Aliyeenguliwa kuwania urais ADC kutinga kwa msajili

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Chama Cha Alliance Democratic For Change (ADC) kumpata mgombea urais wa Tanzania na Zanzibar, kada wa chama hicho na aliyewahi kuwa Mbunge wa Mwibara mkoani Mara, Mutamwega Mgaywa amekusudia kukata rufaa kwenda  Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, kupinga mchakato huo.

Msingi wa kuchukua uamuzi huo ni kutaka haki itendeke dhidi ya kitendo anachodai cha kihuni kilichofanywa na uongozi wa chama hicho kumuengua kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kugombea urais wa Tanzania, kwa kunyofoa baadhi ya taarifa zake muhimu zilizojazwa kwa ufasaha na kuwekwa nyingine asizozitambua.


Katika uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili Juni 29, 2025, ukiambatana na  mkutano mkuu maalumu, wajumbe wa chama hicho walimchagua, Wilson Elias kuwa ndiyo mgombea urais wa chama hicho kwa upande wa Tanzania bara  huku mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Hamad Rashid akichaguliwa kugombea urais upande wa visiwani.

Mgaywa aliondolewa kwenye ukumbi wa mkutano huo kinguvu kwa kile kilichoelezwa hakuwa sehemu ya wajumbe halali licha ya kuwa ni  mtia nia wa nafasi ya kuomba ridhaa ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Akisoma taarifa za kuenguliwa Mgaywa kabla ya kuingia kwenye hatua ya kupigiwa kura, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Mtoro Mvunye alisema katika nafasi ya urais wa Tanzania wagombea walikuwa wawili Elias na Mgaywa aliyeondolewa kwa sababu ya kutokukidhi vigezo.

“Fomu yake sehemu nyingine haijajazwa ikiwemo kuweka picha, kutojaza sehemu ya wadhamini 100 ili ikidhi sifa, kwa hiyo tunamuondoa na tutabakiwa na mgombea mmoja ambaye fomu yake imekidhi vigezo,” amesema Mvunye.


Hoja hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa chama hicho, Shabani Itutu ambaye alisema Mgaywa licha ya kwamba alitoa Sh1 milioni kulipia gharama ya fomu hiyo, lakini hawawezi kwenda na mtu ambaye ameshindwa kukaza fomu vizuri.

“Huyu mgombea tukimpitisha anaweza kwenda kutuaibisha mbeleni, halafu tunataka akagombee nafasi ya urais hawezi kujaza fomu, si anaweza kuturudisha nyuma,” amesema

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Juni 30, 2025, Mgaywa amesema tayari ameshaandika barua na muda wowote kuanzia sasa atatinga Ofisi za Msajili wa Vyama Vya Siasa kwenda kupinga mchakato huo, huku akisema ameonewa na alichofanyiwa ni uhuni ambao unapoka uhai wa demokrasia kwenye vyama vya siasa.

“Nimeshakuwa mbunge wa Mwibara mkoani Mara kwa miaka 10, nashindwaje kujaza fomu? Nina akili timamu si mjinga kiasi hicho, kilichofanyika uhuni nimeshaandika barua ya kukata rufaa kwenda kupinga,” amesema Mgaywa.

Mgaywa amesema kitendo cha kuambiwa ameshindwa kujaza fomu amefedheheshwa anataka kwanza wafute maneno hayo kwani hawezi kushindwa kujaza fomu.

“Nyaraka zote ninazo, nakala ya fomu niliyojaza ninayo zote nitawasilisha kwa msajili, siwezi kukubali kudharauliwa namna hii halafu navamiwa na kutolewa kinguvu nje,” amesema Mgaywa.

Amesema alichukua fomu hizo makao makuu ya chama hicho Buguruni na alizirejesha ofisi ndogo za chama zilizopo Zanzibar zimejazwa vizuri na nakala anayo.

“Kilichofanyika ni uhuni wamenyofoa taarifa zangu na kuweka zingine ili kuonyesha kwa wajumbe sijakidhi vigezo,” amesema.

Mwananchi limezungumza na Msajili Msaidizi wa Vyama Vya Siasa, Sisty Nyahoza aliyekuwepo kwenye mkutano huo, ingawa ilipofikia muda wa kuzungumza hakuwepo, ameeleza kusikitishwa na kile kilichotokea huku akimsihi Mgaywa awasilishe ushahidi wake.

“Sijafurahishwa na kile kilichotokea, ninachotaka kusema awasilishe ushahidi wake kwenye ofisi zetu tutalifanyia kazi,” amesema.

Akizungumzia kwa ujumla majibu ya msajili na malalamiko ya Mgaywa, Itutu amesema, “sitaki kuzungumzia tena hilo suala la Mgaywa labda tuzungumzie jambo lingine.”

Related Posts