Serikali yajitosa huduma za teksi mtandao

Dar es Salaam. Ni rasmi Serikali imejitosa kwenye huduma za teksi mtandao, hivi ndivyo inavyoweza kutafsiriwa kufuatia Shirika la Posta Tanzania kuingia mkataba na kampuni ya taksi mtandao kutoa huduma za usafirishaji wa abiria na vifurushi.

Katika kuongeza wigo wa huduma hizo ushirikiano huo utawezesha kusafirishwa pia kwa mizigo kutoka maeneo mbalimbali nchini na kutoa huduma za kuhama.

Hatua hiyo inalenga kuwasogezea wananchi huduma za usafirishaji inayoendana na maendeleo ya teknolojia huku suala la usalama kwa pande zote likipewa kipaumbele.

Akizungumza kwa niaba ya PostaMasta Mkuu, Meneja wa Posta Mkoa wa Dar es Salaam Ferdinand Kabyemela amesema hatua hiyo inalenga kutanua wigo wa huduma za usafirishaji ikiwa ni jukumu kuu la shirika hilo.

Amesema kwa kutambua kuwa sasa dunia inakwenda kidigitali wameamua kuingia ubia na kampuni ambayo itawezesha lengo hilo la kutoa huduma za usafirishaji kukamilika.

Kabyemela amesema kwa mtandao mpana wa shirika hilo ambalo lipo katika mikoa yote nchini huduma hizo zitatolewa.

“Kwa kuwa shirika letu ni la Serikali kuna namna tunaenda kujenga uaminifu kwa wananchi kuanzia huduma watakazopata hadi usalama wao na mali zao wanazokwenda kusafirisha.

“Kilichofanyika hapa wenzetu wa Swifpack wameleta teknolojia ambao ndiyo hiyo application inapakuliwa kwenye simu janja kumuwezesha mtu kuita aina yoyote ya usafiri kwa ajili yake au mizigo na ikafikishwa sehemu husika kwa usalama kabisa,”amesema.

Mkurugenzi wa Swifpack, Marco Mhagama amesema walitengeneza mfumo baada ya kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo na madereva na kwa kiasi kikubwa umezitatua.

Amesema tofauti na taksi mtandao nyingine hiyo itahusisha pia maguta, magari madogo na makubwa ya mizigo ambayo yatakuwa na uwezo wa kusafiri kutoka mkoa mmoja hadi mwingine.

“Hadi kufikia Juni 26 madereva wa pikipiki na magari madogo walijisajili na mfumo huo na wengine 2500 wenye magari ya kusafirisha mizigo, matarajio yetu kufikia mwisho wa mwaka huu tuwe tumesajili madereva wasiopungua 30,000,” amesema Mhagama.

Hatua hii ya shirika la posta kuingia kwenye huduma za taksi mtandao imekuja kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko dhidi ya kampuni zinazotoa huduma hizo.

Hali hiyo ilisababisha mara kadhaa kuwepo kwa vuta nikuvute baina ya pande hizo kama ilivyotokea Oktoba mwaka 2024 ambapo madereva hao walifanya mgomo wakitaka kupunguzwa kwa kamisheni inayotozwa.

Baadhi ya madereva waliozungumza na Mwananchi wameleeza kuwa makubaliano ambayo wameingia kati yao na shirika la posta na Swifpack yanaonekana kuleta ahueni kwao.

Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mtandaoni (UMM) Issa Swahibu amesema wameshirikishwa katika kila hatua kabla ya application hiyo kuanza kutoa huduma.

“Tulieleza changamoto zote ambazo tunakutana nazo ikiwemo kilio chetu cha kukatwa kamisheni kubwa, tuliyoyataka yote yamefanyiwa kazi ndiyo maana tunasema hii itakuwa mkombozi kwetu.

“Hizi application ambazo sisi tunaziita za kikoloni tunakatwa asilimia 25 kila safari, hili suala linatuumiza tumezungumza na hawa wa Posta kwa sababu wanataka kusiwe na maumivu pande zote tumekubaliana itakuwa asilimia 15 na hakuna mabadiliko yatakayofanyika bila kutushirikisha,” amesema Shwaibu.

Kwa upande wake Jeremia Lucas ambaye ni dereva bodaboda amepongeza hatua ya Serikali kuingia kwenye huduma hiyo ambayo kwa sasa imekuwa tegemezi.

“Hii huduma ya taksi mtandao inawezekana ikaonekana ni kitu kidogo lakini kuna vijana wengi wamejiajiri, sasa kama kutakuwepo na usimamizi mzuri kama walioahidi Shirika la Posta ni imani yangu hata hiki kilio cha ukosefu wa ajira kitapungua. Wengi tutakuwa tumejiajiri upande huu,” amesema Lucas.

Related Posts