SMZ yaeleza tatizo wataalamu wa mafuta na gesi, yawaita kuchangamkia fursa

Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar imesema kuwa mojawapo ya changamoto inayoikabili ni namna ya kuimarisha na kuingiza utaalamu wa mafuta na gesi kisiwani ili kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na rasilimali hizo.

Wizara hiyo imesema kuwa licha ya kuchukua hatua mbalimbali, zikiwemo kuwasomesha wafanyakazi na kuwaajiri wataalamu waliobobea katika masuala ya mafuta na gesi, bado sekta hiyo inakabiliwa na upungufu wa wataalamu wa fani hiyo.

Kutokana na changamoto hiyo, wizara imewataka vijana kuchangamkia fursa zilizopo kwa kujifunza na kushiriki kikamilifu katika kuiunganisha Serikali na jamii kupitia sekta ya mafuta na gesi, kwa kuwa ni eneo lenye manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Zanzibar na wananchi wake.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Julai 28, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Zahor Kassim Alkharous wakati akifungua mkutano wa wataalamu wa mafuta na gesi kutoka ndani na nje ya Afrika, kwa niaba ya Waziri mwenye dhamana, Shaaban Ali  Othman.

Amesema, amefurahishwa kuona kuwa waandaji wa mkutano ni vijana kutoka Zanzibar kwa kuungana na vijana na wengine kutoka Afrika wakiwemo Nigeria, Libya na Tanzania.

“Sera za uchumi wa buluu nikuweka msisitizo katika kuendeleza vijana hivyo kupitia mkutano huu tumeona mambo makubwa waliyoifanya kwa kuiletea sifa Zanzibar katika uso wa kimataifa na jambo hili serikali imelifurahia,” amesema Zahor. 

Naibu Katibu huyo, ametoa wito kwa vijana wa kizanzibar kuwa wajasiri katika kuanzisha vitu vyao, pia wajikite katika mafuta na gesi kwani sekta hiyo ina tija na wasiache kujifunza kutoka kwa wenzao walioendelea.

Naye, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Jumuiya ya Vijana katika Sekta ya mafuta na gesi kutoka mataifa tofauti ya Afrika (Yapa), Jaffar Mohamed Hamza amesema lengo kubwa la mkutano huo ni kuonesha teknolojia mpya na utumiaji wake katika mafuta na gesi na kuhamamisha uwekezaji na utalii kisiwani hapo.

Amesema, Jumuiya hiyo ina mikakati ya kushirikisha vijana wa vyuo vikuu katika kutoa elimu juu ya ubora wa sekta ya mafuta na gesi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar, Dk Mwadini Juma Khatib amesema Serikali ina mikakati ya kuwapa moyo vijana hao ili kuona juhudi hizo zinazaa matunda.

Amesema, wao wakiwa wizara yenye dhamana watahusika kutoa ushirikiano kwa lengo la kuona wanawezekeza katika mafuta na gesi kupitia vijana hao waliokuwa tayari kuitangaza Afrika katika sekta hiyo.

 Awali, akizungumza katika ufunguzi mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Rashid Simai Msaraka amesema mkutano huo unalenga kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika sekta ya mafuta na gesi na kubadilishana mawazo kwa kuangazia changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kuzitatua.

Related Posts