Leo nimemsikiliza Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akitoa hotuba ya kuaga Bunge la 12 na kuelezea mafanikio lukuki ikiwamo maswali zaidi ya 20,300 yakiulizwa na wabunge na kupatiwa majibu na Serikali.
Ni kweli ni mafanikio na linastahili pongezi, lakini Waswahili wanasema siku zote kizuri hakikosi kasoro, kwani pamoja na mazuri yote ya Bunge la 12, kuna mambo mawili ambayo mimi pengine na Watanzania tunaona hamkututendea haki.
Inawezekana Bunge la tisa lililokuwa chini ya Spika mwenye standard speed (kasi na viwango), Samwel Sitta (marehemu) na Bunge la 10 chini ya Spika Anne Makinda, yakawa na mazuri na upungufu wake, lakini leo nitazungumzia Bunge la 12.
Kwa nini, ni kwa sababu katika vigezo vya sita vinavyofanya habari iwe habari (newsworthy story) ni pamoja na “timeliness” ambayo inataka habari itolewe kwa wakati tukio linapotokea ili isije ikawa ngera (kiporo) tena kiporo kilichochacha.
Sasa leo Juni 26, 2025 nimemsikiliza Spika wetu wa Bunge la 12, Dk Ackson, linahitimiswa kesho na Rais Samia Suluhu Hassan, akisema katika uhai wa bunge hili, maswali ya msingi 5,057 na ya nyongeza 15,000 yaliulizwa na wabunge wetu.
Mbali na maswali hayo, lakini maswali ya papo hapo kwa waziri mkuu, Kassim Majaliwa ambayo huulizwa kila siku ya Alhamisi yalikuwa 260 hivyo ukijumlisha maswali yale ya msingi, ya nyongeza na ya waziri mkuu unapata maswali 20,317.
Lakini kwa mujibu wa Dk Tulia, miswada 60 ilijadiliwa na kupitishwa kuwa sheria na kwamba mikataba, maazimio na itifaki 16 za kimataifa ziliridhiwa na Bunge hili lakini kubwa zaidi lilijadili na kupitisha bajeti za Serikali katika kipindi hicho.
Ninachoweza kusema, kati ya asilimia 100, kwa tathmini yangu ninaweza kulipa Bunge hili asilimia 99 kuwa limetekeleza majukumu yake vizuri kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Ukiisoma ibara ndogo ya (2) inasema Bunge litakuwa ndicho chombo kikuu ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake ya Kikatiba.
Sasa hayo yote aliyoyasema Spika ni majukumu ambayo yanatajwa na Ibara hiyo ambayo sisi kama wananchi tuliitegemea, kuona Bunge hili licha ya kuwa na sura ya chama kimoja kwa wingi wao, lakini lingesimama upande wa wananchi.
Pamoja na mafanikio hayo, mie nimeondoa ile asilimia moja kutokana na namna bunge halikutimiza wajibu wake wa kikatiba vizuri katika kuisimamia serikali katika suala la watu wasio na hatia kutekwa, kupotezwa na hata wengine kuuawa.
Nawapongeza wabunge wale wachache waliojaribu bila mafanikio kutaka hoja hii ijadiliwe kwa dharura bila mafanikio, na nasema wazi kabisa sababu zilizokuwa zikizuia mijadala hii zilizokuwa zinatolewa na Dk Ackson hazikunishawishi.
Bunge letu halikuonyesha makali yake katika suala hili katika kuisimamia na kuishauri Serikali hasa tukitambua kuwa uhai huwa haununuliwi dukani, hivyo hadi uhai wa bunge la 12 unamalizika bila kujadili suala hili hii ni dosari kubwa.
Pengine lingejadili suala hili au hata kuunda Kamati Teule kuchunguza matukio haya yaliyoanza na mwaka 2016, pengine leo tungekuwa na akina Deusdedith Soka na wenzake na tungeepusha mauaji ya mzee wetu Ally Mohamed Kibao.
Tungeyajadili haya, pengine leo tusingehoji kutekwa na kupotezwa kwa mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na pengine tungezuia kutekwa na kuteswa kwa kada wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo na wegine wengi tu.
Kama Bunge hili lingetimiza vyema wajibu wake katika eneo hili la asilimia moja niliyoiondoa, wangeisimamia na kuishauri Serikali itekeleze mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 31, 2023.
Tume hii ilisema uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka ya kukamata imekuwa ni changamoto na inawawia vigumu wananchi kutambua taasisi iliyomkamata ndugu yao na mahali alipohifadhiwa, na kama ametekwa na genge la wahalifu au la.
Kulingana na Tume, uwepo wa vyombo vingi vya ukamataji na vyenye mahabusu hapa Tanzania umetafsiriwa na jamii kuwa ni sababu mojawapo ya watu waliokamatwa kupotea wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Tume ilipendekeza mamlaka ya kukamata waliyonayo mamlaka za usimamizi (regulatory bodies) yatekelezwe kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na taasisi nyingine zenye mamlaka ya kukamata, zikamate kwa kushirikiana na Polisi.
Lakini kubwa zaidi, Tume ilipendekeza mahabusu za Jeshi la Polisi ndizo pekee zitumike kuhifadhi watuhumiwa wa makosa ya jinai na ikaenda mbali na kupendekeza kuundwa kwa Taasisi ya Upelelezi inayojitegemea.
Haya yote kama Bunge letu lingeibana Serikali na yakatekelezwa kikamilifu pengine leo tusingekuwa tunazungumzia wimbi la utekaji kwa sababu wananchi tungejua yeyote anayemkamata ndugu yetu bila kuwa na polisi ni mtekaji.
Mpaka ninapoandika makala haya, ninajiuliza sana, kigugumizi cha bunge katika kuisimamia na kuishauri Serikali katika hili kilisababishwa na nini?
Ukiacha matukio hayo, lakini kumekuwa na kilio kikubwa cha wananchi juu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na baadhi ya askari wetu wa Jeshi la Polisi yakiwamo mateso, vipigo na hata kusababisha vifo.
Mimi binafsi nilitarajia wabunge wetu ambao ndio wawakilishi wetu, wangekomaa na Serikali na kuhakikisha inaleta muswada wa sheria bungeni wa kuanzisha chombo huru cha kuchunguza ukiukwaji wa maadili ya kazi unaofanywa na polisi.
Kulipotokea mauaji ya mfanyabiashara wa madini kule Mtwara ambayo yalifanywa na baadhi ya Polisi, tulimsikia Rais Samia akisema Polisi hawawezi kufanya unyama wao halafu wakajichunguza wenyewe hivyo akasema uchunguzi uwe huru.
Nilitarajia wabunge wetu wangeshikilia hapo hapo kwanza tuanze chombo kama IPOA (Independent Policing Oversight Authority) cha Kenya ambacho ndicho huchunguza matukio ya ukiukwaji wa sheria yanayofanywa na vyombo vya Dola.
Jambo lingine lililonifanya niondoe ile asilimia moja ni kutoona ukali wa Bunge wakati Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinapowasilishwa, kulinganisha na ukali tuliouona bunge la tisa na lile la 10.
Mabunge hayo ninayoyazungumzia ndio ambayo tulishuhudia ripoti za CAG zilizojaa madudu kama hizi hizi zilizowasilishwa Bunge la 12 zilivyowang’oa baadhi ya mawaziri na hata watendaji wengine ambao ni wateule wa Rais kuwajibishwa.
Ni kutokana na Bunge la 12 kutoonyesha makali yake, ndio maana kulikuwa na kumeendelea kuwa na hisia kutoka kwa wananchi kuwa pengine hii imechangiwa na kukosekana kwa kambi rasmi ya upinzani bungeni na wabunge machachari.
Nasema hivyo kwa sababu, mathalan kati ya 2005 hadi 2015, miongoni mwa wabunge waliokuwa mwiba bungeni walikuwa ni kutoka CCM. Hawa ni kama Aloyce Kimaro, James Lembeli, Beatrice Shelukindo (marehemu) na Lucas Selelii.
Ndio maana nimetangulia kusema ‘hongera Bunge la 12 kwa maswali 20,300 ila deni hili mmetuacha nalo kwa sababu ya mambo hayo na mengine ambayo kiukweli hamkututendea haki sisi kama wananchi tunaoumizwa na mambo hayo.
Kwa hiyo tunapokwenda kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 2025, tunatarajia kupata wabunge ambao wataguswa kweli kweli na shida za wapiga kura wao na kuibana Serikali kweli kweli kama ilivyokuwa katika mabunge ya tisa na 10.
Haiwezekani katika uhai wa Bunge la 12 tumeshindwa hata kuunda kamati teule kuchunguza wimbi hili la utekaji ambao limefanya wananchi walio wengi sasa wanaishi kwa hofu bila kujua kesho yao itakuwaje. Bunge hamkututendea haki.