Msanii maarufu, Sean “P. Diddy” Combs, ameondolewa hatiani kwenye mashtaka mazito ya kuendesha mtandao wa kihalifu na usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono. Mahakama ilikosa ushahidi wa kumtia hatiani kwenye tuhuma hizo.
Combs, ambaye alikuwa akikabiliwa na mashitaka matano, amepatikana na hatia kwenye makosa mawili madogo ya kuwasafirisha wanawake kwa ajili ya ngono, lakini amesafishwa kwenye mashtaka makubwa ambayo yangemuweka jela kwa miongo kadhaa.
Katika ushahidi uliodumu kwa miezi miwili na kushirikisha mashahidi 34, ilibainika kuwa aliwasafirisha Cassie Ventura na mwanamke mwingine aliyetajwa kama “Jane” kwa ajili ya ngono, lakini majaji hawakuona ushahidi wa kulazimisha au kuwahusisha katika biashara haramu ya ngono.
Kila kosa alilobainika nalo linaweza kuzaa kifungo cha hadi miaka 10 jela. Upande wa utetezi umeomba aachiwe kwa dhamana ya dola milioni moja (sawa na takribani shilingi bilioni 2.6 za Kitanzania), lakini upande wa mashtaka umetaka abaki rumande hadi hukumu rasmi itakapotolewa.