Rukwa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limetoa onyo kali kwa mgombea yeyote atayechochea vurugu au kuwa na shamrashamra za matarumbeta, ngoma, wapambe na pikipiki katika kuchukua na kurudisha fomu za ubunge na udiwani kuanzia Jumamosi Juni 28, 2025.
Kauli hiyo ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa imetolewa ikiwa imebaki siku moja kuanza kwa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za ubunge na udiwani kwa makada waliotia nia ya kugombea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 26, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija amesema wananchi na wagombea wote wenye nia ya kuchukua fomu wanapaswa kuzingatia mwongozo na maelekezo kuhusu utaratibu wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wanachama.
Amesema lengo la zuio ni kutokana na umuhimu wa mchakato katika kuwaunganisha wanachama na wananchi ili kulinda misingi ya umoja, upendo, ushirikiano, mshikamano.
“Ili kusimamia misingi hiyo, inaelekezwa kwamba ni marufuku kwa mwanachama yeyote au mgombea kualika kundi la wapambe kumsindikiza kwenda kwenye ofisi ya a chama chochote kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea,” amesema Kamanda Masija.
Kamanda Masija amesisitiza kuwa vitendo hivyo vinaleta viashiria vya makundi na mpasuko ndani ya jamii, havipaswi kufanywa na mwanachama hata mwananchi yoyete.
“Wananchi wanapaswa kutumia haki yao ya msingi ya kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi zilizopo bila kushurutishwa na mtu yeyote na hatimae kuchagua na kuchaguliwa ifikapo mwezi oktoba mwaka huu,” amesema.
Kwa upande wake, aliyekuwa meya wa manispaa ya Sumbawanga, Justin Malisawa ameliambia Mwananchi kuwa ni muhimu kila mmoja akafuata maelekezo yanayotolewa na viongozi hasa kwa wale wenye lengo la kugombea nafasi za uongozi na kuacha chokochoko za kisiasa ambazo muda wake bado.
“Wananchi, wanachama na wagombea wenyewe wanapaswa kuwa watulivu wakachukue fomu kwa amani na kwa wale wanaoendelea na nafasi zao waendelee kulinda heshima yao kwani wananchi ndio wenye maamuzi ya kumchagua mtu anayewafaa,” amesisitiza.
Mwananchi limezungumza na Dawood Juma ambaye amesema atachukua fomu na kugombea tena nafasi ya udiwani katika kata ya Mazwi na kusema ni kweli kuwa wanahitaji ulinzi uimarishwe siku hiyo ili kuwahakikishia usalama wao katika zoezi hilo.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha amani na utulivu vinaimarishwa na wananchi wanashiriki uchaguzi katika hali ya amani na utulivu.