Hamdi ashtukia jambo Yanga mapema

KUCHEZA mechi nne za mashindano ndani ya kipindi cha takribani siku 11, imeonekana kuwa ni changamoto kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi.

Hata hivyo, kocha huyo amesema anapambana na hali hiyo kwani hana namna ya kufanya zaidi ya kuzicheza mechi hizo na kufanikisha malengo.

Hamdi ameyasema hayo kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Singida Black Stars utakaochezwa kesho Jumapili Juni 29, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mchezo huo uliopangwa kuanza saa 2:15 usiku, utahitimisha rasmi msimu kwa timu hizo ambapo Yanga inahitaji kutetea ubingwa iliouchukua msimu uliopita ikiifunga Azam kwa penalti 6-5 uwanjani hapo.

Akizungumzia mchezo huo, Hamdi ameanza kwa kuipongeza Singida Black Stars kufuzu fainali huku akibainisha kuwa hakushangazwa kuona timu hiyo ikifunga Simba nusu fainali.

“Kwanza nawapongeza Singida Black Stars kufuzu fainali, sikushangazwa na hilo, nilitegemea watakuwa na matokeo mazuri kwa sababu wamebadilisha mambo mengi sana wakijijenga kuwa klabu kubwa, naamini watafanikiwa kwa hilo.

“Singida ni timu nzuri, wameshinda nusu fainali dhidi ya Simba, sikushangazwa na hilo, Hii mechi ni muhimu kila upande.

“Kwa upande wetu huu ni mchezo wa nne ndani ya siku 10, ni ngumu kwetu lakini lazima tucheze.

“Kesho tunafahamu mchezo utakuwa mgumu kwa sababu Singida wana timu nzuri, wana wachezaji wazuri na wamekuja kushinda kama ilivyo kwetu. Utakuwa mchezo mzuri ukizikutanisha timu nzuri,” amesema Hamdi.

Yanga inakwenda kukabiliana na Singida Black Stars ikiwa ni mchezo wa nne kucheza ndani ya siku 11.

Juni 18, 2025, Yanga iliifunga Tanzania Prisons mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kisha Juni 22, 2025 ikaishushia Dodoma Jiji kipigo kama hicho kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar. Juni 25, 2025, ikaichapa Simba 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar. Hizo zote zilikuwa mechi za Ligi Kuu Bara. Kesho Juni 29, 2025 itakuwa zamu ya kukabiliana na Singida Black Stars.

“Unapokuwa katika klabu kubwa kama Yanga ambayo viongozi wamefanya kazi nzuri ya kuleta wachezaji wengi wazuri, kazi yangu ni kufanya mabadiliko ya hao wachezaji, mechi tatu za nyuma nimefanya hivyo,” amesema Hamdi namna anavyopambana kulinda ubora wa kikosi hicho na kukabiliana na mechi mfululizo.

“Najali sana kuhusu wachezaji wangu. Kila mmoja nampa nafasi ya kucheza, hapa tunaye Sheikhan na wengine ambao wamekuwa wakipata nafasi.

“Sitaki kuona nawaharibu wachezaji wangu kwa kuwaweka sana benchi au jukwaani, nafanya yanayowezekana kupata nafasi ya kucheza ili wawe tayari kufikia malengo tuliyonayo ya kushinda makombe,” amesema Hamdi.

Kocha huyo amefichua kuwa, katika fainali ya kesho ambayo amekiri inazikutanisha timu mbili bora, anaamini kuna mstari mwembamba utakaomtenganisha bingwa.

“Kuna jambo dogo ambalo litatenganisha matokeo ambalo kila mmoja analihitaji kuweka tofauti. Inahitajika kazi ya ziada kufanikisha, kwa upande wangu nitafanya juhudi zote kushinda mchezo huu,” amesema Hamdi.

Kesho Yanga ambayo ni bingwa mtetezi wa Kombe la FA, itaikabili Singida Black Stars katika fainali ya michuano hiyo ikiwa ni siku nne zimepita tangu iifunge Simba mabao 2-0 na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Related Posts