BAADA ya kiungo wa Azam FC, Gibril Sillah kuaga kwenye timu hiyo mabosi wake wa zamani tayari wameshaweka sawa nani atakuwa mbadala wake.
Kiungo huyo ambaye aliitumikia Azam ndani ya misimu miwili, majuzi aliandika waraka wa kuagana na timu hiyo, huku taarifa zikidai kuwa anaweza kuibukia kwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga.
Sillah alikuwa na msimu bora uliopita baada ya kufanikiwa kuifungia klabu hiyo mabao 11 akiwa ndiye kinata wa ufungaji kwenye kikosi hicho ambacho kilimaliza msimu wa ligi kikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo.
Kwa ujumla kwa misimu miwili, staa huyo amefanikiwa kufunga mabao 19 baada ya msimu uliopita kufunga mara manane kwenye ligi akiwa mmoja kati ya wachezaji waliofanya vizuri zaidi kwenye timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema mkataba wa kiungo huyo umefika mwisho, lakini kama klabu bado ina wachezaji ambao wanaweza kuzipa pengo lake.
“Kuhusu mbadala? Azam ina mastaa wengi sana kama Abdul Sopu ambaye pia ana kiwango kizuri na hatuna shaka naye kabisa licha ya kuwa hajaonekana uwanjani kwa kitambo kidogo, lakini ni mchezaji mwenye kiwango bora na anaweza kufanya mambo makubwa uwanjani.
“Lakini pia huu ni muda wa usajili na Azam ni timu kubwa itaongeza mastaa ambao wana uwezo mkubwa ili kujipanga na mashindano ya kimataifa na ndani yatakayochezwa msimu ujao, hili ni jambo ambalo mashabiki wanatakiwa kulisubiri,” alisema Zakazi.