Moshi. Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukimbizwa katika Mkoa wa Kilimanjaro kuanzia Juni 28 hadi Julai 4, 2025, ambapo utapitia miradi 52 ya maendeleo yenye thamani ya Sh84.9 bilioni.
Akizungumzia mbio hizo za Mwenge leo Alhamisi Juni 26, 2025, ofisini kwake mjini Moshi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Mwenge utapokewa katika Uwanja wa Ndege wa Moshi na kukimbizwa katika halmashauri zote saba za mkoa huo, kabla ya kukabidhiwa kwa Mkoa wa Arusha, Julai 5, 2025.
“Katika miradi hiyo, miradi 23 itazinduliwa, 20 itawekwa mawe ya msingi na tisa itatembelewa kwa ajili ya kukagua utekelezaji wake,” amesema Babu.
Ameeleza kuwa miradi hiyo imefadhiliwa na wadau mbalimbali wa maendeleo ambapo serikali kuu imetoa Sh23.2 bilioni, halmashauri na manispaa imetoa Sh2.3 bilioni, nguvu za wananchi Sh2.7 bilioni, huku wafadhili wakichangia Sh55.2 bilioni.
Babu amebainisha kuwa miradi hiyo imegusa sekta mbalimbali ambapo sekta ya afya kuna miradi minane, barabara na madaraja saba, sekta ya elimu miradi 11, sekta ya maji miradi saba, nishati salama miradi mitatu, vijana miradi saba na miradi tisa ya kijamii.
Aidha, amesema Mwenge wa Uhuru pia utatembelea na kuona jitihada mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa na vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia shughuli za uzalishaji mali.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amesema wilaya hiyo imejipanga kuhakikisha miradi inayopitiwa na Mwenge wa Uhuru inakamilika kwa ubora unaotakiwa ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
“Wilaya ya Rombo tutaupokea Mwenge wa Uhuru Julai 2, 2025, ambapo utatembelea miradi mbalimbali kwa ajili ya kuzinduliwa, kuwekwa mawe ya msingi na mingine kukaguliwa,” amesema Mwangwala.
Mwenge wa Uhuru umekuwa ukitumiwa katika kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji, uzalendo na mshikamano wa kitaifa, ambapo kila mwaka hukimbizwa nchi nzima kutembelea, kuzindua au kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya kijamii na kiuchumi.