Kigoma. Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kura ya wananchi imepoteza thamani katika chaguzi tatu zilizopita.
Amezitaja kuwa ni pamoja na ule wa Serikali za Mitaa wa 2019, Uchaguzi Mkuu wa 2020 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024 huku akisema hali hiyo imesababisha wananchi wengi kupoteza imani na mchakato wa upigaji kura.
Zitto ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 26, 2025 katika mwendelezo wa ziara yake ya siku sita katika Jimbo la Kigoma aliyoianza Juni 21 na anahitimisha leo.
Lengo la ziara hiyo ni kukiandaa chama hicho na wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Katubuka, Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto amesema wakati chama chake kilipokuwa kikijadili kushiriki au kutoshiriki Uchaguzi Mkuu ujao, wapo wanachama waliopendekeza kutoshiriki kabisa uchaguzi huo.
“Tulikuwa kwenye wakati mgumu wa kufanya uamuzi na wenzetu wengine kwa hoja za msingi walisema hakuna sababu ya kupoteza muda kushiriki uchaguzi bila kufanyika kwa mabadiliko,” amesema Zitto.
Hata hivyo, amesema viongozi wa ACT Wazalendo walijadili faida na hasara za uamuzi huo, wakikumbuka madhara yaliyotokana na ususiaji wa uchaguzi wa Zanzibar mwaka 2015.
Lakini, amesema hatimaye waliamua kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa lengo la kupigania na kulinda kura.
“Tuna mifano mingi duniani ya kujifunza. Mungu ametupa vichwa tuweze kufikiri mbinu za kukabiliana na udikteta, wizi wa kura na matendo mengine yanayopora haki yetu ya uchaguzi. Ndiyo maana tunasema, ‘Oktoba hii, linda kura’,” amesisitiza Zitto.

Amesema ACT Wazalendo haiendi kwenye uchaguzi kusubiri huruma ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kushinda kata au jimbo, bali inakusudia kushinda kwa kura halali.
Aidha, Zitto amekosoa kudorora kwa shughuli za maendeleo katika Jimbo la Kigoma Mjini, akisema CCM imeshindwa kutekeleza miradi iliyoanzishwa wakati Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma–Ujiji ilipokuwa chini ya ACT Wazalendo mwaka 2015–2020.
“Tulileta kampuni kutoka Korea Kusini iliyosanifu mifereji ya kudhibiti mafuriko katika mji mzima wa Kigoma. Kazi hiyo tuliifanya sisi, CCM walichopaswa kufanya ni kutekeleza tu, lakini wameshindwa,” amesema Zitto.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Majengo, Jimbo la Kigoma Mjini, Jumanne Juni 24, 2025, Zitto alibainisha mambo matatu yanayoweza kuinua uchumi wa Ujiji na kumaliza umaskini.
Miongoni mwayo amesema ni Bandari ya Ujiji kufanya kazi kwa ufanisi, ujenzi wa barabara ya Kasulu–Ujiji na kukamilika kwa mradi wa umwagiliaji wa Bonde la Mto Luiche.
“Bandari tumeijenga, mradi wa barabara ya Kasulu nimeacha fedha kutoka Benki ya Dunia, mradi wa umwagiliaji nimeacha fedha zimetengwa. Wameshindwa kusimamia miradi hii iliyokamilika,” amesema Zitto.
Hivyo, kiongozi huyo amewataka wakazi wa Kata ya Gungu kuchangamkia fursa zinazotokana na eneo hilo ambalo linaelekea kuwa mji mpya ndani ya Kigoma kutokana na uwepo wa stendi kuu ya mabasi na mpango wa ujenzi wa stesheni ya SGR.
Naye aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Kigoma–Ujiji, Hussein Ruhava amesema wakazi wa Bungu na Kigoma Mjini wana kila sababu ya kujitokeza kupiga kura, kwani wanatambua umuhimu wa kufanya hivyo.
“Kwa nini nasema haya ndugu zangu? Sisi tumekuwa madiwani tangu mwaka 2015 hadi 2020, wakati wote huo tulihakikisha tunaujenga mji wetu wa Kigoma. Matokeo ya uongozi wa CCM kila mtu anayaona. Sasa sisi ACT Wazalendo tunataka kurudi tena madarakani ili tuendelee kujenga mji wetu,” amesema Ruhava.

Amesisitiza kuwa ACT Wazalendo ina mipango mingi kwa ajili ya wananchi, ikiwemo kumaliza migogoro ya ardhi inayoendelea kuwasumbua wakazi wa Kigoma.