Unguja. Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kuachana na muhali na kushirikiana kwa dhati na vyombo vya dola kuwafichua watu wakubwa wanaoingiza dawa za kulevya.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Maryam Juma Sadala Juni 26, 2025, akizungumza baada ya kushiriki usafi katika Hospitali ya Wagonjwa wa Akili ya Kidongo Chekundu.
Alisema vijana wengi wana ndoto kubwa lakini zinapotea kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, hali inayosababisha Taifa kupoteza nguvu kazi muhimu kwa maendeleo yake.
Shughuli hiyo ilikuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na matumizi na biashara haramu ya Dawa za Kulevya.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa vijana wengi wanatumia bangi aina ya skanka, ambayo ina kiwango cha juu cha sumu hadi asilimia 45.
Alibainisha kuwa kwa mwaka huu pekee, mamlaka zimeteketeza kilo 1,388 za bangi hiyo, tofauti na bangi ya kawaida, yenye sumu kwa asilimia tano.

Rajab Haji Abdallah ambaye ameacha kutumia dawa za kulevya kwa miaka mitatu sasa akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya ambapo kwa Zanzibar imefanyika katika Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo Chekundu Unguja. Picha na Jesse Mikofu
“Tunalo tatizo kubwa sana, vijana wanateketea kwa matumizi ya dawa za kulevya. Zinapoteza nguvu kazi, ndoto na mustakabali wa Taifa. Hii ni vita ya pamoja, tushirikiane kulitokomeza,” alisema Sadala.
Takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 zinaonyesha Zanzibar ina watu milioni 1.8, ambapo vijana ni asilimia 37.
Katibu Mkuu alieleza kuwa mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya imetoa nafasi 10 kwa vijana watakaoamua kuachana kwa hiari na dawa hizo, ambapo watapewa elimu na mafunzo ya ujasiriamali ili kuwasaidia kuanza maisha mapya.
Daktari bingwa wa afya ya akili, Mtumwa Makame Mohamed alisema matumizi ya dawa hizo yanachangia matatizo ya afya ya akili, saratani na hata vifo.
Dk Mtumwa ambaye pia ni daktari mfawidhi wa hospitali hiyo, ameeleza kuwa kwa sasa hospitali hiyo inalaza wastani wa wagonjwa 90 na wengi wao ni vijana.
“Changamoto kubwa ni kwamba, baada ya kutibiwa na kurejea nyumbani, wengi wao hurudi tena kwa sababu hakuna mfumo wa kuwawezesha kupata shughuli maalumu za kufanya,” alisema.
Baadhi ya vijana waliowahi kuwa watumiaji wa dawa za kulevya walieleza hali waliyoipitia na kutoa wito kwa wenzao kuachana na matumizi hayo.
Rajab Haji Abdalla, ambaye sasa ana miaka mitatu tangu aache dawa hizo, alisema ushauri wa wazazi na mazungumzo ya karibu na watoto wao ni njia muhimu ya kuwalinda.
“Vijana wenzangu, acheni kutumia dawa za kulevya. Mimi nilikuwa mtumiaji mkubwa lakini nimepona. Tena naomba waje wapate ushauri na tiba. Hakuna faida, ni hasara tu,” alieleza Rajab.

Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Jang’ombe, Khamis Ahmada Salum, alieleza kuwa hali ya matumizi ya dawa hizo mitaani ni mbaya, hasa maeneo ya mijini, na ameomba kuwepo kwa mkakati maalumu wa kitaifa kushughulikia janga hilo.
“Nipo katikati ya changamoto hizi. Mitaa yetu imejaa matumizi ya dawa za kulevya. Hili ni janga, tukae pamoja tufikiri namna ya kulitokomeza kwa vitendo,” alisema.
Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Suleiman, alieleza kuwa maeneo yenye matumizi makubwa ya dawa hizo huathirika pia kimaendeleo, kwa kuwa vijana hushindwa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi.
Alisisitiza kuwa jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele kuwafichua wauzaji na waingizaji wa dawa hizo.
“Dawa hizi hazilimwi hapa Zanzibar. Hakuna kiwanda, hakuna shamba. Zinapita njia fulani kuingia, kwahiyo lazima tukabiliane na uingizaji kwanza. Tukifanikiwa hapa, tutadhibiti matumizi,” alisema Waziri.