Sasa dunia imeanza sura mpya kabisa katika uhusiano kati ya Marekani na Iran uhusiano ambao unaweza kuwa bora zaidi au mbaya zaidi kabisa.
Kwa karibu miaka hamsini iliyopita, dunia imekuwa mashuhuda wa uhasama sugu vitisho, njama na maneno yenye sumu kati ya Marekani na Iran.
Marekani imekuwa ikiitaja Iran kama ‘Shetani Mkuu’ au ‘Kitovu cha Uovu’ kuhusu matatizo ya Mashariki ya Kati.
Sasa tuna Rais wa Marekani anayesema, ‘Mungu ibariki Iran’.
Mabadiliko haya ya kauli, hata kama yatadumu kwa kipindi kifupi, yalijitokeza baada ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran wiki hii, na mashambulizi ya Iran ya kulipiza kisasi lakini kwa kiasi dhidi ya kambi ya jeshi la Marekani Qatar, pamoja na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kwa juhudi za Rais Donald Trump katika mzozo kati ya Israel na Iran.
Ripoti ya ujasusi ya Marekani ilibaini kuwa mashambulizi yalilenga maeneo matatu na kusababisha uharibifu mkubwa lakini hayakuruhusu maeneo hayo kuharibiwa kabisa, ikipinga madai ya Trump kwamba yale mashambulizi ‘yameharibu kabisa’ programu ya nyuklia ya Iran.
Hata hivyo, kuna maswali na majibu kuhusu historia ndefu ya uhasama mkali kati ya mataifa haya mawili Marekani na Iran
Kwa nini Trump alitamka baraka kwa kila upande?
Katika hatua za awali za makubaliano ya kusitisha mapigano, hata kabla ya Israel na Iran kuonyesha kuwa wako tayari kikamilifu, Trump alijivunia mafanikio hayo.
“Mungu ibariki Israel,” aliandika kwenye mitandao ya kijamii. “Mungu ibariki Iran.” Pia alitamka baraka kwa Mashariki ya Kati, Marekani na dunia kwa ujumla.
Hata hivyo, ilipobainika kuwa mapigano hayakuwa yamekoma kabisa kama ilivyodhaniwa, akaanza kutumia lugha kali.
“Kimsingi tunazo nchi mbili ambazo zimekuwa zikigombana kwa muda mrefu na kwa nguvu kiasi kwamba hazijui tena kinachoendelea,” alisema kwa ukali mbele ya kamera za waandishi wa habari.
Wakati huo, Trump aliilaumu Israel ambayo ni mshirika wa karibu wa Marekanikwa kuonekana kutokuwa tayari kushikilia usitishaji mapigano kama Iran, taifa ambalo limekuwa likipiga kelele za Marekani Ife kwa miaka mingi na linalotuhumiwa kupanga njama za kumuua yeye.
Ni lini uhusiano wa Marekani–Iran ulianza kuharibika?
Jibu la swali hili liko kwenye maneno mawili: Operesheni Ajax.
Hayo yalikuwa ni mapinduzi ya mwaka 1953 yaliyopangwa na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) kwa msaada wa Uingereza, yaliyoiangusha serikali ya kidemokrasia ya Iran na kumuweka madarakani shah, Mohammad Reza Pahlavi.
Mataifa ya Magharibi yalihofia kuongezeka kwa ushawishi wa Umoja wa Kisovieti na hatua ya Iran ya kutaka kitaifisha sekta yake ya mafuta.
Shah alikuwa mshirika wa kimkakati wa Marekani ambaye alirejesha uhusiano rasmi na Washington.
Hata hivyo, chuki zilikuwa zikichemka miongoni mwa Wairani kutokana na utawala wake wa kiimla na kujipendekeza kwake kwa masilahi ya Marekani.
Yote hayo yalilipuka mwaka 1979, shah alipokimbia nchi na mapinduzi ya kidini yakatwaa madaraka, yakaanzisha utawala wao wenye misimamo mikali.
Mapinduzi ya Iran yaliendeleza vipi mvutano?
Jibu ni ndiyo. Jumapili ya Novemba 4, 1979, wakati chuki ya Iran dhidi ya Marekani ikiwa imefika kwenye kilele chake, wanafunzi raia wa Iran waliwachukua mateka wanadiplomasia na raia 66 wa Marekani, na zaidi ya 50 kati yao walishikiliwa kwa siku 444.
Tukio hilo lilikuwa fedheha kubwa kwa Marekani na Rais Jimmy Carter, ambaye aliagiza operesheni ya siri ya kuwaokoa mateka hao miezi kadhaa baada ya mzozo huo kuanza.
Katika Operesheni Eagle Claw, helikopta nane za Jeshi la Majini na ndege sita za usafirishaji za Jeshi la Anga za Marekani zilipelekwa kukutana katika jangwa la Iran.
Dhoruba ya mchanga ililazimisha operesheni hiyo kusitishwa ghafla, na wanajeshi wanane walifariki dunia baada ya helikopta kugongana na ndege ya kujaza mafuta ya C-120.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili yalivunjika mwaka 1980 na hadi leo hayajarejeshwa.
Iran iliwaachia mateka dakika chache tu baada ya Ronald Reagan kuapishwa kuwa rais Januari 20, 1981.
Hii ilikuwa muda wa kutosha kuhakikisha kuwa Carter, aliyekuwa amezama katika mzozo huo kwa zaidi ya mwaka mmoja, hatawaona mateka hao wakiachiliwa wakati wa utawala wake.
Je, shambulio la Marekani wiki hii lilikuwa la kwanza dhidi ya Iran?
La hasha. Shambulio kubwa la mwisho lilitokea baharini.
Jumatatu ya Aprili 18, 1988, Jeshi la Wanamaji la Marekani lilizamisha meli mbili za Iran, likaharibu nyingine moja na kuharibu majukwaa mawili ya upelelezi katika mapambano yake makubwa zaidi baharini tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia kumalizika mwaka 1945.
Operesheni hiyo, iliyojulikana kama ‘Praying Mantis’, ilikuwa ni hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya uharibifu uliofanywa na Iran dhidi ya meli ya ‘USS Samuel B. Roberts’ katika Ghuba ya Uajemi siku nne kabla. Mabaharia kumi walijeruhiwa, na mlipuko uliacha ufa mkubwa kwenye ganda la meli hiyo.
Je, Marekani ilikuwa na upande katika vita vya Iran na Iraq?
Ingawa hakuna jibu la moja kwa moja, lakini kimsingi jawabu ni ndiyo.
Marekani iliisaidia Iraq kiuchumi, ikashirikiana nayo taarifa za kijasusi na kuipa teknolojia ya kijeshi, ikiwa na wasiwasi kwamba ushindi wa Iran ungesababisha machafuko zaidi katika eneo hilo na kuhatarisha upatikanaji wa mafuta.
Vita hiyo ya Iran na Iraq ilidumu kuanzia mwaka 1980 hadi 1988 bila mshindi wa wazi, huku mamia ya maelfu wakipoteza maisha, na uhusiano kati ya Marekani na Iraq ukivurugika vibaya miaka ya baadaye.
Kashfa ya Iran-Contra ilikuwa nini?
Ni mfano wa aina fulani ya ushirikiano kati ya Marekani na Iran uliokuwa haramu na wa siri hadi ulipofichuliwa.
Mwaka 1984, muda mfupi baada ya Marekani kuiorodhesha Iran kama mfadhili wa ugaidi wa kimataifa hadhi ambayo bado haijabadilika ilibainika kuwa Marekani ilikuwa ikiuzia Iran silaha kwa njia zisizo halali.
Lengo moja lilikuwa kuokoa mateka waliokuwa wakishikiliwa nchini Lebanon na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
Lengo jingine lilikuwa kukusanya fedha za siri kwa ajili ya waasi wa Contra nchini Nicaragua, kinyume cha marufuku ya Marekani ya kuwasadia.
Rais Ronald Reagan alijikokota kupitia kashfa hiyo, lakini hakushtakiwa angalau kisheria, japo jina lake lilitiwa doa.
Ni mataifa mangapi ambayo Marekani inayatambua kama wafadhili wa ugaidi?
Ni manne tu: Iran, Korea Kaskazini, Cuba na Syria.
Hali hiyo huyaweka mataifa hayo kuwa shabaha ya vikwazo vikubwa vya kiuchumi na kidiplomasia. Hadhi ya Syria kwa sasa inapitiwa upya kufuatia kuanguka kwa serikali ya Bashar al-Assad.
Neno ‘Mhimi wa Uovu’ (Axis of Evil) lilitoka wapi?
Lilitamkwa na Rais George W. Bush katika hotuba yake ya ‘State of the Union’ mwaka 2002.
Alitoa hotuba hiyo miezi mitano baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001, na mwaka mmoja kabla hajaanzisha uvamizi nchini Iraq kwa msingi usio sahihi kwamba Saddam Hussein alikuwa na silaha za maangamizi ya halaiki.
Aliitaja Iran, Korea Kaskazini na Iraq ya Saddam, na kusema: “Mataifa kama haya, pamoja na washirika wao wa kigaidi, yanaunda mhimili wa uovu, yakiwa yamejihami kutishia amani ya dunia.”
Katika kujibu hilo, Iran na baadhi ya washirika wake wa kupinga Marekani kwa kuwataja kuwa “Mhimili wa Uovu”.
Vipi kuhusu ‘vibaraka’ na washirika hao?
Baadhi yao, kama vile Hezbollah na Hamas, wamepoteza nguvu kutokana na mashambulizi makali na ya muda mrefu yaliyofanywa Israel.
Nchini Syria, Assad alikimbilia Moscow kwa usalama wake baada ya kupokonywa madaraka na waasi waliowahi kuhusishwa na kundi la kigaidi la al-Qaida, lakini sasa wanapokwewa kwa tahadhari na Trump.
Nchini Yemen, waasi wa Houthi waliovamia meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu na kuonyesha mshikamano na Wapalestina wamekuwa wakishambuliwa na Marekani na Uingereza.
Nchini Iraq, makundi ya Waislamu wa Kishia waliobeba silaha, yanayodhibitiwa au kuungwa mkono na Iran, bado yanafanya kazi na mara kwa mara huandamwa na mashambulizi kutoka Marekani.
Vipi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran?
Mwaka 2015, Rais Barack Obama pamoja na mataifa mengine yenye nguvu walifikia makubaliano na Iran ya kuzuia maendeleo ya mpango wake wa nyuklia kwa masharti ya kulegezwa kwa vikwazo.
Iran ilikubali kuondoa hifadhi ya urani iliyotajirishwa, kuvunja mitambo mingi ya kuchakata urani (centrifuges), na kutoa fursa zaidi kwa wakaguzi wa kimataifa kufuatilia shughuli zake.
Trump alikosoa makubaliano hayo wakati wa kampeni yake ya mwaka 2016, na alipokuwa rais, aliyatupilia mbali mwaka 2018, kisha akaanzisha kampeni ya vikwazo vya “shinikizo la juu kabisa.”
Alidai kuwa makubaliano hayo yalichelewesha tu utengenezaji wa silaha za nyuklia, na hayakuzuia tabia ya uchokozi ya Iran katika eneo hilo.
Mpango wa nyuklia wa Iran ulianza tena taratibu, na kwa mujibu wa wakaguzi, umeharakishwa katika miezi ya hivi karibuni.
Kujiondoa kwa Trump katika makubaliano hayo kulisababisha onyo kutoka kwa Hassan Rouhani, aliyekuwa Rais wa Iran wakati huo, mwaka 2018: “Amerika inapaswa kuelewa vyema kuwa amani na Iran ni mama wa amani zote. Na vita na Iran ni mama wa vita vyote.”
Trump alijibu vipi uchokozi wa Iran?
Januari 2020, Trump aliamuru shambulio la ndege isiyo na rubani lililomuua Qassem Soleimani, kamanda mkuu wa majeshi ya Iran, alipokuwa nchini Iraq.
Baadaye, Iran ilielekeza hasira zake kwake, kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Rais Joe Biden, Merrick Garland.
Siku chache baada ya Trump kushinda uchaguzi wa mwaka jana, Idara ya Haki ya Marekani iliwasilisha mashtaka dhidi ya raia mmoja wa Iran anayeaminika kuwa bado yuko nchini humo, pamoja na washirika wake wawili waliodaiwa kuwapo New York.
“Idara ya Haki imemshtaki mtu anayetajwa kuwa wakala wa serikali ya Iran, ambaye alipewa jukumu na utawala huo kuongoza mtandao wa washirika wa kihalifu ili kutekeleza njama za mauaji dhidi ya walengwa wa Iran, akiwemo Rais mteule Donald Trump,” alisema Garland.
Sasa, Trump anatafuta amani mezani baada ya kuagiza mabomu yarushwe dhidi ya Iran, huku pia akitoa baraka.
Hii huenda ikawa ni mabadiliko makubwa kabisa ya msimamo.