Waeleza namna mbinu za kukabiliana na tembo vilivyowasaidia

Singida. Wananchi waishio maeneo yenye changamoto ya wanyama wakali wamesimulia namna wanavyokabiliana na wanyama hao ikiwemo Tembo kupitia mafunzo waliyoyapata.

Mafunzo hayo yaliyotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia utekelezaji wa mradi wa kupambana na Wanyama Wakali na Waharibifu (IWT) unaotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika ikolojia ya Ruaha-Rungwa.

Mradi huo unaofanyika katika Wilaya ya Manyoni kwenye Kijiji cha Mikwese na Halmashauri ya mji wa Itigi katika vijiji vya Sanjaranda na Doroto mkoani Singida.

Mkazi wa Kijiji cha Mkwese, Julius Chitute ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na UNDP kwa kuwapatia mafunzo, mbinu na mbegu ambazo kwa kiasi kikubwa kwa pamoja vimesaidia kupunguza changamoto ya tembo.

Amekitaja kilimo cha mazao mbadala ambayo hayapendwi na tembo hususani vitunguu, vimesaidia siyo tu kama nyenzo ya kuzuia tembo kushambulia mazao lakini pia imeongeza kipato na kupunguza umasikini.

“Kwa kuwa mkulima ana uhakika wa kulima na kuvuna sambamba na upatikanaji wa soko la uhakika tofauti na mazao mengine ambayo hushambuliwa na tembo kama chakula,” amesema.

Akielezea faida iliyopatikana baada ya kupewa mizinga ya kufugia nyuki kama nyenzo ya kuzuia tembo kuvamia mashamba na kuharibu mazao, Zainabu Saidi amesema mbali na mizinga hiyo kusaidia kuzuia tembo pia imekuwa na manufaa baada ya kuunda kikundi cha ufugaji nyuki na kusaidia kuongeza kipato hususani kwa akina mama kwa kufanya biashara ya uuzaji wa asali na mazao yake. 

Sada Ramadhani ambaye ni mfugaji wa nyuki katika Kijiji cha Sanyaranda kwa upande wake amesema mbinu walizofundishwa kwa ajili ya kufukuza tembo wasiharibu mazao yao mbali na kufanya kazi kwa ufanisi.

“Pia, zimesaidia kujiongezea kipato na kuiomba Serikali kutenga mapori na misitu maalumu ambayo haitakuwa na muingiliano wa shughuli nyingine za kibinadamu ikiwemo ufugaji na kilimo ili kupata asali bora itakayokidhi vigezo vya kimataifa jambo ambalo litawaongezea kipato maradufu,” amesema.

Mtaalamu wa Programu kutoka UNDP, Getrude Lyatuu amesema wameridhishwa na maendeleo yaliyopatikana na kazi zilizofanyika licha ya uwepo wa maeneo ya maboresho, ambapo mbinu na vifaa vilivyotolewa kwa wananchi kwa kiasi kikubwa vimesaidia kupunguza tatizo.

Amesema amefurahishwa na shuhuda za wananchi kuhusu ukubwa wa tatizo kabla na baada ya kupata mafunzo na mbinu.

Pia, vifaa vya kukabiliana na tembo na kupongeza jitihada za wananchi za kutafuta mbinu mbadala za kuendelea kukabiliana na changamoto ya Wanyama wakali na waharibifu hususani Tembo kwa kuwa mnyama huyo hubadili tabia kadri anavyoizoea mbinu ya awali.

“Tunachosisitiza kwa wananchi kile kidogo ambacho mradi umeonesha, na wakaona kuna manufaa, kiboreshwe zaidi kwa nguvu za wananchi kwa kipato wanachopata kutokana na miradi hiyo ili kuwezesha kuleta majibu chanya kwa ukubwa na ubira zaidi” amesema Lyatuu.

Related Posts