Kwa asilimia kubwa, akili za wabongo ni kama za kushikiwa. Kila siku benki zinatoa elimu, matangazo na ofa ili kuwahamasisha watu kujiwekea akiba. Lakini wabongo wanazikimbia benki hizo na kwenda kuwekeza kwenye “michezo” ya vijumbe mtaani. Wanapodhulumiwa ndipo wanapojikusanya na kuanza kupiga mayowe na kulalamika kwa watu ambao hawawezi kuwasaidia kwa lolote.
Wabongo hushindwa kuyaratibu na kuyaendesha maisha yao pasipo msukumo wa ziada kutoka nje. Kwa mfano mtu atashindwa kufanya kazi kwa bidii mpaka atakaposimamiwa na mkubwa wake wa kazi. Au ukute anachapa kazi kwa nguvu anapomwona mkuu yupo maeneo yale. Taasisi nyingi kama klabu za starehe na makampuni mengi yamekufa baada ya kuachwa yaendeshwe na wasaidizi.
Katika hili ndio unaweza kumwona Mtanzania. Anafanya mambo kutokana na macho ya watu na si kutoka moyoni mwake, kama mtu anayetangaza kufunga kula huku anakula kwa siri. Anaweza kuvaa nguo safi zilizonyoshwa vizuri akingali hajaoga. Tabia hii mimi naiona ni kujidanganya mwenyewe kwani mtu msafi hawezi kujisikia vizuri katika mwili na akili. Atahisi harufu ya jasho lake likiwakera wenzie.
Viongozi wanaoteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi huishi na tabia za kibongo. Mara baada ya kuteuliwa huapa mbele za Mungu na mamlaka kwamba watatekeleza majukumu yao kwa nguvu na akili kama wanavyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Na watapambana kwa hali na mali kwa faida ya watu wote bila kuzingatia itikadi zao. Lakini ukweli ni kwamba wanafanya hivyo kwa sababu wanasikiwa na kutazamwa.
Viongozi wa aina hii wamekuwa wakimchonganisha Rais kwa wananchi wake. Hufikia wakati ambao mwananchi haoni kiongozi wa kumshika, kwani kila atakayemfuata atampa majibu yanayoanana na ya kiongozi aliyeshindwa kumfanyia kazi. Inafikia mahala pa mwananchi kutatafuta namna ya kutoa machungu yake mbele za Mkuu wa Nchi. Ni kwa sababu mkuu ndiye mwenye mamlaka ya kuwashurutisha wateule wake kuwajibika.
Hii ni aibu kubwa kwa viongozi. Ufike wakati kiongozi aone vibaya pale mwananchi anapoulalamikia utendaji wake mbele za mkuu. Ni kitu kama kuchongewa kwa kiongozi ambako kwa vyovyote kutazaa chuki baina yao. Isitoshe maana ya Rais kuteua wasimamizi ni kugawa majukumu ili wasimamie kazi na kumletea ripoti. Rais mmoja hawezi kumfikia kila mwananchi.
Kwa mfano taratibu zote zinapokamilika tayari kwa Uchaguzi Mkuu, halafu igundulike kuwa wapiga kura hawajapatiwa elimu ya kutosha kuhusu mchakato huo. Hapa ni lazima chombo chenye dhamana hiyo kihojiwe kuhusiana na mapungufu hayo. Ruzuku ya elimu haijawahi kuwa tatizo, kinachokosekana hapo ni usimamizi wa shughuli hiyo. Kifupi tunasema viongozi hawakuwajibika.
Au kukithiri kwa rushwa kunakosimamiwa na wagombea au wafuasi wao wanaotoa milungula hadharani. Vitendo hivi vinaweza kulalamikiwa na hata kuripotiwa na wananchi. Iwapo hatua kali zitashindwa kuchukuliwa, Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wanapaswa kutoa maelezo ya kina au kuwajibika. Taifa limewaweka hapo kwa sababu wao ndio wataalamu katika eneo hilo.
Wanaofanya kazi kwa weledi huwa hawasubiri malalamiko ya wananchi. Wala hawafanyi kazi kwa mazoea, bali kwa taaluma.
Hivyo ni jukumu lao kuzivumbua na kuzifisha mbinu zote haramu zinazoweza kuzorotesha mchakato kwa kadiri ya Sheria na kanuni za uchaguzi zinavyoelekeza.
Vinginevyo mchakato utakuwa shakalabaghala na utazipaka matope Mamlaka zao pamoja na Serikali Kuu. Wakati mwingine huwa nafikirishwa sana na mapungufu yanayojulikana kinagaubaga pasi na kuchukuliwa hatua za kukabiliwa.
Katika kila msimu wa uchaguzi kumekuwa na malalamiko ya uchache au umbali wa vituo vya kupigia kura. Hili ni tatizo endelevu kwani hujirudia kila wakati unapojiri. Kama vile haitoshi, kuna tatizo la kukosekana kwa vifaa vya kupigia kura au kucheleweshwa kwa vifaa siku ya uchaguzi.
Tanzania ina rekodi za sensa ya watu na makazi, hivyo inajua wingi na uchache wa watu katika maeneo ya nchi.
Isitoshe kuna daftari la kudumu la mpiga kura linaloonesha idadi ya watu walio tayari kupiga kura katika majimbo.
Sasa changamoto ya uchache wa vifaa vya kupigia kura huwa inanichanganya sana. Tena hili la ucheleweshaji wa vifaa ndio halieleweki, kwani mtu anaweza kupoteza nafasi ya kazi aliyoipambania kwa muda mrefu kutokana na kuchelewa saa ya usaili. Hii sijui imekaaje.
Ni vizuri wananchi wapate majibu baada ya wahusika wenyewe kuhojiwa kabla ya kufikia kutokuiamini Serikali.
Wapiga kura wanaweza kupoteza imani au kuhisi kuwa uchaguzi haukupangwa kuwa huru na wa haki.
Jambo hili linaweza kupunguza ari ya kushiriki katika mchakato wa kupiga kura. Kwa maana ingine ni kuibuka kwa dhana kuwa haki ya kikatiba ya mwananchi kumchagua kiongozi wake imesiginwa.
Ili kuepuka lawama ambazo viongozi wakuu na Serikali wangetwishwa bila sababu, ni vema kuwa na uhakika na wateule wanaokusaidia kwenye mambo nyeti. Kila linapotokea la kutokea, wahusika wahojiwe bayana juu ya kadhia zao ili wananchi wapate majibu sahihi.