Dar es Salaam. Ikiwa imesalia miezi michache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imesisitiza kuzingatiwa kwa maadili ya kisiasa na hali ya utulivu katika kipindi chote kuelekea uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Jumuiya hiyo, pia imetaka Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kuhakikisha inasimamia haki katika mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia kipindi cha kampeni hadi siku ya kupiga kura kuwachagua madiwani, wabunge na Rais.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa CCT, askofu Dk Frederick Shoo wakati wa Mkutano Mkuu wa 32 wa jumuiya hiyo uliofanyika leo Alhamisi Julai 3, 2025 jijini Dodoma.
Ujumbe huo umekuja kipindi ambacho maandalizi kuelekea uchaguzi huo yanaendelea kufanyika, vyama vikiwa katika michakato ya kuwapata wagombea watakaochaguliwa kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi.
Kiongozi huyo wa kiroho amesisitiza kufanyika kwa kampeni zisizo za kuvunjiana heshima bali zinazoweka mbele masilahi ya Taifa na kupinga vitendo vyote vya rushwa ili kuwapata viongozi wanaostahili.
“Uchaguzi ni daraja la amani na maendeleo si chanzo cha mifarakano, jamii idumishe amani, mshikamano na uzalendo wa kila mmoja kwa nafasi yake. Pia, Tume Huru ya Uchaguzi iendelee kusimamia haki kwa kushirikiana na waangalizi wa ndani,” amesema Askofu Shoo.
Amesema jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo ya jamii, hivyo ameiomba Serikali itoe unafuu wa kodi na kutotoza ruzuku kwa misaada inayotolewa na wahisani ili kuboresha ubora wa huduma na kuwafikia wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu Dk Doto Biteko ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan amesema imekuwa desturi ya nchi kuwa na waangalizi wa ndani kwenye uchaguzi mkuu na kuwa ni imani INEC itawaalika waangalizi hao ikiwa ni pamoja na asasi za kiraia.
Dk Biteko amewahakikishia kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na taasisi zote za dini ikiwamo makanisa na zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuwanufaisha watu wengi kote nchini.
Amesema pia inatambua mchango wa taasisi hizo katika kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali duniani wanaoendelea kuisaidia dunia dhidi ya majanga mbalimbali akitolea mfano Taasisi za World Coucil of Churches na World Vision kwa kutoa huduma za kibinadamu duniani kote bila kubagua tofauti zilizopo za dini, rangi, kabila na jinsia.
“Tunawapongeza sana na tunawashukuru sana kwa mchango wenu. Tafiti zinaonesha kuwa taasisi za dini barani Afrika huchangia kati ya asilimia30 hadi 70 ya maendeleo ya sekta ya afya.
“Pia, natambua mchango wa viongozi wa dini Afrika na duniani kote, mfano wa hili ni hayati Baba Askofu Desmund Mpilo Tutu alikuwa kiongozi wa dini mwenye upendo, mpenda haki na amani, ambaye amechangia kutetea haki za binadamu na kupambana dhidi ya ubaguzi, hivyo kusaidia kuleta maendeleo na usawa kwa nchi ya Afrika Kusini na dunia kote,”amesema.
Dk Biteko amesema Rais Samia anapenda kushirikiana na viongozi wa dini kwa kuwa anawaongoza wananchi wenye dini ambao wanaziheshimu, hivyo asingependa kuona haki zao zinanyimwa kwa namna yoyote ile.
“Rais anapenda kufanya kazi na viongozi wa dini na ninyi ni mashahidi, amekuwa akiwaalika ili tuzungumze masuala mbalimbali ya kitaifa, ingekuwa ni mtu anayejifungia ndani na akasema analo jeshi, sheria, Katiba na vyombo vya ulinzi basi nitafanya kazi nadhani hivi ingekuwa ngumu.
“Lakini amesema milango yetu iwe wazi, tuzungumze na viongozi wa dini kwa ajili ya kutafuta mustakabali wa nchi yetu pale tunapodhani hatuendi sawasawa,” amesema Biteko.