Madaktari bingwa Zanzibar wafikia 119

Unguja. Licha ya kuwapo upungufu wa wataalamu wa afya, Wizara ya Afya Zanzibar imesema kuna ongezeko la madaktari bingwa kutoka 75 mwaka 2020 hadi 119 mwaka huu huku juhudi za kusomesha madaktari bingwa zaidi zikiendelea.

Hayo yameelezwa Alhamis Juni 26, 2025 na Mkurugenzi Tiba kutoka wizara hiyo, Dk Msafiri Marijani wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja.

Dk Marijani amesema ongezeko la madaktari limesababisha upatikanaji wa huduma za kibingwa kama vile usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo na matibabu ya mifupa kuimarika kwa kiwango kikubwa.

“Huduma za kibingwa zinapatikana hapa Zanzibar bila ya kuhitaji kusafiri kwenda Tanzania Bara, hatua hii imepunguza gharama kwa wananchi na kuokoa muda,” amesema Dk Marijani

Ameongezea kuwa, vifaatiba na mashine za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo na matibabu ya mifupa zinapatikana katika Hospitali ya Lumumba.

Pia, Serikali inatarajia kujenga hospitali mbili za mikoa ikiwemo Mahonda, Unguja na Wete, Pemba pamoja na jengo maalumu kwa ajili ya huduma za mama na mtoto, ili kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuboresha upatikanaji wa huduma.

Dk Marijani ameeleza kuwa lengo la kuifanya hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya rufaa limefikiwa na sasa Serikali ipo katika ujenzi wa kujenga hospitali kubwa ya rufaa Binguni kwa tiba za kibingwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Wakati huohuo, Naibu Katibu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khalid Masoud Bakar amesema Serikali imejipanga kujenga vyuo vya mafunzo ya amali katika kila wilaya kwa lengo la kukuza elimu ya amali na kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi.

Amesema, Serikali itaweka msukumo mkubwa katika kukuza elimu ya ufundi kupitia ujenzi wa karakana tatu katika kila wilaya, zitakazotumika kufundishia fani mbalimbali za amali.

“Lengo letu si kujenga majengo tu, bali kujenga skuli na vyuo vilivyokamilika, vyenye miundombinu bora na vifaa vya kisasa, ili kutoa elimu bora itakayowawezesha vijana kujiajiri baada ya masomo yao,” amesema.

Akitaja mafanikio yaliyopatikana amesema katika kipindi kilichopita, Serikali imefanikiwa kujenga madarasa 4,810, ambayo tayari yanatumika na wanafunzi wakiendelea na masomo kama sehemu ya kuboresha elimu kwa vitendo.

Related Posts