Dar es Salaam. Wazazi na walezi wanaowapeleka watoto shule za bweni wakiwa bado wadogo wameshauriwa kuwafuatilia kwa karibu katika makuzi yao wakiwa shuleni na wakati wa likizo.
Hatua hiyo ni kuwaepusha na wimbi la vitendo vya ukatili wa kijinsia katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Warda Abdallah katika sherehe za mahafali ya nne ya watoto waliohitimu elimu ya awali Katika Shule ya Kimataifa ya Monti iliyopo Mikocheni.
Aidha, amepiga marufuku suala la watoto kubebwa kwenye bodaboda, akisema ni hatari kwa usalama wao, hivyo yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Kama Serikali tunawakumbusha wazazi umuhimu wa kuwa karibu na watoto wao kwa sababu ukiangalia dunia inavyokwenda, tunahitaji mawasiliano ya karibu kati ya mzazi na mwalimu anayemwangalia mtoto akiwa shuleni, pamoja na kujua wanachanganyika na watu gani wanaporudi nyumbani,” amesema Warda.
Awali, Mkurugenzi Mkuu na mmiliki wa shule hiyo, Fatma Fernandes amesema shule hiyo inapokea watoto kuanzia wenye umri wa mwaka mmoja na kuendelea, kisha kumlea na kumkuza kielimu hadi anapofikisha umri wa miaka mitano ndipo anapoanza darasa la kwanza.
“Kwa elimu ya msingi watoto wanasoma kwa miaka sita. Shule ina matarajio makubwa ikiwemo kujenga miundombinu inayolenga kuunga mkono vipaji vya watoto. Mfano tunajenga ‘swimming pool’ kwa wale wanaopenda kujifunza kuogelea.
Aidha, amesema wamejikita kuhakikisha watoto wanasoma kompyuta kupitia maabara ya kompyuta iliyopo shule hapo.
“Kuhusu matumizi ya AI (Akili Mnemba) hatujaangalia tu kwa mtoto lakini pia tumeangalia kwa mwalimu ili kurahisisha kazi ya ufundishaji. Kwa sasa tuna darasa maalumu kuhusu AI na tumeweka kwenye mifumo yetu ambayo inamsaidia mwalimu kumrahisishia kutengeneza mpango kazi wa masomo.
Mwalimu hatumii tena saa 40 kama zamani, kwa muda mfupi anaweza kutengeneza kila kitu anakwenda darasani na kuwafundisha watoto na kumuelewa,” amesema Fernandes.
Mmoja wa wazazi wenye watoto shuleni hapo, Kaley Milao amesema anaridhishwa na uwezo wa watoto walionesha katika masomo pamoja na kufikiri.