Unguja. Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja, licha ya kupongeza hatua mbalimbali za maendeleo wanazozishuhudia, wamemweleza Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohamed Mahmoud, kuhusu changamoto zinazowakabili, huku wakielekeza lawama kwa baadhi ya masheha wanaodaiwa kutozingatia majukumu yao ipasavyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika maskani ya wazee, kupitia programu maalumu ya Kijiwe cha Maendeleo, baadhi ya wazee hao wamesema kuwa kwa sasa Mkoa wa Kusini Unguja una tofauti kubwa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika kipindi cha nyuma.
Katika maskani za Mtendeni na Kizimkazi Dimbani, wazee hao wamesema kuwa Kusini ya sasa si sawa na ile ya miaka iliyopita, wakieleza kuwa maendeleo yaliyopatikana ni ya wazi na yanayoonekana.
Hata hivyo, baadhi yao katika shehia ya Mtendeni Tasani Makunduchi wamesema kinachokwamisha maendeleo zaidi katika eneo hilo ni ubaguzi wa kisiasa huku masheha wakishindwa kufanya mikutano ya kwa ajili ya kujadili maendeleo.
Katika mazungumzo yao na kiongozi huyo wazee hao wamesema ni jambo la kujivunia kwani kwa sasa yapo mambo mengi yamefanyika ndani ya kipindi cha miaka mitano ambayo hawakutegemea kama yangefanyika.
Yussuf Khatib ni mwenyekiti wa maskani ya Kizimkazi Dimbani amesema Kizimkazi ya leo siyo ya miaka iliyopita kwani kuna miradi mikubwa mingi imejengwa kwa kipindi cha miaka minne.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na majengo ya makazi zaidi ya nyumba 100, uwanja wa kisasa wa mpira wenye uwezo wa kuchukua watu 23,000, hospitali na shule.
“Tumenufaika sana na maendeleo tuliyonayo, mathalani katika sekta ya afya, tulikuwa tunaangaika kufuata huduma nje ya Kizimkazi, lakini kwa sasa kuna kituo cha afya cha kisasa mtu hatoki kwenda sehemu nyingine kufuata huduma hizo,” amesema.
Mzee mwingine katika maskani hiyo, Rashid Abdalla amesema hakika wanapongeza maendeleo hayo maana hali inazidi kuwa nzuri kila kukicha.
Katika maskani ya Mtendeni Tasani ambayo ni ya ACT Wazalendo wamedai licha ya kupata maendeleo lakini kuna ubaguzi unaofanywa na baadhi ya viongozi ngazi za chini kwa sababu ya imani za kiitikadi ya siasa ziliziopo katika ukanda huo.
Katibu wa maskani hiyo, Issa Hassan Ameir amesema wanakabiliwa na siasa kali kwa hiyo wanashindwa kupiga maendeleo kutokana na siasa hizo.
Wajumbe wengine walichangia hoja hiyo wakisema hata katika shughuli za kijamii wale wanaoonekana wapinzani wanatengwa na kubaguliwa.
Yahya Mkongo Ali amesema iwapo Serikali ina nia nzuri ya kutaua changamoto hizo wanatakiwa kusimamia kuondoa ubaguzi, kwani viongozi ngazi ya shehia wanawabagua wananchi kwasababu ya tofautia zao za kiitikadi za vyama.
Umasikini mwingine ni wa kujitakia kwa sababu ya ubaguzi, kama kweli tunataka kuleta maendeleo ya kweli basi tushughulikie changamoto hii,” amesema Ali.
Rajabu Rijan Mzee wa maskani hiyo amesema “Hii ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini kuna ubaguzi mkuu na kila wakifika uchaguzi mkuu kuna watu kuumizwa na kupotea.”
Wananchi hao wamesema licha ya kutofanyika mikutano hakuna kamati zinazoshirikiana katika kupanga maendeleo.
“Waondoe utamaduni wa matabaka, jambo hili linatuathiri kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Wazee wa Ukongoroni akiwemo Khamis Haji Mussa amesema kwa muda mrefu walikuwa wakilia na barabara lakini, kwa sasa imejengwa hawahangaiki tena na usafiri kutoka kijini mwao.
“Kwa muda mrefu tuliangaika na barabara hii, ilikuwa ni kazi kutoka huku ukitaka kwenda hata maeneo mengine kwa sababu hakuna miundombinu ya bararabara, lakini leo hii usafiri umeimarika tunashukuru sana,” amesema.
Naye Sheha wa Shehia Ukongoroni, Hassan Makame Hassan amesema kumekuwapo na mabadiliko makubwa katika maeneo yao licha ya changamoto ndogondogo huku akisisitiza kuongeza ushirkiano na jamii husika.
Akijibu hoja na malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohamed Mahmoud amewatoa hofu wananchi hao kuhusu hali ya kisiasa na usalama kuelekea uchaguzi, akisisitiza kuwa dhamira ya viongozi wakuu wa nchi ni kuhakikisha hakuna mwananchi anayenyanyaswa au kuonewa.
“Dhamira ya viongozi wetu wakuu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake bila bughudha. Katika uchaguzi huu, tutaweka mkazo kwenye kuhakikisha haki inazingatiwa na kila mmoja awe na amani,” amesema Mahmoud.
Aliongeza kuwa: “Suala la haki na demokrasia si jambo la kisiasa. Haijalishi unatoka chama gani, huduma ni kwa wote. Siasa si chuki wala uhasama, bali ni mfumo wa kuishi kwa mitazamo tofauti.”
Mahmoud pia amegusia malalamiko dhidi ya baadhi ya masheha, akiahidi kuwa hatua stahiki zitachukuliwa haraka: “Niwatoe hofu ndugu zangu, kuweni na amani. Maendeleo siyo siasa, na kuhusu hao masheha , ndani ya siku chache mtapata majibu. Hatutavumilia uzembe wala ukiukwaji wa maadili.”
Kuhusu maboresho ya kiutawala katika shehia, Mahmoud amesema Serikali iko mbioni kuwaajiri makatibu wa masheha ili kusaidia utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi zaidi.
“Mpango uliopo sasa ni kuwaajiri makatibu wa masheha. Kwa sababu kwa sasa mfumo uliopo si wa ajira rasmi. Baada ya kuajiriwa, makatibu hawa watakuwa watendaji wakuu katika ofisi za masheha na watashiriki kikamilifu katika kazi za shehia,” ameeleza.
Aidha, amesema mfumo huo mpya utamaliza kabisa tabia ya baadhi ya masheha kufanya maamuzi peke yao, kwani makatibu hao pamoja na kamati za shehia watasimamiwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu rasmi.
Katika hatua nyingine, Mahmoud amesema atauagiza uongozi wa wilaya kuhakikisha mikutano ya shehia inafanyika mara kwa mara ili kujadili na kutatua changamoto za wananchi.
“Hatuna sababu ya kuogopa kuwahudumia wananchi. Ni kweli wapo baadhi ya viongozi ambao hawazingatii maadili, lakini sisi tutasimamia uwajibikaji,” amesema.
Amewataka wananchi kuendelea kushikilia misingi ya amani, upendo, mshikamano na ushirikiano, akisisitiza kuwa hayo ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli kwa jamii.