Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limetangaza kutokea kwa hitilafu kwenye gridi ya Taifa iliyosababisha mikoa mbalimbali nchini kukosa huduma mpaka sasa, huku juhudi za kurejesha zikiendelea.
Katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya mawasiliano na huduma kwa wateja Tanesco makao makuu leo Jumapili Juni 29, 2025, imeeleza kuwa hitilafu hiyo imetokea saa 02:36 asubuhi, kwenye mfumo wa Gridi ya Taifa.
Taarifa hiyo imeeleza kumetokea hitilafu kwenye mfumo wa Gridi ya Taifa ambayo imesababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika mikoa yote inayounganishwa na gridi hiyo.
“Timu yetu ya wataalamu inafuatilia kwa karibu ili kubaini chanzo halisi cha hitilafu hiyo na kuhakikisha huduma ya umeme inarejea haraka,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo Tanesco imeomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza na ina waomba wananchi waendelee kuwa watulivu wakati juhudi za kurejesha huduma zikiendelea.