Unguja. Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame amewataka wadau wa kupambana na maafa kuongeza juhudi za kutoa elimu ya tahadhari kwa jamii ili kupunguza ongezeko la majanga yanayolikumba taifa, hususan ajali za barabarani.
Akizungumza katika kikao cha wadau cha utekelezaji wa majukumu ya maafa leo, Juni 28, 2025, Makame amesema wadau hao hawapaswi tu kuorodhesha matukio ya maafa, bali wanatakiwa kuwa chachu ya mabadiliko kupitia elimu ya tahadhari.
“Jamii haihitaji tu taarifa, bali inahitaji kueleweshwa, elimu hiyo itolewe kwa kutumia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na hata kwa njia ya ana kwa ana kwa walengwa walioko kwenye mazingira hatarishi,” amesisitiza Makame.
Amesema jitihada hizo zitaongeza utii wa sheria bila kulazimishwa, hususan katika masuala ya usalama barabarani na kusaidia kupunguza ajali zinazopoteza nguvu kazi ya taifa.
Mkurugenzi huyo pia ametaka Jeshi la Polisi kuwa makini zaidi katika kushughulikia viashiria vya ajali kabla hazijatokea.
“Msubirie watu wameshakufa ndiyo mnamnyang’anya leseni, mkishajua anaendesha kiholela, mzuieni kabla ya kuleta balaa. Sheria zitumike kwa wakati,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Msaidizi wa Mkuu wa Operesheni na Mafunzo Polisi, SP Simai Mustafa Nemshi, amesema ajali 58 zimeripotiwa kati ya Aprili hadi Juni 2025, ambapo 46 kati ya hizo zilisababisha vifo vya watu 52, kati yao wanaume 49 na wanawake watatu na kuacha majeruhi 44.
Amesema Mkoa wa Mjini Magharibi ndio ulioongoza kwa kuwa na ajali 17 zilizosababisha vifo vya wanaume 18 na mwanamke mmoja, ukifuatiwa na Mkoa wa Kaskazini Unguja ulioripoti ajali 11 na vifo vya wanaume 13 vilivyotokana na ajali hizo.
Makosa ya barabarani yalifikia 12,547 kwa kipindi hicho, yakihusisha magari 9,932 na pikipiki 2,615. Mkoa wa Mjini Magharibi uliongoza kwa makosa hayo kwa jumla ya makosa 6,122, huku Mkoa wa Kaskazini Unguja ukiwa na 2,693.
Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano na Uokozi kutoka Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Luteni Malik Makame Hussein, amesema ajali 15 ziliripotiwa katika kituo chao, ambapo tano zilihusisha vyombo vya baharini na 10 watoto waliozama wakiogelea.
Katika ajali hizo, watu 19 walipoteza maisha, mmoja wao akiwa mwanamke, huku wengine 16 wakijeruhiwa.
Amesema wataendelea na kampeni za utoaji elimu sambamba na kazi ya uokozi kwenye bandari mbalimbali za Unguja na Pemba, huku wakihamasisha abiria kutokaa pembezoni mwa meli.
Naye ofisa wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi, Rauhia Abdalla Khamis amesema jumla ya ajali 61 ziliripotiwa, zikiua watu watatu, kujeruhi wawili na kusababisha ulemavu kwa mtu mmoja.
Alibainisha kuwa matukio ya ajali za majanga ya moto wa majumbani ziliongoza zikilinganishwa na moto uliotokea maeneo mengine kama vituo vya mafuta na hoteli ambapo nyumba 29 ziliathirika.
Amesema matumizi mabaya ya umeme na ukosefu wa elimu ya usalama wa miundombinu ya umeme, ndiyo chanzo cha ajali hizo, huku jamii ikihimizwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vifaa vya umeme nyumbani.
“Tumeamua kwenda mbali zaidi ya uokozi, sasa tunajiandaa kukinga majanga haya kabla hayajatokea ili kupunguza gharama na maumivu kwa wananchi wetu,” amesema Rauhia.
Wadau wote walikubaliana kuwa hatua madhubuti, elimu kwa jamii na ushirikiano wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama ni muhimu katika kupunguza maafa na kulinda maisha ya wananchi.