Katika historia ya Afrika, vifo vya viongozi wakuu vinavyotokea wakiwa nje za nchi zao vimekuwa chanzo cha mzozo wa kisiasa, mashauri ya kisheria na mijadala mikubwa ya kitaifa.
Mfano wa karibuni zaidi ni wa aliyekuwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu, ambaye habari za kifo na mazishi yake zimetamba sana katika vyombo mbalimbali vya habari duniani.
Lungu, aliyekuwa Rais wa Zambia kuanzia mwaka 2015 hadi 2021, alifariki dunia Juni 5 mwaka huu katika Hospitali ya Mediclinic Medforum, iliyoko Pretoria, Afrika Kusini kutokana na matatizo ya moyo.
Muda mfupi baadaye baada ya kifo chake uliibuka mgogoro kuhusu ni wapi na kwa jinsi mazishi yake yangefanyika.
Ingawa mazishi ya kitaifa yangekuwa heshima kwa urithi Lungu, Serikali ya Afrika Kusini imethibitisha wajibu wake wa kisheria wa kuheshimu uamuzi wa familia ya marehemu kuhusu kuzikwa kwake nchini Afrika Kusini.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini, ilielezwa kuwa Serikali ya Afrika Kusini ilisema:
“Katika kusisitiza msimamo wa Serikali ya Afrika Kusini, Waziri Ronald Lamola alieleza kuwa maziko ya kitaifa nchini Zambia yangekuwa njia bora na ya heshima zaidi ya kumuenzi Rais wa zamani Lungu kwa mchango wake mkubwa kwa taifa la Zambia.”
Hata hivyo, waziri huyo alikiri kuwa, kwa mujibu wa sheria, Serikali ya Afrika Kusini ina wajibu wa kuheshimu matakwa yaliyowasilishwa na familia ya karibu ya marehemu Rais wa zamani, ya kutaka azikwe nchini humo.
Wiki iliyopita, familia ya marehemu Rais huyo ilitangaza kuwa angezikwa kwa ibada ya faragha nchini Afrika Kusini, kutokana na mvutano uliotokea kati yao na Serikali ya Zambia kuhusu maandalizi ya mazishi ya kitaifa.
Pamoja na makubaliano ya awali kuwa mazishi ya taifa yangefanyika katika eneo la Embassy Park Lusaka, familia yake ilisema kuwa katika maziko hayo asihudhurie Rais wa sasa, Hakainde Hichilema.
Hata hivyo, kwa maelezo ya hivi karibuni, familia imeamua mwili wake uzikwe Afrika Kusini, kwa maombi yao binafsi, licha ya Serikali kujaribu kulazimisha mazishi nchini Zambia.
Suala hili limegeuka na kuacha kuwa mgogoro wa kisiasa badala yake likageuka kuwa uamuzi binafsi uliochochewa na maazimio ya kifamilia na sasa liko mahakamani. Hata hivyo, huyu si kiongozi wa kwanza wa nchi za Afrika kukutwa katika hali hiyo.
Jose Eduardo dos Santos—Angola
Jose Eduardo dos Santos alifariki Julai 8, 2022 katika Kituo cha Tiba cha Teknon kilichopo Barcelona nchini Hispania, akiwa na umri wa miaka 79 baada ya kuiongoza Angola kwa miaka 38. Aliaga dunia baada ya kulazwa hospitalini kufuatia mshtuko wa moyo.
Kifo chake kilizua sintofahamu na mvutano mkubwa ndani ya familia, Serikali ya Angola, na vyombo vya sheria vya Hispania.
Mara baada ya kifo chake, taarifa zilienea kwamba binti yake, Tchizé dos Santos, aliwasilisha malalamiko kwa mamlaka za Hispania, akieleza mashaka kuwa huenda kulikuwapo na vitendo vya hujuma au uzembe uliosababisha kifo cha baba yake.
Kutokana na dai hilo, mahakama jijini Barcelona iliamuru kusitishwa kwa mipango yote ya kuutoa mwili wa marehemu kwa familia kwa ajili ya mazishi, ikisisitiza kuwa uchunguzi wa kina unapaswa kufanyika kwanza ili kubaini ukweli wa madai hayo ya uwezekano wa ushirikishwaji wa watu wengine katika kifo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa zilizosasishwa baadaye, baada ya uchunguzi wa kitabibu na wa kisheria kukamilika, mahakama ya Hispania iliruhusu mwili wa Santos kwenda kuzikwa Angola baada ya kuthibitisha kwamba alifariki dunia kwa sababu za kawaida.
Mvutano huu ulichochea mgawanyiko ndani ya familia ya marehemu, ambapo baadhi ya wanafamilia walisisitiza kuwa wangependa azikwe kwa utulivu na kwa heshima zote nchini Hispania, ambako aliishi baada ya kutoka madarakani mwaka 2017.
Wengine walipendelea mwili wake urejeshwe Angola kwa ajili ya mazishi ya kitaifa. Serikali ya Angola, kwa upande wake, ilisisitiza kuwa kama rais wa zamani na kiongozi wa kihistoria, mwili wake unapaswa kuzikwa nyumbani ili wananchi wapewe fursa ya kumuaga kwa heshima za taifa.
Hatimaye mwili wake ulisafirishwa Agosti 21, 2022 na kuzikwa rasmi Agosti 28 katika Makaburi ya Agostinho Neto.
Ahmadou Ahidjo—Cameroon
Ahmadou Ahidjo alikuwa Rais wa kwanza wa Cameroon tangu mwaka 1960 hadi 1982 alipoondolewa madarakani na kukimbilia Senegal.
Kifo chake kilifuatia miaka mingi ya kuishi uhamishoni baada ya kuondoka madarakani, hali iliyochochewa na mvutano wa kisiasa kati yake na mrithi wake, Rais Paul Biya.
Ahidjo alizikwa katika makaburi ya jiji la Dakar. Lakini katika hatua ya kipekee ya kihistoria, Desemba 1991, Bunge la Cameroon lilipitisha sheria rasmi ya kumrejeshea heshima, likimtakasa kwa makosa ambayo hapo awali yalikuwa yamemlazimu kuishi uhamishoni.
Oktoba 30, 2007, Rais Biya alizungumza kuwa abaki ya mwili wake ni suala la kifamilia, na hivyo hakutaka kuingilia bila makubaliano ya moja kwa moja na familia ya marehemu.
Kauli hiyo ilionekana kama njia ya kuepuka mvutano wa kisiasa uliohusiana na historia ya uongozi wao wawili.
Juni 2009, makubaliano rasmi yalifikiwa kati ya Serikali na familia ya Ahidjo kuhusu kurejesha mwili wake nchini Cameroon na ilitarajiwa kuwa mabaki yake yangeletwa nyumbani mwaka 2010 kwa maziko ya heshima.
Lakini hadi kufikia mwaka 2021, mwili wa Ahmadou Ahidjo uliendelea kubaki Dakar, Senegal, ambapo alizikwa kando ya mke wake, Germaine Ahidjo, aliyefariki dunia Aprili wa mwaka huo.
Mobutu Sese Seko—Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Zaire)
Mobutu Sese Seko aliongoza Zaire kuanzia mwaka 1965 hadi 1997. Akiwa uhamishoni Morocco alifariki Rabat Septemba 7, 1997. Bunge la DRC mwaka 2007 lilipendekeza mazishi yake kufanyika Katonga River, lakini bado mwili wake uko Rabat, Morocco.
Mutesa II wa Buganda—Uganda
Mutesa II wa Buganda wa Uganda aligeuzwa mpinzani wa kisiasa na kupinduliwa mwaka 1966. Alifariki dunia jijini London Novemba 21, 1969. Mazishi yake yaliandikwa huko London, kisha, baada ya mazungumzo ya kisiasa, mwili wake ulirejeshwa Uganda mwaka 1971 na kuzikwa Kasubi Tombs.
Mfalme Mwambutsa IV—Burundi
Mfalme Mwambutsa IV ni mhamiaji aliyefariki dunia nchini Switzerland mwaka 1977. Mwili wake ulirejeshwa Burundi mwaka 2012 baada ya mzozo wa kisheria, lakini hivi karibuni mwaka 2016 ulirudishwa Switzerland tena kulingana na uamuzi wa mahakama na kuzikwa huko.
Zine el Abidine Ben Ali—Tunisia
Zine el Abidine Ben Ali aaada ya kuondolewa madarakani nchini Tunisia mwaka 2011, alikimbilia uhamishoni Saudi Arabia ambako aliaga dunia Septemba 19, 2019. Mazishi yake yalifanyika kwa siri, huku Serikali ya Tunisia ikijadili kurejesha mwili wake nyumbani. Alizikwa kwenye makaburi ya Medina, Saudi Arabia.
Robert Mugabe alifariki dunia Septemba 6, 2019, katika Hospitali ya Gleneagles nchini Singapore, Septemba 11, mwili wake ulisafirishwa kupelekwa Harare kwa maziko.
Serikali ilipinga maombi ya familia mwili wa Mugabe kuzikwa Kutama. Mahakama iliamua kuwa angezikwa Heroes’ Acre. Mwishowe, Septemba 28, 2019, alizikwa Kutama, karibu na kaburi la mama yake.
Thomas Sankara—Burkina Faso
Thomas Sankara alifariki dunia Oktoba 15, 1987 kwa kupigwa risasi na watu wake wakiongozwa na rafiki yake, Blaise Compaore.
Mwili wake ulizikwa kwa kificho katika kaburi la pamoja eneo la Dagnoen. Juhudi za familia za kuupata mwili hazikufanikiwa.
Hata hivyo, baada ya mapinduzi ya 2014, mwaka 2015 mwili wake ulifukuliwa. Hatimaye mabaki ya mwili huo, pamoja na ya wenzake wawili waliouawa pamoja naye, yakazikwa Februari 23, 2023.
Alifariki dunia Aprili 27, 1972 huko Bucharest, Romania. Mwili wake ulisafirishwa hadi Conakry, Guinea, ambako alikuwa akiishi uhamishoni. Baadaye, kufuatia majadiliano kati ya Baraza la Ukombozi wa Taifa la Ghana na Rais wa Guinea, Sekou Toure, Julai 7 mwili wa Nkrumah nchini Ghana kwa maziko.
Rais Idi Amin wa Uganda ambaye alijaribu kuikalia kwa mabavu Mkoa wa Kagera mwaka 1978, aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Julius Nyerere, aliamuru Jeshi la Tanzania (JWTZ) kuivamia Uganda.
JWTZ walifanikiwa kuuteka mji wa Kampala mwaka 1979 na kumuondoa Amin madarakani. Amin alikimbilia uhamishoni, kwanza Libya, kisha Iraq, na hatimaye Saudi Arabia ambako aliishi hadi alipofariki dunia mwaka 2003 na kuzikwa katika Makaburi ya Ruwais mjini Jeddah.