Dar es Salaam. Chama cha Alliance For Change, (ADC), kimemchagua Wilson Elias kuwa mpeperusha bendera kwa tiketi ya chama hicho kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu itakaofanyika Oktoba 2025.
Pia wajumbe wa mkutano mkuu wamemchagua aliyewahi kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Hamad Rashid Mohamed kuwania nafasi hiyo kwa upande wa Zanzibar.
Wilson na Hamad wameshinda nafasi hizo baada ya kukosa ushindani hivyo wajumbe wa mkutano mkuu huo maalumu waliwapigia kura ya ndiyo na hapana na kupita.
Wilson aliyejiunga hivi karibuni na chama hicho akitokea chama Cha Tanzania Labour Party (TLP), baada ya kushindwa kupenya kwenye mchakato kama huo sasa mpango wake umetiki na anasubiria kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), na kuingia kwenye kampeni kushindana na wagombea wa vyama vingine.

Mgombea wa nafasi ya urais Tanzania kupitia chama cha ACT,Wilson Elias akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho,baada ya kuchaguliwa kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi Mkuu.
Wilson na Hamad wametangazwa kwenye mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam, leo Jumapili Juni 29, 2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza. Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, Mtoro Mvunye amesema chama kina wajumbe 200 lakini katika uchaguzi huo, walikuwepo wajumbe152 na idadi hiyo ilikidhi akidi ya kikatiba kufanyika uchaguzi huo.
“Wilson Elias ameshinda kwa kura 135 sawa asilimia 88.8 hivyo namtangaza rasmi kama mgombea wetu wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu lakini pia namtangaza Hamad Rashid mshindi na atakuwa mgombea urais upande wa Zanzibar ameshinda kwa kura 138 sawa asilimia 90.8,” ametangaza Mvunye.
Kwa upande wake, Wilson ambaye kitaaluma ni mwanasheria akizungumza baada ya ushindi huo, amewashukuru wajumbe kwa kumchagua kwa kishindo kuwa mpeperusha bendera wa chama hicho katika uchaguzi mkuu.
“Kikubwa nimependa uhuru na uwazi na demokrasia ya kweli iliyotawala katika mchakato huu na kupatikana mimi kuwa mshindi na Hamad Rashid upande wa Zanzibar,” amesema Wilson.
Amesema mipango yake ni kuhakikisha anakwenda kuwakwamua Watanzania kuondokana na shida zinazowakabili ikiwemo kwenye eneo la uchumi.
Wilson amemtaja Shoka Hamidu Juma kuwa mgombea mwenza wake.
“Chama chetu hakina fedha tumejipanga kuchukua dola, lakini si hivyo tu tunahitaji kupata wawakilishi wengi bungeni ili tunufaike na ruzuku inayotolewa na Serikali,” amesema Shoka.

Mgombea wa nafasi ya urais Zanzibar kupitia chama cha ADC,h
Hamad Rashid akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho,baada ya kuchaguliwa kuwania nafasi iyo katika uchaguzi mkuu.
Naye, Hamad Rashid amesema pamoja na kwamba umri wake umeenda lakini bado anaona ana kibarua kikubwa katika kuleta mageuzi ya kuwakomboa Watanzania.
“Nimechoka lakini akili yangu inafanya kazi, nina akili kubwa katika kutaka kuwakomboa Watanzania na Wazanzibar kikubwa tuungeni mkono safari hii hatuendi kujaribu,” amesema.
Mwenyekiti wa chama hicho, Shabani Itutu amesema baada ya kupata wagombea hao wanaenda kufanya maajabu huku akisema wamejipanga kimipango kwenda kuchukua dola.
“Hakuna chama kinachoweza kutoka kushindana na ADC, kwani chama chetu kina sera nzuri na kimejipanga kwa hoja zenye masilahi na Watanzania ili kuwakwamua kwenye magumu wanazopitia,” amesema Itutu.

Awali, katika mkutano huo chama hicho kilianza na kufanya mabadiliko madogo ya katiba yao ya kubadili rangi ya bendera ya chama hicho sasa zitakuwa tatu badala ya tano zilizokuwa zimepambwa na kukitambulisha chama hicho mbele ya kadamnasi.
Katika mabadiliko hayo yaliyoridhiwa kwa kauli moja, bendera hiyo sasa itakuwa imepambwa na rangi ya machungwa, nyeupe na nyeusi na wameziondoa rangi mbili bluu na nyekundu.
Akifafanua kuhusu rangi ya machungwa, ambayo inachukua nafasi kubwa, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Hassan Mvungi amesema ni ishara ya mabadiliko na matumaini na mwamko mpya dhidi ya chama tawala kwa kuendesha harakati za kistaarabu za kudai haki kwa amani.
Akitaja sababu ya kufanyika mabadiliko hayo, Mwenyekiti wa chama hicho, Shabani Itutu amesema bendera ya chama hicho ilikuwa inafanana na ya vyama vingine na mchanganyo huo wakati mwingine ulikuwa unawakosesha kura.