Kilichojili kesi ya kanisa kumnyang’anya zawadi mtoto wa Askofu Sepeku

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, imepanga Julai 18, 2025 kuendelea na usikilizwa katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa na mtoto wa Askofu John Sepeku, Bernardo Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa kanisa hilo pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Bernado, ambaye ni mtoto wa marehemu John Sepeku, ambaye alikuwa askofu wa kwanza Kanisa hilo hapa nchini, alifungua kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Sepeku alipewa zawadi na kanisa hilo ambayo ni nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke  kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo, kama Askofu wa kwanza kanisa hilo.

Katika kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, Bernado ambaye kwa sasa ni msimamizi wa mirathi ya baba yao anapinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yao.

Anaiomba Mahakama iamuru alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.

Vilevile anaiomba alipwe Sh493.65 milioni kama fidia ya hasara ya mazao yaliyoharibiwa katika shamba hilo.

Kesi hiyo ilipangwa leo, Alhamisi, Juni 26, 2025 kwa ajili ya shahidi wa upande wa utetezi kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili wa mlalamikaji, kuhusiana na ushahidi aliyoutoa mahakamani hapo dhidi ya kesi hiyo.

Haya hivyo, kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Arafa Msafiri, imeshindwa kuendelea baada ya mawakili wa pande zote mbili yaani mawakili wa mdai na mdaiwa kukutana na kujadiliana na kisha kukubaliana kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea kesi hiyo.

Bila kuweka wazi sababu za kuomba kupangiwa tarehe nyingine na mahakama hivyo mawakili wa mlalamikaji katika kesi hiyo, Deogratius Butawantemi na Gwamaka Sekela na wakili Denis Malamba anamtetea mshtakiwa wa kwanza na wa pili, wamedai kuwa wamekubaliana kupangiwa tarehe nyingine ambayo mashahidi wa upande wa utetezi watafika mahakamani hapo kutoa ushahidi wao.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Sarah Buya, ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 18, 2025 itakapoendelea na kuelekeza mashahidi hao wafike mahakamani hapo tarehe hiyo.

Tayari mashahidi wawili wa upande wa utetezi wameshatoa ushahidi wao kuhusiana na kesi hiyo, baada ya upande wa mlalamikaji kufunga ushahidi wao.

Baadhi ya mashahidi wa upande wa utetezi waliotoa ushahidi wao mahakamani hapo ni Katibu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Mchungaji George Lawi.

Lawi ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wadhamini wa Kanisa hilo, alitakiwa leo kuhojiwa maswali ya Dodoso na mawakili wa Sepeku.

Katika utetezi wake aliyoutoa Juni 4, 2025, akiongozwa na wakili wake, Denis Malamba, shahidi huyo  aliomba Mahakama ipokee Katiba ya Kanisa hilo ya Mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, iwe sehemu ya ushahidi wake.

Katiba hiyo ilikusudiwa kuwa sehemu ya ushahidi wake katika kuunga mkono ushahidi wake wa maandishi aliokwisha uwasilisha mahakamani kwa maandishi pamoja na ufafanuzi alioutoa mahakamani kwa mdomo.

Hata hivyo, Katiba hiyo ilipingwa na mawakili wa madai katika kesi hiyo, kutokana na ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika uwasilishaji na upokewaji wa vielelezo mahakamani.

Katika maelezo yake ya ushahidi wake wa maandishi na ufafanuzi alioutoa mahakani kwa njia ya mdomo pamoja na mambo mengine, Katibu huyo wa kanisa hilo alidai kuwa ofisini kwake hakuna kumbukumbu zinazoonesha kuwepo kwa kikao kilichopendekeza Askofu Sepeku kupewa zawadi hizo.

Aliendelea kudai kuwa vikao vya mamlaka zinazodaiwa kupendekeza na kumpa Askofu Sepeku zawadi ya Ardhi inayobishaniwa yaani Kamati ya Kudumu na Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, hazina mamlaka ya kugawa mali ya Kanisa.

Badala yake alidai kuwa uamuzi kama huo unafanywa na kikao cha Wadhamini huku akielezea hatua mbalimbali na kwamba hajawahi kuona kumbukumbu za kikao cha Wadhamini kilichopendekeza na kupitisha uamuzi wa kumpa zawadi hiyo Askofu Sepeku.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mashahidi wa upande wa mlalamikaji katika kesi hiyo, wakiwemo maaskofu, mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa hilo na Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo mstaafu, Dk Valentino Mokiwa walikiri kutambua uamuzi huo.

Pamoja na kutambua, kuona na kushiriki vikao vilivyoridhia na kupitisha pendekezo hilo la kumpa zawadi Askofu Sepeku, walisema kuwa Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam ina mamlaka ya kufanya hivyo.

Maaskofu hao walifafanua kuwa Sinodi ni Mkutano Mtakatifu wa Juu unaowahusisha Askofu wa Dayosisi, mapadri na waumini kwa ajili ya kufanya uamuzi wa Kanisa na kwamba uamuzi wake haiwezi kupinga popote wala kutenguliwa na mtu yeyote.

Related Posts