RC Kheri James amwapisha Sitta, amkabidhi ofisi

‎Iringa. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amemkabidhi rasmi ofisi Benjamin Sitta ambaye ni mkuu mpya wa wilaya hiyo.

‎Makabidhiano hayo yamefanyika mchana wa Juni 30, 2025 katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa iliyopo Mawelewele, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, yakihusisha viongozi wa wilaya, watendaji wa Serikali na wawakilishi wa taasisi mbalimbali.

Hatua hiyo imekuja  baada ya uapisho wa mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Iringa.

‎Akizungumza wakati wa makabidhiano, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Kheri James amesema amekabidhi ofisi hiyo kwa mtu sahihi aliyeaminiwa na Rais na anaamini ataendeleza kazi ya kuwatumikia wananchi.

‎Amesema kipindi chake akiwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, kilikuwa cha kujifunza na kujenga msingi mzuri wa kiuongozi ambao sasa ataendelea nao akiwa mkuu wa mkoa.

‎Katika salamu zake baada ya kupokea ofisi, Benjamin Sitta amesema yuko tayari kutumikia wananchi kwa kushirikiana na viongozi wote na kuhakikisha wilaya inaendelea kusonga mbele kimaendeleo.

‎DC Sitta ameahidi kuwa karibu na wananchi na kusikiliza kero zao, ili kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa kwa wakati na kwa ufanisi.

Related Posts