:::::
Waziri Mstaafu wa Balozi Liberata Mulamula, aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa na Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amechukua fomu ya kuwania Ubunge wa viti maalum kundi la Vyuo na Vyuo Vikuu, kupitia Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT).
Mheshimiwa Balozi Mulamula, amechukua fomu hiyo leo, Juni 28, katika Ofisi za UWT, Taifa, zilizopo jijini Dodoma, ambapo amekabidhiwa fomu hiyo na Ndugu Mary Mwanisongole, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Organizationi ya UWT Taifa.
Balozi Mulamula amechukua fomu hiyo, akiwa amemaliza nafasi ya Ubunge wa viti maalumu katika nafasi kumi za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mulamula ni Balozi mbobevu na mahiri ambaye katika utumishi wake, ameliwakilisha Taifa katika Balozi mbalimbali ikiwemo Marekani, huku akipata uzoefu huo tangu wakati wa Mwalimu Julius Nyerere.
Aidha, Balozi Mulamula amekuwa mkufunzi, mshauri na mlezi kwa wanazuoni, wanafunzi na viongozi chipukizi, hasa katika vyuo vya elimu ya juu, na uongozi wavijana wa vyuo vikuu, akitoa msukumo mkubwa kwa wanawake, wasomi na vijana kushiriki kwenye uongozi na taaluma.
Amekuwa msaada mkubwa katika Afrika na Dunia, kwani amehusika katika usuruhishi wa migogoro mbalimbali ya kikanda ikiwemo wa DRC Congo na mingineyo.
Hivi karibuni Liberata Mulamula aliteuliwa na Umoja wa Afrika (AU) kuwa Mjumbe Maalumu kushugulika na kundi la wanawake kuhusu amani na usalama ambapo kwa hapa nchini, pamoja na majukumu mengine aliyonayo ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Benjamin Mkapa.