Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema viongozi wana wajibu mkubwa wa kutatua kero zinazowakabili wananchi, migogoro ya ardhi na migogoro ya kiongozi baina ya viongozi, huku akisisitiza kuwa kero za wananchi haziishi na anayesema zimeisha ni muongo.
Mtanda amesema hayo leo Jumatatu Juni 30, 2025 katika hafla ya kumuapisha Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jubilete Win Lauwo aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Juni 23, 2025 akichukua nafasi ya Joshua Nassari ambaye amechukua fomu kuomba ridhaa ya kuwania ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
Amesema nafasi ya Mkuu wa Wilaya inapimwa kwa majukumu matatu ambayo ni kusimamia usalama, miradi ya maendeleo inayoletwa kwenye halmashauri yako na ukusanyaji wa mapato na kushughulikia kero za wananchi.
”Kero za wananchi ni kitu muhimu sana. Kero haziishi bali zinapungua atakayekwambia kero za wananchi zimeisha ni muongo, kwa hiyo ukifanikiwa hili changamoto hii itaibuka, migogoro ya ardhi haiwezi kuisha bali inadhibitiwa na kupunguzwa kwa hiyo kiongozi hodari ni yule anayedhibiti migogoro na kushughulikia kero za wananchi wake,” amesema Mtanda.
Hata hivyo, Said Mtanda amemtaka DC Lauwo ambaye alikuwa Katibu Tawala Magu kwa miaka miwili kabla ya uteuzi huo, kuyavaa kikamilifu majukumu ya nafasi hiyo na kuenea kwenye kiti chake huku akimtahadharisha kutoendekeza urafiki kwenye ofisi ya umma na kuigeuza kuwa kijiwe.

”Nenda uwe jasiri simamia kauli, kawe na msimamo wasije wakasema wewe ni yule DAS (Katibu Tawala) waliyekuzoea. Wapo watu wanakuja ofisi ya mkuu wa wilaya wanasema nakuja kumuona shoga yangu, hapa hakuna shoga wamsubirie saluni.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jubilete Win Lauwo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kuanzia nafasi ya Katibu Tawala, huku akiahidi kwenda kuyaishi maelekezo ya Mkuu wa Mkoa, Said Mtanda.
”Namshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kunipa maneno mazuri nimejaribu kuyaandika ili niwe nayasoma ninapoamka asubuhi. Napenda kuahidi yote uliyoyasema nitayaishi, nawaomba viongozi wenzangu mnipe ushirikiano ili kufanya kazi yangu vizuri,” amesema Lauwo.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge amesema;
“Nichukue nafasi hii kukukaribisha Mwanza, tunayo timu nzuri sina mashaka na wewe kwa sababu siyo mgeni tumefanya kazi wote ukiwa DAS (Katibu Tawala) tunategemea utakwenda kufanya kazi nzuri,” amesema Lushinge.