Wajumbe CCM wageuka lulu majimboni

Dar es Salaam. Kama ambavyo ungetamani shuka nyakati za baridi na chandarua panapo mbu, ndivyo walivyo muhimu wajumbe katika kipindi hiki ambacho Chama cha Mapinduzi (CCM), kinafungua pazia la mchakato wa ndani wa kuwapitisha wagombea wa udiwani, ubunge na uwakilishi.

Umuhimu wa wajumbe, unatokana na jukumu lao katika mchakato huo –kupiga kura za maoni zinazoamua nani aongoze na hatimaye jina lake liwasilishwe katika vikao vya uteuzi wa wa wagombea ndani ya chama.

Turufu waliyonayo wajumbe, ndiyo inayosababisha vikumbo vya wagombea, wakitumia mbinu mbalimbali kuwajengea ushawishi ili wawachague na hatimaye wapewe ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho, wengi wakiamini ukipishwa na CCM unakuwa na nafasi kubwa kuikaa nafasi unayosaka.

CCM inatarajiwa kuanza mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu Jumamosi kati ya Jumamosi Juni 28 hadi Julai 2, mwaka huu, hivyo kipindi hiki ndicho lala salama, huku chama hicho kikiwa kimepiga marufuku mikutano ya wajumbe na wagombea.

Kati ya wanaopigana vikumbo, wamo wabunge, wawakilishi na madiwani wanaomaliza muda wao na wanahitaji kurudi tena kwenye vikao vya maamuzi na watia nia wapya wanaohitaji nafasi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, kila mtia nia amekuwa akitumia mbinu yake ili kuwafikia wajumbe ambao nao wamekuwa na ‘mapozi’ kutokana umuhimu wao, wengi wao wakikutana nyakatio za usiku

Dirisha hili linafunguliwa baada ya kesho Ijumaa, Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia Bunge la 12 kwa lengo kulivunja. Mabaraza ya Madiwani yalihitimishwa Juni 20, 2025 na Juni 23, 2025, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alilihutubia Baraza la Wawakilishi na kutangaza kulivunja ifikapo Agosti 13, 2025.

Juni 23, 2025, Dk Emmanuel Nchimbi, katibu mkuu wa CCM alitangaza marufuku kwa wagombea ndani ya chama hicho, kuitisha vikao, warsha, ziara na makongamano na wajumbe watakaopiga kura za maoni.

Marufuku hiyo, ilitangazwa ikiwa ni miezi kadhaa baada ya chama hicho kuweka kibano kwa wagombea hao, kwa kuongeza orodha ya wajumbe wataoshiriki kupiga kura za maoni ili isiwe rahisi kwa ‘kuwalainisha’.

Yote hayo kwa mujibu wa wataalamu wa siasa, yanalenga kupunguza vitendo vya rushwa kuelekea mchakato wa ndani wa chama hicho na kuweka mizania sawa miongoni mwa wagombea.

Licha ya mipango iliyowekwa na CCM, harakati za chinichini za wagombea kukutana na wajumbe zinaendelea kama kawaida na viongozi wanaotetea nafasi zao inakuwa rahisi kwa sababu wanajua wanakopatikana wajumbe na kuwafikia kwa kutumia mbinu zao.

Kwa watia nia wapya inawawia vigumu, hali inayosababisha watumie nguvu za ziada ili kufanikisha mchakato huo, kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi.

Hivi sasa wajumbe na viongozi wa CCM ngazi ya matawi hadi wilaya ndio wamekuwa lulu kwa sababu ndio wanaowajua wajumbe kwa undani na mahali wanakaopatikana, ikiwemo kuwa na mawasiliano yao.

Taarifa ambazo Mwananchi linazo zinaeleza kwa wagombea wapya wanachokifanya ni kutafuta ‘mkeka’ (orodha ya majina ya wajumbe wote) waliorodheshwa katika daftari la mtaa, kata au wilaya.

Ili kulifikia daftari hilo, watia nia kuwatafuta makatibu CCM kata ili kuhakikisha wanapata mkeka huo kwa lengo la kujua idadi na orodha ya wajumbe watakaowawezesha kuibuka kidedea katika mchakato wa kura za maoni.

Orodha ya wajumbe inawarahisishia kazi kwa kuwa imewekwa namba za simu za kila mjumbe, hivyo kuwezesha kupatikana kwake kwa kutumia timu za wapambe wanaowaunga mkono.

Kutokana na hilo, makatibu wa CCM hasa kata wamekuwa kama wafalme katika maeneo yao, kutokana na kuhitajika na kila mtiania wa ngazi ya udiwani na ubunge.

Inaelezwa wajumbe wanaoingia katika mkutano wa kupiga kura za maoni wanaweza kufika hadi 14,000 ay 1, 260 kulingana na ukubwa wa jimbo au kata mtawalia.

Mjumbe mmoja wa Halamshauri Kuu (NEC) aliyeomba jina lake lihifadhiwe, amesema: “Huko chini hali ngumu, kuna vikumbo kwelikweli, makatibu wetu wa wilaya hadi mashina kwa sasa ni watu mhimu kwelikweli kwani wao wana orodho yote ya wajumbe.

“Kwa hiyo, vita ni kubwa na kama unavyojua CCM ni chama kubwa, kila mmoja anautaka udiwani au ubunge. Sasa ni nguvu yako na ushawishi ndio vitaamua.”

Ukiacha maneno kama tupo pamoja, sitakuangusha, hilo limekwisha, yote niachie mimi au umepita, sifa nyingine inayomtambulisha mjumbe ni nguvu ya kura yake katika kipindi cha kuelekea uchaguzi.

Mjumbe ndiye binadamu mwenye cheo cha ngazi ya chini, kisicho mshahara, wala marupurupu, lakini thamani yake inaamua kupatikana kwa viongozi wanaoamua mwelekeo wa Taifa na ambaye thamani yake hupanda ukaribiapo uchaguzi.

Lakini wakati tunaelekea katika mchakato huo, watiania wapya, wabunge na madiwani wanaotetea nafasi za, bila shaka akilini mwao wanakumbuka ule usemi kwamba “wajumbe si watu”, kulingana na kilichotokea katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Katika uchaguzi huo, mmoja watiania ubunge wa Iringa Mjini, Steven Mengele maarufu ‘Steve Nyerere’ alitoa usemi huo kutokana na kilichomtokea katika mchakato huo, alipoambulia kura sita kwenye kura za maoni za CCM.

Alisema wajumbe ukiwaona wamechoka lakini kiroho ni hatari, kwanza baadhi yao wamesoma hadi darasa la saba, lakini wakijikusanya 400 kwa pamoja wanakuwa na akili.

“Wajumbe sio watu, mjumbe anakukumbatia, chakula anakula jioni anakwambia nimeshakupigia kura, sita? Sasa bora mimi wengine wamepata sifuri. Walau wajumbe wa Iringa wamenisitiri kupata sita,” alisema Steve Nyerere.

Januari 19, 2025 katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika jijini Dodoma, chama hicho kilitangaza mabadiliko ya katiba ili kuongeza idadi ya wajumbe kwenye kura za maoni.

Mkazi wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Zuwena Samson amesema licha ya idadi kuongezeka, lakini wajumbe walio wengi wanajulikana na watia nia wanawafuata kwa kutembelea tawi moja baada ya jingine.

Samson amesema: “Ukifika unakutana na katibu wa tawi, yeye anawafahamu wajumbe wake, anakutafutia mmoja baada ya mwingine unakutana naye na kuzungumza naye,” amesema Samson.

Samson anasema wajumbe walio wengi wana akili, kwanza wanaangalia kama ni mwenzao, kwa maana kama mtia nia aliyekuwa nao wakati wa shida na raha na si wa kuhitaji nafasi ya ubunge tu.

“Hekaheka ni kubwa kwenye nyumba za wajumbe, kwanza sasa hawatoki nyumbani kwao, ‘wanaringa’ wanataka wafuatwe.

“Hivi sasa nyumba za wajumbe watu hawakauki kila mtia nia anatuma mtu wake ni wakati wao huu mavuno… ”amesema Samson.

Kwa mujibu wa Samson, hivi sasa wati ania wanakusanya kwa wanaotaka udiwani na ubunge na wale wa viti maalumu, lakini ana imani atakayepiga kura za maoni bado itabaki kuwa siri.

Mkazi wa Bunda mkoani Mara, Charles Edwin amesema wajumbe na viongozi wa CCM hivi sasa wameguka lulu kwa sababu wameshikilia hatima kubwa katika kuamua yupi apenye hatua inayofuata.

“Watia nia wanawafanyia mambo mengi wajumbe, hawana shida. Wakihitaji fedha za kwenda kufanya starehe au wana shida wanatuma ujumbe mfupi wanasaidiwa, ni muda wao,” amesema.

Naye, Njile Maduhu anayeishi mkoani Simiyu amesema katika majimbo na kata za mkoa huo, hivi sasa kila mtia nia anafanya kila mbinu ili kuungwa mkono na wajumbe watakaoamua hatima yake.

“Sasa hivi kila mgombea ana timu ya watu wanaomuunga mkono ambao wanaopita kila kata ili kuwafikia wajumbe na kuzungumza nao.

Hivi sasa wajumbe wana thamani kuliko wakati mwingine, na walivyo wajanja kila mtia nia wanampokea na kumsikiliza pasipo kushtukiwa,” amesema.

Mkazi mwingine wa Mwanza, Anastazia Kapela ameungana na wenzake akisema hivi sasa wajumbe wanajiona wenye thamani na walio wengi wapo makini.

Kapela amesema hawafanyi makosa hasa mabalozi walio wengi ni wapya na hawana makundi na viongozi waliopo madarakani.

Kwa mujibu wa Kapela, wajumbe waliokuwepo tangu zamani wana makundi, kwa sababu walikuwa wananufaika na posho za viongozi waliopo madarakani.

“Washirika wa karibu wa wabunge au madiwani wanapita sasa hivi kila maeneo, wanachokifanya wanakupigia simu ili muonane hata eneo lisilokuwa rasmi katika nyakati mbalimbali ikiwemo usiku wa manane,” amesema.

Related Posts