Wanaodaiwa kuendesha biashara ya upatu waendelea kusota rumande

Dar es Salaam. Washtakiwa watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya kesi ya kuendesha biashara ya upatu na kutakatisha fedha kiasi cha Sh3.6 bilioni, wataendelea kusota rumande hadi Julai 15, 2025 kesi hiyo itakapotajwa.

Washtakiwa hao ni ambao wote ni wafanyakazi kutoka Kampuni ya Mikopo ya Atlantic Micro Credit Limited ni Sultan Mdee (29), Mhasibu na mkazi wa Goba; Frank Tengia (34) Meneja tawi na mkazi wa Mbezi Juu pamoja na Mwiga Mwiga (31) ambaye ni Ofisa Masoko wa kampuni hiyo.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika pia mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Wendy Ishengoma (38) ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo yupo nje kwa dhamana baada ya kufutiwa shtaka la kutakatisha fedha hivyo kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu.

Wendy na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu, kuendesha biashara ya upatu na kutakatisha fedha kiasi cha Sh3.6 bilioni, katika kesi ya uhujumu uchumi 30853/2024.

Leo Jumatatu Juni 30, 2025, kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Wakili wa Serikali, Frank Rimoyi amedai uchunguzi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Rimoy ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa kutajwa.

Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 15, 2025 saa tano asubuhi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, shtaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu, linalowakabili washtakiwa wote wanne, ambapo wanadaiwa kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa makusudi waliongoza na kusimamia genge la uhalifu kwa kufanya biashara ya upatu.

Shtaka la pili ni kuendesha biashara ya upatu, linalowakabili washtakiwa wote,  tukio wanalodaiwa kulitenda  kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Inadaiwa washtakiwa katika kipindi hicho, walifanikisha mpango wa kuendesha biashara ya upatu kwa kutoa ahadi kwa wanachama na kuingia mikataba ya ubia yenye thamani ya Sh3.6 bilioni kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Shtaka la tatu ni kutakatisha fedha, linalowakabili washtakiwa watatu ambao ni Mdee, Tengia na Mwiga.

Washtakiwa wanadaiwa katika kipindi hicho ndani ya Jiji la Dar es Salaam, wanadaiwa kujipatia Sh3.6 bilioni wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la jinai ambalo ni kuendesha biashara ya upatu.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 29, 2024 na kusomewa mashtaka hayo.

Related Posts