Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu Juni 25, 2025 iliyofanyika katika Chuo cha Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu cha Sabasaba mkoani Singida, Ridhiwani amesema WCF imekuwa mfano wa taasisi zinazotekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kumlinda mfanyakazi na kukuza usawa kwa makundi yote ya jamii.
“Nitoe wito kwa taasisi nyingine kuiga mfano wa WCF wa kurejesha kwa jamii, iwe ni kwa huduma, vifaa au fursa mbambali,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ameishukuru Serikali kwa kuwezesha watu wenye ulemavu kupata nafasi zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii bila kujali hali zao.
Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk John Mduma amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuanzishwa kwa Fao la Utengamao lenye vipengele vitatu ambayo ni utengamao wa kiafya (medical rehabilitation), utengamao wa ujuzi (vocational rehabilitation), na utengamao wa kijamii (social rehabilitation).
Mkuu wa Chuo cha Sabasaba, Fatuma Malenga amemshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vyuo vipya, pamoja na kuwezesha vijana kupitia mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya mitaji.
WCFni taasisi ya serikali iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura 263, inayolenga kutoa fidia kwa wafanyakazi waliopatwa na madhara kazini, kama vile ajali, magonjwa au vifo. Mfuko huu ulianza rasmi Julai 1, 2015, ukiwa na jukumu la kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi na familia zao kupitia fidia stahiki kwa mujibu wa sheria.
Miongoni mwa mafanikio tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa waajiri na wafanyakazi kuhusu haki zao na wajibu wao, kuongezeka kwa idadi ya wanachama, kuboreshwa kwa mfumo wa usajili na ulipaji wa madai kwa njia ya kidigitali, pamoja na kupunguza muda wa kushughulikia madai ya fidia.
Aidha, Mfuko huo umeweza kulipa fidia kwa wafanyakazi na familia zao, hivyo kuongeza usalama wa kijamii na kiuchumi kwa wahusika. Vilevile, WCF imeendelea kuimarisha mifumo yake ya ndani, kutoa elimu kwa umma na kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kuboresha mazingira ya kazi nchini.