Straika JKT Tanzania kiroho safi

MSHAMBULIAJI wa JKT Tanzania, Edward Songo amesema msimu wa Ligi Kuu Bara uliomalizika jana Jumatano ulikuwa  mzuri kwao, lakini umewaachia somo la kujipanga ili ujao wa 2025/26 waweze kufanya makubwa zaidi.

Songo ambaye amemaliza msimu akiwa na mabao sita na asisti mbili, alisema kitendo cha timu hiyo kumaliza nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu kwao kimewapa nguvu ya kujipanga zaidi, ili kurejea na nguvu mpya ya ushindani.

“Jambo la msingi kwetu ni timu kusalia Ligi Kuu, kwani zipo zingine ambazo zimeshuka na zingine zinacheza mtoano, ndiyo maana nasema ulikuwa msimu mzuri kwa upande wetu,” alisema Songo na kuongeza.

“Japokuwa mafanikio yangu binafsi nilitamani kumaliza na mabao si chini ya 10, ila sijatimiza hilo badala yake nimefunga mabao sita na asisti mbili, najipanga kwa ajili ya msimu ujao, naamini nitafanya makubwa zaidi.”

Alisema kwa ujumla Ligi Kuu ilikuwa ngumu na ya ushindani kwa wachezaji wageni na wazawa, kitu ambacho kinaongeza thamani kwa wachezaji kunufaika na vipaji vyao.

“Mfano nafasi ya ushambuliaji kuna wazawa wana mabao mengi Clement Mzize, Fei Toto ndiye kinara wa asisti 13 na mabao manne, ni muendelezo wa kufanya vizuri kwake tangu msimu uliyopita,” alisema.

Related Posts