyaraka za kesi.

Jaji Msafiri alisema hatua hiyo haikuwa imefanyika katika kielelezo hicho na hivyo ilikuwa ni nyaraka mpya, hivyo haiwezi kupokewa na Mahakama katika hatua hiyo kwa kuwa ni nyaraka mpya.

Katika maelezo yake ya ushahidi wake wa maandishi na ufafanuzi alioutoa mahakani kwa mdomo pamoja na mambo mengine, Lawi  alidai kuwa ofisini kwake hakuna kumbukumbu zinazoonesha kuwepo kwa kikao kilichopendekeza Askofu Sepeku kupewa zawadi hizo.

Pia, alidai kuwa vikao vya mamlaka zinazodaiwa kupendekeza na kumpa Askofu Sepeku zawadi ya ardhi inayobishaniwa yaani Kamati ya Kudumu na Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, hazina mamlaka ya kugawa mali ya kanisa.

Badala yake alidai kuwa uamuzi kama huo unafanywa na kikao cha wadhamini huku akielezea hatua mbalimbali na kwamba hajawahi kuona kumbukumbu za kikao cha Wadhamini kilichopendekeza na kupitisha uamuzi wa kumpa zawadi hiyo Askofu Sepeku.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mashahidi wa upande wa mlalamikaji katika kesi hiyo, wakiwemo maaskofu, mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa hilo na Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo mstaafu, Dk Valentino Mokiwa walikiri kutambua uamuzi huo. 

Pamoja na kutambua, kuona na kushiriki vikao vilivyoridhia na kupitisha pendekezo hilo la kumpa zawadi Askofu Sepeku, walisema kuwa Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam ina mamlaka ya kufanya hivyo.

Maaskofu hao walifafanua kuwa sinodi ni mkutano mtakatifu wa juu unaowahusisha Askofu wa Dayosisi, mapadri na waumini kwa ajili ya kufanya uamuzi wa Kanisa na kwamba uamuzi wake haiwezi kupinga popote wala kutenguliwa na mtu yeyote.

Related Posts